JENGO LA TIGO LAZUA TAHARUKI

Hofu na taharuki ya kuporomoka kwa jengo la makao makuu ya ofisi za kampuni ya simu za mikononi ya Tigo zilizoko eneo la Makumbusho jijini Dar es salaam zimesababisha kusitishwa kwa huduma katika jengo hilo kwa dharura kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi na wateja wa kampuni hiyo ili kupisha wataalamu wa uhandisi kufanya uchunguzi wa kina kutokana na uwepo wa madai ya tukio la kutikisika kwa jengo hilo la ghorofa tisa.

Tukio hilo limevuta hisia za taharuki kwa wafanyakazi, wateja na baadhi ya wapita njia karibu na jengo hilo.

Wafanyakazi wa kampuni hiyo walitoka nje ya jengo ambapo meneja chapa wa Tigo bwana William Mpinga amesema taharuki hiyo imetokana na uwepo wa nyufa katika sakafu ya ghorofa ya nne ya jengo hilo ambapo mkutano ulikuwa ukifanyika na kusababisha baadhi ya wafanyakazi kukimbia hovyo na kwamba kampuni hiyo imeamua kusitisha huduma katika jengo hilo kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi na wateja wa Tigo.

Tukio hilo limesababisha baadhi ya majengo na ofisi zilizopo karibu na jengo pia kusitisha shughuli zao huku baadhi ya mashuhuda wakielezea kile walichokishuhudia.

Imeshuhudiwa mojawapo ya ufa ulioko kwa nje ya jengo hilo licha ya kuzuiwa na meneja chapa wa Tigo kuingia ndani kwa ajili ya mahojiano na baadhi ya wahandisi waliokuwa ndani ya jengo hilo kuchunguza ukubwa wa tatizo huku jengo hilo likionekana kuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha ambapo mkuu wa polisi wa wilaya ya Kinondoni Willbroad Mtafungwa akiwaambia waandishi wahabari kuwa wamepata taarifa ya madai ya kutikisika kwa jengo hilo na kuzua taharuki kwa watu waliokuwemo ndani ya jengo hilo.