MELI YA KOREA KASKAZINI YAKAMATWA LIBYA

Wakuu nchini Libya, wamesema kuwa wameikamata meli moja iliyokuwa na bendera ya Korea Kaskazini, ikiwa na shehena haramu ya mafuta katika bandari inayodhibitiwa na waasi.

Msemaji wa shirika la kitaifa la mafuta, amesema kuwa meli hiyo ilisimamishwa ilipokuwa ikijaribu kungoa nanga na kwa sasa inasindikizwa katika bandari inayodhibitiwa na serikali ya Libya.

Maafisa wa serikali ya Libya waliisimamisha Meli hiyo ya Korea Kaskazini ilipokuwa ikiondoka kutoka bandari inayodhibitiwa na waasi siku ya Jumatatu ikiwa imesheheni mzigo usio rasmi wa mafuta ghafi.

Jeshi la nchi hiyo limethibitisha tukio hilo.

Waasi wa zamani wanaotaka kuitenga eneo la Libya Mashariki, wamekuwa wakimiliki bandari ya Al-Sidra na vituo vingine muhimu vya kuuzia bidhaa nje katika eneo hilo tangu Julai mwaka uliopita.

Mnamo siku ya Jumamosi, walianza kupakia shehena ya mafuta yasiyosafishwa ndani ya meli hiyo ya Korea Kaskazini iitwayo Morning Glory, iliyokuwa imetia nanga katika bandari ya Al-Sidra.