Akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa nakala za vitabu vya hotuba hizo iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema uamuzi wa kuchapisha hotuba hizo umechangia historia ya Tanzania na kubainisha kuwa hotuba za Rais si zake wala mali yake binafsi.
Rais Kikwete alisema Rais huyo mstaafu, amefanya jambo kubwa sana katika historia kwa sababu alichokuwa anafanya wakati wa utawala wake ni historia ya nchi na lazima kiwekwe kwenye kumbukumbu kwa ajili ya kuvionyesha vizazi vijavyo.
"Hotuba zitaendelea kuweka kumbukumbu na kuvionyesha vizazi vijavyo mambo yaliyotokea wakati wa urais wako, msimamo wako na wa nchi katika kipindi hicho na hata fikra zako zilizosaidia kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu," alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alimtaka Rais huyo mstaafu kuangalia namna ya kuweka historia ya uongozi wake katika kitabu kadiri alivyoshuhudia miaka 10 ya uongozi wa Tanzania na kusisitiza kuwa bado wanaendelea kusubiri kitabu chake hicho.
Alisema kuna haja kwa wadau mbalimbali wa elimu, hasa wale wenye mapenzi ya kusoma vitabu, kuchukua hatua za kuamsha ari na mapenzi ya Watanzania ya kusoma vitabu ambayo kwa sasa, imepungua kwa kiasi kikubwa.
Kitabu hicho kiko katika machapisho matatu kuonyesha kuwa pamoja na kwamba alikuwa Rais wa miaka 10, lakini kila siku yauongozi wake ilikuwa tofauti na nyingine, hali kadhalika mwezi mmoja mwingine.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amemwapisha Dk Aziz Ponary Mlima kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia na Jaffary Ally Omari kuwa Mjumbe wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Mlima alikuwa Msaidizi wa Rais Mstaafu Mzee Benjamin Mkapa.