KAMATI YA ZITTO YATIMUA VIGOGO

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), jana iligeuka ‘mwiba mkali’ kwa watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Ranchi ya Taifa (Narco) na Wizara ya Nishati na Madini, baada ya kuwatimua wakurugenzi na wenyeviti wa bodi kwa kushindwa kutoa maelezo ya kina kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma, uzembe na wizi.

Katika uamuzi wake, kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, Zitto Kabwe iliwatimua watendaji wa TPDC baada ya kushindwa kuwasilisha mikataba 26 ya gesi na mapitio yake kama walivyoagizwa na kamati hiyo mwaka mmoja uliopita.
Huku ‘wakijikanyaga’ kujibu maswali, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael Manda na Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, James Andilile wametakiwa kuwasilisha mikataba hiyo katika kamati ya PAC kesho, baada ya saa za kazi ili kupangiwa siku ya kukutana na kamati hiyo.
Zitto alianza kwa kumtaka Manda na Andilile kueleza sababu za kutowasilisha mikataba hiyo na kujibiwa kwamba mikataba ya Serikali ina utaratibu wake wa kuipata, huku wakisema kwa Kamati ni kupitia ofisi za Bunge.
Walisema kuwa aliyetoa agizo la kutakiwa kwa mikataba hiyo ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Kauli hiyo ilichafua hali ya hewa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini hapa na kumlazimu Zitto na Makamu wake, Deo Filikunjombe kueleza kuwa Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inaruhusu kamati kupata taarifa yoyote ile.
“Taarifa ambazo zinaweza zisifike katika kamati ni zile zinazohusu mambo nyeti ya usalama wa nchi. Hata hivyo, taarifa hizo zinaweza kufika katika kamati, lakini akaonyeshwa mwenyekiti tu. Mnajua tunaweza kuwapa adhabu kali kwa kuinyima kamati nyaraka na kuizuia kufanya kazi,” alisema Zitto.
Licha ya onyo hilo, Manda na Andilile kwa nyakati tofauti walijitetea kuwa nyaraka hizo za mikataba ya gesi zipo, lakini hawakwenda nazo katika kamati hiyo, huku wakirejea kauli yao kwamba kiutaratibu zinatakiwa kupitia ofisi za Bunge.
“Tunataka kujua huo utaratibu mmeutoa wapi kwamba nyaraka zikitakiwa na kamati lazima zipitie katika ofisi ya Bunge. Mwaka umepita na hamjaleta nyaraka hizo. Sasa kama nyaraka anazo Profesa Muhongo mbona hamjaja naye hapa hata na Katibu wake (Maswi) Eliakim,” alihoji Filikunjombe.
Akijitetea, Manda aliomba kamati kutowachukulia adhabu kali na kuahidi kuziwasilisha nyaraka hizo kama walivyoagizwa.
Katika hatua nyingine, PAC ilieleza ubadhirifu wa maeneo matatu unaodaiwa kufanyika Narco na kusababisha kupotea zaidi ya ng’ombe 360 ndani ya miezi mitatu na kukwama kwa ujenzi wa machinjio ya kisasa.
Wakati ubadhirifu huo ukielezwa, Narco iliwasilisha ombi katika kamati hiyo ikiomba Sh17 bilioni serikalini kwa ajili ya kuongeza mtaji wake.

Akitoa maagizo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Narco, Salum Shamte, Filikunjombe alisema kamati yake haijaridhishwa na maelezo ya kampuni hiyo na kuipa wiki tatu iwe imetoa majibu ya maeneo hayo matatu, ili kujua hatua zinazoweza kuchukuliwa.
“Sisi kama kamati hatuwezi kuiagiza Serikali iwape fedha nyingine. Kwanza hamkopesheki, kwa hali halisi, mkipewa Sh17 bilioni mnazozitaka nazo zitapotea kama hizo nyingine. Tunakwenda kusema bungeni kwamba msipewe hata shilingi mpaka mtakapobadilika,” alisema Filikunjombe.
Alisema watawasiliana na msajili wa Hazina kujua hatua za kuchukua kwa sababu wamebaini kuwa shida ya Narco ni menejimenti.
“Pia umri wa kustaafu ni miaka 60, lakini hapa tunaona Mkurugenzi Mtendaji wa Narco (Dk John Mbogoma) ana miaka 61. Mtueleze kwa nini anaendelea kuwepo kazini wakati umri wake wa kustaafu ulishapita,” alisema.
Pia alisema katika kipindi hicho cha wiki tatu watawasiliana na msajili wa Hazina, ili kujua kama mwenyekiti wa bodi (Shamte), anastahili kuendelea kushika nafasi hiyo.

Wizara ya Nishati
Kutokana na Wizara ya Nishati na Madini kutokuwa na maelezo ya kuridhisha kuhusu fedha za kulipa matangazo ya bajeti ya wizara hiyo katika vyombo vya habari, Zitto aliagiza Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa malipo hayo.
Katika maelezo yake, Maswi alifafanua Sh400.65 bilioni kati ya Sh648 bilioni ya fedha za maendeleo zilivyotumika kugharimia mpango wa dharura wa umeme pamoja na deni.
Pia alieleza utaratibu wa ulipaji wa madeni wa TPDC kwa kampuni za Songas na Pan Afrika.


Chanzo: Mwananchi