Siku ya Jumanne, Shirika la utozaji ushuru nchini Kenya KRA ilitangaza kuwa mapato yote watakayoshinda wanariadha, ikiwa ni pamoja na wachezaji wa soka nje na ndani ya nchi ni sharti itozwe ushuru kuanzia mwezi huu.
Lakini wanamichezo hao ambao huchagia kiasi kikubwa cha mapato yao katika uchumi wa taifa, wametishia kususia mashindano yote ya kimataifa ikiwa serikali itaendelea na mpango huo wa kuwatoza ushuru.
Wanariadha hao wamesema fedha wanazopata sio nyingi kwa huwa hawashindi hela kila mwezi na huenda ikawachukua zaidi ya miaka mitano kujiinua tena ikiwa serikali itawatoza ushuru.
Wakiongea mjini Eldoret, Magharibi mwa Kenya wanariadha hao, wakiongozwa na mbunge wa Cherangani ambaye pia ni bingwa wa zamani wa mbioza Boston Marathon Wesley Korir, wanariadha hao wanadai kuwa KRA haina mfumo dhabiti wa kubaini kiasi cha fedha walizoshinda wanariadha, kwa sababu shirika hilo halija orodhesha mbio walizo shiriki na kiasi cha fedha walizoshinda.
Mwaka wa 2012, wanariadha kadhaa akiwemo mshikilizi wa rekodi ya dunia wa mbio za mita mia nane kwa upande wa wanaume David Rudisha, bingwa mara mbili wa dunia wa mbio za Marathon Abel Kirui, walikabithiwa nyaraka na KRA kuwataka kulipa malimbikizi ya kodi inayokisiwa kuwa mamilioni ya madola.
*SUNDERLAND YAIBANDUA MAN U*
Manchester United, kwa mara nyingine tena ilikiona cha mtemakuni pale ilipobanduliwa nje ya kinyanganyiro cha kuwania kombe la Ligi maarufu kama Capital one na timu inayoshikilia nafasi ya pili kutoka mkia kwenye msururu wa ligi kuu ya Premier, Sunderland.
United ililazimika kuyaaga mashindano hayo baada ya kushindwa kupitia mikwaju ya penalti na Sunderland.
Baada ya muda wa kawaidia United ilikuwa ikiongoza kwa goli moja kwa bila, lakini kuwa walipoteza mechi ya awamu ya kwanza kwa magoli mawili kwa moja, mechi hiyo ilibidi kuongezwa dakika thelathini zaidiza ziada.
Katika muda huo wa ziada Sunderland nusura ifuzu moja kwa moja lakini sherehe hizo zilikatizwa baada ya dakika moja pale United iliposawazisha kupitia kwa nyota wake Chicharito, na hivyo kufanya timu hizo mbili kutoshana nguvu ya jumla ya magoli matatu kwa matatu bada ya dakika mia moja na Ishirini.
Mechi hiyo iliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti na kwa mara ya kwanza, makipa wa timu hizo mbili waliokoa mikwaju kadhaa.
Kwa Ujumla mikwaju saba ziliokolewa au kupigwa nje na hivyo Sunderland kujikatia tikiti ya fainali dhidi ya Manchester City kwa magoli mawili kwa Moja.
Fainali ya kombe hilo itachezwa tarehe mbili Machi mwaka huu katika uwanja wa Wembley.
*KATIKA USAJILI*
Ombi la Manchster United la kutaka kumsajili nyota wa Chelsea Juan Matata imekubalika.
Ripoti zinasema United imetumia takriban kitita cha pauni milioni 37 kumsajili mcheza kiungo huyo wa Chelsea.
Mata mwenye umri wa miaka 25,anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu baadaye hii leo, kabla ya kukamilisha usajili huo.
Mchezaji huyo kutoka Uhispania anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka minne na nusu na klabu hiyo iliyo na makao yake katika uwanja wa Old Trafford.
Mata ambaye aliichezea Chelsea, mechi 32, aliwaaga wachezaji wenzake na wakufunzi wa Chelsea katika uwanja wao wa mazoezi wa Cobham siku ya Jumatano.