KITU KINACHOZANIWA KUWA NI BOMU CHAZUA TAHARUKI JIJINI DAR

Tishio la kuonekana bomu laleta hali ya taharuki eneo la Shekilango DSM.

Taharuki imewakumba baadhi ya wapita njia na wafanyabiashara katika makutano ya barabara ya Morogoro na Shekilango jijini Dar es salaam,na kusababisha baadhi ya shughuli kusimama baada ya wapita njia wawili kuona kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono huku baadhi ya askari polisi wakiwa na kazi ya ziada ya kuwaondoa baadhi ya wananchi waliokuwa wakitaka kushuhudia kitu hicho.

Tukio hilo limevutia hisia za watu wengi katika eneo hilo na kukusanyika kwa wingi wengine katika maghorofa yaliyoko katika eneo hilo kwa lengo la kushuhudia badala ya kusimuliwa jambo lililowafanya polisi kuzungushia kamba maalum kwa ajili ya kuwazuia raia kufika katika eneo hilo ambapo watu wawili mtu na mwanaye ndio walioshuhudia.

Baadhi ya askari ambao wanadhaniwa kuwa wataalam wa mabomu kutoka katika kikosi cha kutuliza ghasia Upanga jijini Dar es Salaam walifika katika eneo la tukio na kuanza harakati za kukichukua kitu hicho kinachodhaniwa kuwa ni bomu kwa tahadhari kubwa na baada ya kufanikiwa kukiondoa wakakiweka katika mfuko maalum na kutoweka katika eneo la tukio
itv kiguu na njia hadi kwa kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi wa kinondoni kwa ajili ya kupata uthibitisho kuhusu kitu hicho kinachodhaniwa kuwa ni bomu na kujulishwa kuwa taarifa juu tukio hilo inaandaliwa naa baada ya kukamilika kwake kamanda wa polisi wa Kinondoni Camilius Wambura akaitoa taarifa hiyo.

Kamanda Wambura hakusita kutoa tahadhari kwa wananchi pale wanapobaini kitu ambacho si cha kawaida na cha hatari kwa maisha ya binadamu.


Chanzo: ITV