Vyama vya upinzani vimeandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa
mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya vyama vinne vya upinzani
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutiliana saini
makubaliano saba ya ushirikiano, kubwa ikiwa kusimamisha mgombea mmoja
katika kila ngazi ya uchaguzi kuanzia sasa.
Tukio hilo lilifanywa na viongozi wakuu wa
NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD jana katika Viwanja vya Jangwani, Dar
es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi wa dini
na taasisi mbalimbali.
Akisoma makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa alianza kwa kueleza historia ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977 ilitengenezwa kwa muundo wa chama kimoja cha siasa
(CCM)... “ilifanyiwa marekebisho mwaka 1992 baada ya kuanza mfumo wa
vyama vingi.
Mwaka 2011 tulianza mchakato wa kuandika Katiba
Mpya, ilipatikana Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi
lakini maoni hayo yameondolewa katika Katiba Inayopendekezwa.”
Alisema kitendo cha kuachwa kwa maoni ya wananchi
yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, kimesababisha athari
katika matukio muhimu ya kidemokrasia.
Akitaja makubaliano hayo, saba aliyosema yana
lengo la kuzaa Tanzania Mpya, Dk Slaa alisema, “Jambo la kwanza ni
kuhusisha sera za vyama vyetu na kuchukua yale yote yanayofanana ili
tumwe na kauli zinazolingana na kufanana kwa Watanzania.”
Alisema jambo la pili ni kusimamisha wagombea wa
pamoja kwenye ngazi zote za uchaguzi kuanzia Serikali za Mitaa,
madiwani, wabunge, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na
Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Tatu, alisema utaratibu wa namna gani vyama
vinavyounda Ukawa vitashirikiana katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na
vijiji mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015, utatolewa na vyama hivyo
katika wakati muafaka na kusambazwa kwa viongozi wa vyama hivyo wa ngazi
zote ili waweze kuutumia kama mwongozo na kufanyia kazi.
Nne, kushirikiana katika mchakato wa kuelimisha
umma kuifahamu na kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa
ambayo haijazingatia maoni ya wananchi badala yake imezingatia masilahi
ya kikundi kimoja cha watu ambacho ni CCM.
Tano, kujenga ushirikiano wa dhati katika mambo yote na hoja zote za kitaifa na zenye masilahi kwa Watanzania.
Sita, kuulinda Muungano bila kuwa na migongano ya
masilahi kama ilivyo sasa na kama inavyojidhihirisha katika Katiba
Inayopendekezwa.
Saba, “kuhimiza na kusimamia ushirikiano wa pamoja baina yetu na
asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania yenye nia ya dhati ya kulinda
na kuenzi Muungano wetu bila kunyenyekea masilahi binafsi ya kikundi,
kabila au itikadi.”
Dk Slaa alisema kwa uamuzi huo wa Ukawa ni wazi kuwa Watanzania watawaunga mkono huku akiwataka wajiandae kuwa na Tanzania Mpya.
Maalim Seif
Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia
ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alisema
msimamo wa Ukawa ni msimamo wa Watanganyika na Wazanzibari, huku
akiwataka wananchi kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa na
kuifananisha na takataka.
“Wamepiga kura kupitisha Katiba peke yao,
wakaikubali peke yao, wakaitangaza peke yao. Eti wameikabidhi Katiba kwa
Rais (Jakaya) Kikwete na Rais wa Zanzibar, sijui hawa viongozi
wameikubali vipi hii Katiba, hakuna kitu pale,” alisema huku
akishangiliwa na wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Maalim Seif alisema theluthi mbili kutoka Zanzibar
haikupatikana na Bunge hilo lilitumia ujanja wa kuongeza idadi ya
wajumbe wawili kutoka Zanzibar, ambao hawakutakiwa kupiga kura kupitia
upande huo wa Muungano.
Profesa Lipumba
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema: “Ukawa ina msingi wa uadilifu, uwazi na uwajibikaji na ndiyo
kiboko ya kupambana na CCM. Kama mnataka rasilimali za nchi yenu kataeni
Katiba Inayopendekezwa. Adui wa nchi hii ni mafisadi ndani ya CCM,
lazima tuwe na mtandao wa mabadiliko nchi nzima. Vijana tufanye mazoezi
ya viungo kwa ajili ya kupambana na mafisadi hawa.”
Aliwataka wananchi kuhakikisha kuwa wanajisajili
katika daftari la Serikali za Mitaa ili kuwachagua viongozi wa vyama
vinavyounda Ukawa... “Naanza kuona mwanga wa kuiondoa CCM madarakani.
Tujenge ushirikiano kwa ajili ya nchi yetu.”
Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema:
“Yaliyotokea leo siyo mapenzi ya Lipumba, Mbowe, Mbatia, Makaidi wala
Nyambabe, bali ni mapenzi ya Mungu. Kama kuna mmoja wetu aliyepo hapa
anayeshuhudia tukio hili huku amenuna … dhoruba limtokee.”
Huku akishangiliwa na umati wa wafuasi wa Ukawa,
Mbowe alisema ni mategemeo yake kuwa viongozi wote waliotia saini
makubaliano hayo, walizungumza kutoka rohoni kwamba wanaungana na wana
nia moja.
Aliwataka viongozi wa chama chake katika ngazi zote, kuhakikisha
wanakubaliana na mapendekezo yanayotolewa na Ukawa na kwamba yeyote
anayeona hataweza aondoke mapema.
“Katika chama chetu hakuna masilahi ya maana
kuliko nchi yetu. Ni marufuku kiongozi wa Chadema kupuuza muungano wa
Ukawa na kama yupo mwenye masilahi binafsi aanze safari mara moja,”
alisema Mbowe.
Aliwaagiza viongozi wa taasisi zote za Chadema,
Bawacha, Bavicha na Baraza la Wazee, kuhakikisha wanafanya kampeni za
kuipinga Katiba Inayopendekezwa nchi nzima kuanzia Novemba Mosi. Aidha,
aliwaomba viongozi wa Ukawa kuhamasisha viongozi wao kuipinga Katiba
Inayopendekezwa.
Mbatia
Mbatia alisema Taifa limeandika historia mpya na
kuwaomba viongozi wenzake ndani ya Ukawa kuaminiana ili Watanzania nao
wawaamini kwa kuwa wanataka kuweka mbele masilahi ya taifa.
Kuhusu Katiba, Mbatia alisema ni maarifa, mwongozo
na inayounda dola hivyo asiwepo wa kuifanyia mchezo. Alitaka Katiba
Inayopendekezwa ikataliwe na wananchi kwa kuwa haisadifu sifa hizo.
“Ukawa wana utulivu wa ndani wa kuwatumikia
Watanzania wote… tuache kuangalia masilahi binafsi. Wakishinda Chadema…
mimi nikubali, akishinda CUF lazima nikubali, hata wakishinda NLD nao
nitakubali lakini na NCCR tukishinda nao waone tumeshinda kusiwepo na
kinyongo kwa kuwa wote tunapigania mama Tanzania,” alisema.
Makaidi
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema
umoja wa wananchi ndiyo utakaowapa nguvu viongozi wa Ukawa na kuongeza
kuwa anaipenda Tanzania na anataka Zanzibar iwe na mamlaka kamili.
“Mungu siyo Athuman wala siyo wa John… Mungu
alijua kupitia misukosuko hii ya Katiba, Ukawa tutaunganishwa. Bahati
hii inaweza isitokee tena, wakati wa ukombozi ni sasa na utakapofika
wakati wa kupigia kura ya maoni tuseme hapana, hapana, hapana na moto…
moto mpaka CCM iungue,” alisema Dk Makaidi huku akishangiliwa kwa nguvu.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi