MWANAMKE APEWA KICHAPO KWA KUCHELEWA KUPOKEA SIMU YA MUMEWE

MWANAMKE mkazi wa Kata ya Lubaga, Sophia Haji (22) Manispaa ya Shinyanga anadaiwa kupigwa na mumewe na kusababishiwa majeraha makubwa kwa kile kilichodaiwa alichelewa kupokea simu ya mumewe.

Polisi inamsaka mwanamume huyo,Daniel Daud ambaye kutokana na kipigo, mkewe alitokwa na damu nyingi sehemu za siri. Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema wanamtafuta mtuhumiwa afikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Kwa upande wake, mwanamke huyoaliyelazwa Hospitali ya Mkoa Shinyanga, aliwaambia waandishi wahabari kwamba alipigwa kutokana na kuchelewa kupokea simu ya mumewe wakati akivuka ng'ambo ya barabara.

"Nilipofika nyumbani mume wangu alianza kunipiga," alisema.

Alisema alijitetea kwa mumewe, lakini hawakuelewana, na zaidi alimtuhumu kuwa ana uhusiano na mwanamume mwingine. Kwa mujibu wa Sophia, mumewe alimfungia ndani siku mbili huku akiwa na majeraha pamoja na kumnyima chakula.

"Mimi nilichelewa kupokea simu ya mume wangu kwa sababu nilikuwa navuka barabara ili kujiepusha na ajali, nilikuwa na wifi yangu mdogo, lakini nilivyofika nyumbani mume wangu akawa mkali wala hakunielewa na kuanza kunipiga," alisema.


Alisema wifi yake alimtetea, lakini mumewe aliendeleza kipigo. Alisema baada ya kipigo hicho kuzidi, wifi yake alipiga kelele na majirani walifika kuamua ugomvi huo.

Alisema ilipofika usiku, alihisi maumivu makali mwilini akamweleza mumewe ambaye hakumsikiliza, zaidi ya kumfungia ndani siku mbili. Anna Gilbert ambaye ni rafiki wa mwanamke huyo, alisema baada ya kukaa siku mbili bila kumwona, siku ya tatu aliamua kwenda nyumbani kwake na hakumkuta mumewe.

Alisema alisikia sauti ya mtu anayelia ndani na alipochungulia, alimuona yuko mahututi na alichukua jukumu la kumpeleka hospitali. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dk Fredrick Mlekwa alikiri kumpokea mgojwa huyo.

Alisema alimfanyia matibabu katika vidonda vyake, ambavyo vilikuwa vinatoa usaha na alikuwa na majeraha sehemu za mapajani.