POPO WAENEZA EBOLA GUINEA

Popo hutumiwa kutengeza kitoweo maarufu sana katika baadhi ya maeneo ya Guinea, lakini sasa inahofiwa kuwa popo wanachangia kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola kusini mwa nchi hiyo.

NI marufuku kula na kuuza popo Guinea

Maafisa nchini humo sasa wamepiga marufuku uuzaji na ulaji wa nyama ya popo katika juhudi za kudhibiti ugonjwa hatari wa Ebola, ambao kufikia sasa umesababisha vifo vya watu 62.

Nchi za kanda hiyo zikiwemo Liberia na Sierra Leone, zimechukua hatua kabambe kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo zikiwemo kuwafanyia uchunguzi wa kiafya watu wanaongia mipakani.

Maafisa wa afya wanapata msaada kutoka shirika la afya duniani na ujumbe wa kuhamasisha watu unapeperushwa kupitia televisheni.

Watu watano kati ya sita walioingia nchini Liberia kutoka Guinea walikua na ishara za ugonjwa huo na wamethibitishwa kufa.

Hata hivyo maafisa wa utawala nchini Liberia bado hawajathibitisha kikamilifu kama kweli walikufa kutokana na ugonjwa wa Ebola.