MVUTANO WAIBUKA KUHUSU KANUNI BUNGE LA KATIBA

Mwenyekiti wa bunge maalum la katiba Mh Samweli Sitta amelazimika kuliahirisha bunge ili kutoa muda kwa kamati ya kanuni na haki za bunge kukutana kwa lengo la kutafuta tafsiri sahihi ya kanuni ambazo zimeibua mvutano ikiwemo ile kanuni ya 87 kifungu cha pili.

Mvutano huo ulitokana hatua ya mwenyekiti kutaka kutoa ruhusa kwa mwenyekiti wa kanuni na haki za bunge kuwasilisha taarifa yake ndipo Mh Tundu Lisu aliposimama na karatasi aliyodai ni jedwali lilokuwa limeandaliwa kwa lengo la kufanya marekebisho ya kanuni kinyume na utaratibu.

Kutokana na hali hiyo ndipo mwenyekiti alipoamua kuahirisha kikao hicho ili kuruhusu ufumbuzi uweze kupatikana katika kikao kijacho.

Baadhi ya wajumbe wamelaani kitendo hicho na kusema kuwa kinalengo la kurudisha nyuma jitihada za kupatikana kwa katiba mpya huku wengine wakidai kuwa wapo wenzao miongoni mwao ambao wanaagenda tofauti.

Awali dalili za kuharibika kwa mkutano huo zilionekana mapema kufuatia kikao kilichofanywa na wajumbe wa umoja wa katiba ya wananchi ukawa ambao kupitia viongozi wao Mh James Mbatia na Freeman Mbowe walisema zipo njama zimepangwa za kubadili kanuni na hivyo hawatakubali.