Kikwete ambaye amesema amepata minong'ono kuwa baadhi ya walioondoka wanarudi kinyemela, amewataka wanaopenda kuishi nchini, wafuatenjia halali.
Suala hilo pamoja na mengine mengi, ikiwemo dawa za kulevya, elimu na Operesheni Tokomeza, aliyasema katika salamu zake za Mwaka Mpya alizozitoa juzi. "Nimepata minong'ono kuwa baadhi ya watu walioondoka wanarudi kinyemela.
Napenda kuwa tahadharisha kuwa wasifanye hivyo. Wanajisumbua bure. Hawatadumu. Ushauri wangukwao ni kuwa kama wanapenda kuishi Tanzania wafuate njia halali za kufanya hivyo," alisema.
Rais Kikwete alisema kukithiri kwa ujambazi katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Mwanza ndiko kulimfanya akatoa uamuzi wa kuanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na mafanikio ya kutia moyo.
Alisema hali ya usalama katika mikoa hiyo inaelekea kuimarika ingawaje ni mapema mno kusema tatizo limedhibitiwa.
Lakini alikemea baadhi ya watu waliokuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria kurudi kinyemela. Kuhusu dawa za kulevya, alisema Serikali yake iko katika hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka ujao wa fedha.
Alisema katika kupambana na biashara hiyo haramu, wanaitazama upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili kuifanya iwe na meno makali zaidi." Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya. Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa kufanya zaidi," alisema Rais Kikwete.
Elimu Alisema mwaka uliomalizika Serikali iliajiri walimu 28,666, lakini hata hivyo bado kuna upungufu wa walimu 57,755 kati yao 20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za sekondari.
Alisema mwaka ujao wataajiriwa walimu wapya 36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000 wa sekondari ili kupunguza pengo lililopo.
Rais alisema walimu wa masomo ya sanaa wapo wengi na tatizo lake linakaribia kumalizwa. Alisema changamoto kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya Sayansi.
Operesheni Tokomeza Rais Kikwete ametangaza kuunda Kamisheni ya Uchunguzi itakayo ongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuchunguza malalamiko juu ya uhalifu na unyama uliofanyika wakati wa Operesheni Tokomeza, Alisema uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu kadhia yote hiyo.
"Makosa yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya kutambuliwa ili wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.
"Alisema ni muhimu kufanya hivyo ili haki itendeke ipasavyo. Aliongeza kuwa mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi.
Rais alisisitiza kuwa ni lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili.
"Ni matumaini yangupia kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe."