JESHI LA POLISI LAWASHIKIRIA ASKARI MAGEREZA KWA WIZI

JESHI la Polisi mkoani Mbeya, linawashikilia watu watano wakiwemo askari Polisi na mwingine wa Jeshi la Magere za wakihusishwa na tukio la kumteka na kumpora mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia zaidi ya Sh milioni 3.7.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi, waliokamatwa ni pamoja na Sajenti Juma Musa (38), askari Magereza Gereza la Ruanda, Mbeya na PC James (32), askari Polisi wa Mbeya.

Wengine ni Mbaruku Hamisi (29), Amri Kihenya (38) na Elinanzi Mshana (29), wote wakazi wa Forest, jijini Mbeya.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Msangi alisema watuhumiwa hao walikutwa na baadhi ya mali walizopora ambazo ni mabegi matatu ya nguo, simu moja ya kiganjani aina ya Samsung na Laptop moja aina ya Samsung.

Alisema vifaa hivyo vilikutwa kwenye gari aina ya Toyota Grand Mark II aina ya GX – 6011835 hukublangeti mbili zikikutwa kwenye buti la gari Toyota Crest GX 100 lenye namba za usajili T 782 BEU.

Alisema tukio hilo la unyang'anyi lilitokea juzi jioni majira ya saa 11:35 katika eneo la Mlima Kawetele Wilaya ya Mbeya Vijijini ambako watu hao walimpora Speedhar Pasupeleti (38) mwenye asili ya Kihindi, mkazi wa Makata wilayani Chunya.

Kamanda Msangi alisema mfanyabiashara huyo akiwa na wenzake wawili kwenye gari aina ya Toyota Pick Up lenye namba za usajili T 756 ABL, alinyang'anywa pesa zaidi ya Sh milioni 3.7 baada ya waporaji kuweka magogo barabarani ili kuzuia magari yasipite.Mbali ya pesa, waliiba pia begi lililokuwa na nguo na vitu mbalimbali baada ya kuwatishia Pasupeleti na wenzake kwa kutumia silaha.

Kutokana na tukio hilo ambalo uchunguzi wake unaendelea, Kamanda Msangi ameitaka jamii kujiepusha na tamaa ya kusaka utajiri wa haraka kwa njia zisizo halali, huku ahimiza watu kufanya kazi halali ili kujiingizia kipato.

Katika tukio jingine, Kamanda Msangi alisema, siku hiyo hiyo mchana, mtoto wa kike mwenye umri wa miezi 10 alikufa katika ajali ya gari iliyotokea mkoani ikihusisha lori la mafuta aina ya Scania na basi dogo aina ya Toyota Hiace.

Watu 13 walijeruhiwa katika ajali hiyo, kati yao tisa wakiwa wanawake.

Alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Hospitali Teule ya Ifisi, Kata ya Songwe, Tarafa ya Bonde laSongwe wilayani Mbeya Vijijini ambapo gari lenye namba za usajiliT 330 ACK na tela lenye namba T 422 ACK aina ya Scania likiendeshwa na Yusuph Fakhi (45) mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam likitokea Mbeya kuelekea Tunduma liligonga gari lenye namba za Usajili T 897 ALH aina yaToyota Hiace.

Alisema gari lililogongwa lilikuwa ikiendeshwa na Musa Hamisi (25) Mkazi wa Iyunga, mjini Mbeya na kusababisha kifo cha mtoto huyo ambaye bado hajafahamika wala wazazi wake.

Alisema majeruhi wawili wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na wengine 11 wamelazwa katika Hospitali Teule ya Ifisi akiwemo dereva wa Hiace na hali zao zinaendelea vizuri. Chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa huku dereva wa Scania akiwa anashikiliwa na Polisi.

Chanzo:Habari leo