*Everton kicheko lakini Aston Villa kilio
Arsenal wamedhihirisha dhamira yao ya kutwaa kombe msimu huu baada ya kuwa adhibu mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur kwa mara nyingine.
Safari hii ilikuwa ni katika hatua ya tatu ya Kombe la FA, ambapo Arsenal walipata ushindi mzuri wa mabao 2-0 dhidi ya timu iliyoonekana kufufuka.
Tangu walipomfukuza kocha wao machachari wa Ureno, Andre Villas-Boas, Spurs walianza kufanya vyema ikiwa ni pamoja na kuwafunga mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England (EPL), Manchester United 2-1 juma lililopita.
Mabao ya Arsenal yalifungwa na viungo wao Santi Cazorla na Tomas Rosiscky baada ya kocha Arsene Wenger kuwaonya nyota wake kutofanya mchezo kwenye michuano hiyo, vinginevyo hangekubaliana nao.
Hata hivyo, Wenger hakuanza na baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza, ikiwa ni pamoja na kumwanzisha kipa Lukasz Fabianski, nahodha anayeelekea kuondoka klabuni, Thomas Vermaelen, kiungo Serge Gnabry huku watu kama Mesut Ozil, Per Metersacker wakiwa benchi japo wengine waliingia baadaye, huku Theo Walcott akiumia tena.
Wakati hali ikiwa hivyo jijini London, huko Ewood Park Manchester City wanaosifika kwa kasi ya kufunga mabao kwa mafuriko walishikwa shati na vibonde wa Ligi Daraja la Pili (Championship), Blackburn Rovers kwa kuwahenyesha ka sare ya 1-1.
City walisubiri hadi dakika ya 45 kupata bao la kwanza kupitia kwa Alvaro Negredo, lakini dakika tano tu baada ya kipindi cha pili kuanza lilisawazishwa na Scott Dann.
Man City walikuwa nusura waage mashindano hayo kama si jitihada za ziada katika dakika tisa za mwisho kuzuia vibonde hao kuwaaibisha, hasa baada ya mlinzi Dedryck Boyata kupewa kadi nyekundu.
Kocha Manuel Pellegrini hakupenda kuwa na mechi ya marudiano kwa sababu tayari Januari hii ana msongamano wa mechi, ikiwa ni pamoja na mechi ya nusu fainali ya Kombe la Ligi (Capital One Cup) dhidi ya West Ham United waliowang'oa Chelsea kwenye robo fainali.
Blackburn ndio waliokuwa washindi wa pili wa kombe hili msimu uliopita na ni miaka 130 imepita sasa tangu walipotwaa kwa mara ya kwanza Kombe la FA, yaani mwaka 1884. 'Mende' waliendelea 'kuangusha makabati' kwani timu ya League One inayohangaika kujinusuru kushuka daraja ya Sheffield United walipowapiga wale wa EPL, Aston Villa kwa bao la Ryan Flynn na kuwatupa nje ya mashindano haya.
Katika mechi nyingine za awamu hiiya Kombe la FA, Barnsley walifungwa 2-1 walipowa karibisha Coventry, Bolton wakawafunga Blackpool 2-1, Bournemouth na Burton mechi yao ikaahirishwa wakati Brighton wakizidi kuwa aibisha Reading kwa kichapo cha 1-0.
Kwingineko, Doncaster walifungwa 3-2 na Steveage, Everton wa Roberto Martinez wakawacharaza Queen Park Rangers wanaofundishwa na Harry Redknapp (QPR) 4-0, Grimsby wakafungwa 3-2 na Huddersfield huku Ipswich wakiambulia sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Preston.