Raia wa Uganda kutoka dini mbali mbali hii leo wamekusanyika katika uwanja wa Kololo mjini Kampala kwa maombi maalum na kutoa shukurani kwa Rais Yoweri Museveni kwa kutia saini mswaada wa sheria unaozuia mapenzi ya jinsia moja.
Viongozi wa dini mbalimbali wakristo na waislamu wamehimiza waumini wao kujitokeza kwa wingi katika ibaada hiyo maalum.
Hii ni mara ya kwanza viongozi wa dini mbali mbali nchini Uganda kujitokeza kwa pamoja na kuandaa Ibaada maalum ya kumshukuru Rais Museveni na kuliombea taifa kuepuka vitendo vya ushoga.
Rais Museveni aliidhinisha sheria hiyo ambayo raia wengi wa Uganda wameipigia debe sana.
Ibaada hiyo maalum inafanyika uwanja wa uhuru wa Kololo mjini Kampala, baada ya karibu mwezi mmoja na nusu tangu rais Yoweri Museveni kuiidhinisha.
Tangu Rais Museveni kuidhinisha sheria hiyo kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa mataifa ya Magharibi yakimtaka kubadili msimo wake, huku baadhi ya mataifa yakipunguza msaada kwa Uganda.
Lakini raia wengi wa Uganda walimsifu Rais Museveni kwa hatua yake.