UPINZANI WAUNGANA A.KUSINI

Chama rasmi cha upinzani nchini Afrika Kusini,(Democratic Alliance) kimemtangaza Dr Mamphela Ramphele ambaye pia alikuwa mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi kuwa mgombea wake wa uchaguzi mkuu mwezi Aprili.

Bi Ramphele, aliyekuwa mwandanani wa mpigania uhuru Steve Biko, aliunda chama chake cha kisiasa cha Agang mwaka jana.

Kiongozi wa chama cha Democratic Alliance, Helen Zille alisema hakuna mwanasiasa mwingine ana uwezo wa kutawalanchi hiyo kama Bi Ramphele.

Muungano huo uliotarajiwa kuundwa tangu zamani, utashuhudia Dr Ramphele aliyekuwa afisaa mkuu mtendaji katika benki ya dunia na kiongozi wa chama cha Agang South Africa- akiwa kinara wa muungano na mgombea wake mkuu katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Aprili.

Tangazo la Muungano huo kati ya vyama hivyo viwili na chama cha Mamphela Ramphele - Agang South Africa - umesifiwa na wafuasi wake kama mwamko mpya wa kisiasa nchini humo.

Baadhi wanasema hii ni dalili ya chama cha DA - kilichoshinda 16% ya kura katika uchaguzi uliopita kuwa katika hali ngumu kisiasa, na pia bado kinaonekana na wengi kama chama cha wazungu.

Dr Ramphele - msomi wa hali ya juu na mkurugenzi wa zamani katika benki ya dunia, licha ya kusifika kwa maoni yake, angali kupata ufuasi mkubwa miongoni mwa wananchi wa taifa hilo.

Chama chake Agang South Africa, kinaangazia zaidi maswala ya elimu, mageuzi ya mfumo wa uchaguzi na ustawi.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Cape Town, Dr Ramphele alisema kuwa kifo cha Mandela mwezi Disemba kilibadili siasa za nchi hiyo na kusema ni wakati sasa wa kuweka hai ahadi za mwaka 1994 - mara ya kwanza ambapo nchi hiyo ilifanya uchaguzi huru.