MELI YA MV VICTORIA YANUSURIKA KUZAMA

Meli ya mv victoria inayo fanya safari zake kati ya mikoa ya mwanza na kagera katika ziwa victoria imenusurika kuzama karibu na bandari ya kemondo nje kidogo ya mji wa bukoba tukio ambalo limesababisha meli hiyo kushindwa kuendelea na safari yake.

Baadhi ya abiria waliokuwa wanasafiri na meli hiyo kutoka mjini Bukoba kwenda mwanza wamesema meli hiyo imekuwa ikipata hitilafu za mara kwa mara bila kuchukuliwa hatua na kwamba katika safari ya jana meli hiyo iliondoka mjini bukoba saa tatu usiku lakini ilizima mara tatu ndani ya maji na hivyo ikachelewesha safari ya meli hiyo ambayo ilifika katika bandari ya kemondo saa tisa usiku na kuleta usumbufu na wasiwasi kwa abiria waliokuwa wanasafiri na meli hiyo.

Kwa upande wake nahodha wa meli hiyo John Mwita amesema meli hiyo ilipata hitilafu kutokana na usukani kuwa mbovu hali ambayo ilisababisha meli hiyo kuzimika mara kwa mara na kwamba tayari kampuni ya huduma za meli imeagiza vipuri kwaajili ya matengenezo ya meli hiyo ambayo inatarajiwa kuendelea na safari baada ya matengenezo kukamilika ambapo meneja wa bandari ya kemondo joashi miso amesema meli hiyo ilikuwa na abiria zaidi ya mia nne na hamsini na tani mia moja na hamsini za mizigo na amewataka abiria kuwa watulivu wakati taratibu za kutatua tatizo hilo zikiendelea.

Kufuatia tukio la kukwama kwa meli hiyo ya mv victoria katika bandari ya kemondo, wengi wa abiria wa meli wakiwa na hasira walifunga barabara kutoka mjini bukoba kwenda muleba inayopita karibu na bandari ya kemondo kama njia ya kushinikiza uongozi wa bandari kuwarudishia nauli ili waweze kuendelea na safari yao kwa njia ya barabara ingawa baadae jeshi la polisi mkoani kagera lilifanikiwa kudhibiti hali hiyo na kuruhusu magari kuendelea na safari zao.