Aidha, mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernesti Mangu, ametuma timu maalum kutoka makao makuu ya jeshi la Polisi inayohusisha kamisheni ya Oparesheni, Upelelezi na Intelijensia kwenda kuongeza nguvu katika juhudi zinazofanyika na ngazi ya mkoa kuhakikisha kwamba, jambazi huyo anakamatwa upesi ili kuondoa hofu kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Jeshi hilo, Mnamo tarehe 26 Januari, 2014 majira ya saa 12.00 asubuhi huko katika kijiji cha Mogabiri jambazi asiyefahamika kwa jina aliwaua kwa risasi Zakaria Mwita na Erick Maranya baada ya kukutana nao njiani.
Siku hiyo hiyo, saa 4:00 usiku, katika kijiji hicho hicho, jambazi huyo alimuua Robert Kisiri miaka 45 baada ya kuvamia Grocery inayomilikiwa na Chacha Ryoba na kumjeruhi mtu mwingine mmoja.
Tarehe 27 januari, 2014 saa 11:30 alfajiri kijijini hapo, jambazi huyo alifanya mauaji tena kwa kumpiga risasi David Matiko mwenye umri wa miaka 39 na kumpora simu yake aina ya Nokia.
Katika tukio hilo, pia, alimjeruhi Machungu Nyamahemba miaka 19 ambaye bado amelazwa katika hospitali ya Tarime kwa Matibabu.
Siku hiyohiyo ya tarehe 27 Januari, 2014 majira ya saa 2:00 usiku katika kijiji cha Nkende, jambazi huyo alimuua kwa kumpiga risasi Juma Nyaitara miaka 30.
Baada ya kufanya mauaji hayo, jambazi huyo aliwapora simu zao za mkononi Chacha Magige na Masero Marigiri wote wa kijiji cha Nkende.
Usiku wa kuamkia tarehe 28 Januari, 2014, jambazi huyo aliendelea kuua watu wengine watatu ambao bado majina yao hayajafahamika.
Mtu mmoja alipigwa risasi wakati akiendesha pikipiki katika kijiji cha Nkende nawengine wawili waliuawa baada yakukutwa na jambazi huyo wakiwa wanatengeneza gari lililokuwa limewaharibikia katika kijiji cha Mogabiri na kuondoka bila kuchukua chochote wala kuwapekua.