WAJUMBE WAAFIKIANA KUHUSU HOMS

Mazungumzo ya amani kuihusu Syria yanayoendelea mjini Geneva yanatarajiwa kuingia siku ya nne hivi leo Jumatatu, ili kujaribu kuyajibu maswali makubwa ya kisiasa kama vile sala linalozua utata la kukabidhi madaraka.

Lakini mazungumzo ya leo yataangazia pia maswala ambayo hayajapata suluhu kama vile kuruhusu misafara ya magari yanayobeba misaada ya chakula kuingia maeneo yaliyozingirwa namajeshi ya serikali katika mji wa kale wa Homs. Hapo jana Jumapili ujumbe wa serikali ya Syria katika mazungumzo hayo ulikubali kuwaruhusu watoto pamoja na wanawake kuondoka katika mji huo.

Akitoa hakikisho hilo Naibu waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Syria Faisal Mikdad alisema kuwa serikali ya Syria iko tayari kuwaruhusu watoto pamoja na wanawake kuondoka akisema kuwa Serikali iko tayari kuwapokea na kuwapa misaada ya madawa, makao na mahitaji mengine ya kimsingi ikiwa makundi ya wapiganaji ambayo aliyataja kuwa 'magaidi' yatawaruhusu kuondoka.

Na katika hatua muhimu ya kuleta afueni katika mji huo wajumbe wa upinzani wamesema kuwa wapiganaji waliopo eneo hilo wataweka silaha chini kuruhusu misaada ya kibinadamu iwafikie maelfu ya raia.

Lakini baadhi ya viongozi wa upinzani wameelezea tashwishi kuhusiana na pendekezo hilo la serikali na kutaka hakikisho kwamba hakuna mtu atakaye kamatwa na kuzuiliwa. Mjumbe kutoka barazala kitaifa la upinzani nchini Syria Obeida Nahas amesema hatua hiyo ni muhimu. "Hii ni hatua muhimu ikiwa itaruhusiwa kufanyika.

Utawala haukutilia maanani kuruhusu hili mwanzoni, ulitaka orodha ya raia na watu waliojihami ndani ya mji wa kale wa homs swala ambalo kwa kweli haliwezekani ikiwa tunataka watu hawa waondoke. Lakini natumai watawaruhusu kuondoka. Nina maana ya raia waaruhusiwa kuondoka ikiwa wanataka." anasema Obeida Nahas.

Lakini taarifa kutoka mji wa homs zinasema kuwa raia wanafahamu kinacho endelea katika mazungumzo ya mjini Geneva lakini hawana imani katika serikali.

Mmoja wa madaktari wanaotoa huduma za matibabu kwa raia katika maeneo ya mashinani aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Abu, amesema raia hawana imani katika serikali. "Wanafahamu, lakini kuna kitu muhimu-hawataondoka hadi pawe na hakikisho kwamba hawata kamatwa baada ya kutoka maeneo yaliyozingirwa. Tunahitaji hakikisho kutoka kwa utawala au umoja wa mataifa au shirika la msalaba mwekundu kutoa mwanya salama kwao.

Watakapo ondoka maeneo yaliyozingirwa tunapaswa kuhakikisha kuwa hawakamatwi" anasema Abu.

Mpatanishi wa umoja wa mataifa Lakhdar Brahimi amechangamkia hatua hiyo ya kwanza muhimu iliyopigwa katika mazungumzo hayo akisema kuwa ingawa hapajakuwa na makubaliano kuhusu swala la kuachiliwa huru mahabusu, pande zote zitarejea kwenye meza ya mazungumzo hivi leo Jumatatu.