TANZANIA KWANZA

RAIS Jakaya Kikwete amewasihi wajumbe wa Bunge maalum kaulimbiu yao iwe Tanzania kwanzana si vyama vyao vya siasa au makundi wanavyoviwakilisha kwenye Bunge hilo.
Aliwaambia wajumbe hao jana kuwa misimamoya vyama ambavyo wajumbe wamepewa na vyama vyao sio jambo baya kama ni suala la kujenga lakini kama ni suala la kubomoa misimamo hivyo haifai.

Rais amwataka wajumbe wazingatie maslahi mapana kwa taifa lao, kwani wananchi wanawategemea wajumbe hao kuipa Tanzania katiba nzuri na si katiba ambayo itakataliwa na wananchi.

"Kaulimbiu yenu iwe Tanzania kwanza naomba msijali makundi yenu kwanza," alisema Rais Kikwete na kusisitiza kuwa maslahi ya taifa shabaha yake ni kujenga nasi kubomoa.

Aliwataka waunganishe mawazo yote pamoja na si kutumia nguvu ili mawazo ya kundi fulani kupita kwani Katiba ni maridhiano na si kuonyeshana umwamba.

Aliwasihi wafanye kazi pamoja licha ya kuwa na itikadi za vyama tofauti, lakini suala la Katiba ni lazima waweke mawazo yao pamoja hata kama wanachukiana kutokana na itikadi zao.

"Mwisho wa siku hapa ni lazima mpige kura, hivyo toeni hoja zinazojenga ili muweze kushawishiana ili katiba tunayoenda kuandika ipatikane," alisema Kikwete.

Alionya kuwa kama wajumbe hao wasiposikilizana kuna hatari Katiba isipatakane kwani kuna makundi ambayo yanataka serikali mbili ambayo yanahitaji kuwashawishi wa upande mwingine wakubaliane nao na wale ambao wanataka serikali tatu nao wana kazi ya kuwashawishi wa kundi lingine nalo wakubaliane nalo.

Alisema Katiba inayotengenezwa nilazima ije na majawabu ya kero mbalimbali zilizopo, lakini akawataka wajumbe hao kuwa mahodari wa kukubali hoja nzuri za upande mwingine wanaopingana nao.

Alionya kuwa kama kuna kundi linataka kulazimisha upande mwingine ni hatari kubwa hivyo njia pekee ni kushirikiana na asiwepo mshindi bali mwisho wa siku wajumbe wote hao wawe washindi.

Alisema wajumbe hao wasipo jenga daraja, hawata afikiana hivyo akasisitiza suala la maridhiano litawale na akapongeza hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa za kuridhiana katika mambo ambayo yanaleta taofuti za kiitikadi.

Aliwaambia wajumbe hao kuwa walichukua muda mrefu katika kujadili kanuni hivyo akawataka waongeze kasi ya kuhakikisha kuwa mambo ambayo watayajadili wanafidia muda ili waende na wakati.

Rais Kikwete amesema wajumbe hao watafanikiwa tu iwapo watakuwa na mijadala ambayo haina ugomvi na vitendo vingine viovu kama ilivyotokea hapo awali.

"Sitarajii kama hili litatokea tena maana kufanya hivyo ni kuwaangusha wananchi ambao tayari walishakata tama kwa mambo ambayo yalikuwa yanafanyika," alisema Rais Kikwete.