Uongozi wa Simba, umewatimua kambini nyota wake watatu, Shaaban
Kisiga, Amri Kiemba na Harun Chanongo baada ya wachezaji hao kucheza
chini ya kiwango katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Uamuzi huo wa kuwatimua kambini nyota hao
ulipatikana baada ya kufanyika kikao cha kamati ya utendaji ya Simba
jana mkoani Mbeya ilipo timu hiyo inayotarajiwa kurudi leo jijini Dar es
Salaam baada ya juzi kuikabili Prisons na kutoka sare ya bao 1-1 kwenye
Uwanja wa Sokoine.
“Pia benchi la ufundi la Simba limepewa mechi
tatu, wakishindwa kufanya vizuri yatafanyika mabadiliko kwani mwenendo
wa timu ni mbaya,” kilisema chanzo chetu cha habari ndani ya Simba.
Naye kocha Patrick Phiri wa Simba akizungumzia
mwenendo wa timu yake ambayo imetoa sare tano katika mechi tano za Ligi
Kuu ilizocheza msimu huu alikiri wachezaji wake kucheza chini ya kiwango
katika mechi dhidi ya Prisons hasa kipindi cha pili.
Simba inajiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.