MAJAMBAZI WAMUUWA MWENZAO KWA RISASI

Watu wanaoaminika kuwa majambazi waliokuwa na silaha za moto, wamemuua mwenzao kwa kumpiga risasi usoni baada ya majambazi hao kujichanganya wakati wakiwa katika harakati za kutoroka.

Habari zilizopatikana jana zilisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:30 usiku eneo la Captown katika Manispaa ya Moshi baada ya jaribio la majambazi hao kupora katika duka la simu kugonga mwamba.

Habari hizo zilidokeza kuwa muda huo wakati mmiliki wa duka hilo, Ramadhan Sauko akijiandaa kufunga duka lake, waliingia watu wanne waliojifanya wateja na baadaye kumtolea bastola. Hata hivyo, mfanyabiashara huyo alianzakupiga kelele za kuomba msaada ambapo mmoja wa majirani aliamua kufyatua risasi hewani ambayo iliwafanya majambazi watatu kukimbilia uchochoroni.

"Wakati wananchi wakijikusanya yule jambazi wanne akakurupuka kutoka kule dukani akakimbilia kuleuchochoroni kwa wenzake na ndipomlio wa risasi ulisikika uchochoroni," alidai shuhuda mmoja.


Inadaiwa majambazi wale waliamini aliyekuwa akiwafuata uchochoroni walikokuwa wamekimbilia kujificha alikuwa ni mmoja wa wananchi waliojitokeza kutoa msaada na ndipo walipompiga risasi. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alipozungumza na wanahabari jana,alisema baada ya kusikika milio ya risasi, alionekana mtu uchochoroni akiwa amejeruhiwa kwa risasi.

Kamanda Boaz alisema baada ya uchunguzi na upekuzi, marehemu alitambuliwa kuwa ni Nicholaus Jacob Mushi (35), akiwa na bastola aina ya Browning yenye namba 043916 ikiwa na risasi nane.

Bastola hiyo imetengenezwa nchini Czech na kusajiliwa nchini kwa namba TZ.TAR 73647.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, kumbukumbu za polisi zinaonyeshamarehemu alikuwa mhalifu mzoefu na alishawahi kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kuvunja na kuiba.

Kamanda Boaz alisema Polisi linaendelea na uchunguzi ikiwamo kuwatafuta watuhumiwa waliofanikiwa kutoroka kabla ya mauaji ya mshirika wao huyo.