MELI YA WANASAYANSI WALIOKWAMA ANTARCTIC WAOKOLEWA

Angalau watafiti 50 waliokuwa wameabiri meli ya Urusi iliyokwama katika bahari ya Antarctic hatimaye wameokolewa.

Meli hiyo kwa jina 'Akademik Shokalskiy' ilikwama kwa siku tisa zilizopita katika bahari hiyo iliyokuwa imejaa theluji.

Ndege aina ya helikopta kutoka katika kampuni moja ya kichina ilifanikiwa kuwaokoa watafiti hao ambao miongoni mwao walikuwa wanahabari na wanasayansi.

Mashine tatu za kusaga theluji zilikosa kuifikia meli hiyo ambayo iliondoka New Zealand mwishoni mwa Novemba watafiti waliokuwa wameiabiri wakiichunguza upya nyayo za karne moja iliyopita za mtafiti Douglas Mawson.

Mawson aliwahi kukwama katika sehemu hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja huku watafiti wake wawili wakiaga dunia wakijaribi kujiokoa.