WAWILI WANUSURIKA KUFA BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI KWA SIKU TANO

Watu wawili wamenusurika kufa baada ya kufukiwa na kifusi kwa siku tano katika machimbo ya dhahabu mkoani Geita na kuokolewa wakiwa katika hali mbaya.

Eneo hilo lipo chini ya leseni ya mgodi wa dhahabu wa Geita na shimo hilo lilikuwa likitumika zamani ambapo kwa sasa halitumiki, mara kwa mara vijana waishio katika mji wa Geita na vijiji vya jirani hufika eneo hilo kuchimba ili kuweza kuambulia angalau masalia ya mchanga wenye dhahabu hata hivyo uongozi wa mgodi huo kwa kushirikiana na jeshi la polisi wamekuwa wakijitahidi kuwazuia vijana hao kutofika eneo hilo kwa kuwa si salama.

Daktari mfawidhi katika hospitali ya wilaya ya Geita Adam Sijaona amethibitisha kupokelewa kwa vijana hao amesema hali zao zinaendelea vizuri, ambapo kwa upande wa mgodi wa dhahabu wa Geita wamewataka viongozi na wananchi waishio kandokando ya mgodi huo kuwaelimisha vijana wao kutovamia maeneo hatarishi kama hayo.

Imedaiwa kwamba kuna baadhi ya wanasiasa ndio wanaowashawishi vijana hao kuvamia maeneo ya uchimbaji yasiyo rasmi ili kuweza kujiongezea mvuto kwa wapiga kura ambapo jeshi la polisi limewataka wananchi kutovunja sheria kwa shinikizo la wanasiasa.