Walioapishwa ni Yahaya Hamisi Hamad ambaye anakuwa Katibu na Dk Thomas Kashilila anashika nafasiya Naibu Katibu wa Bunge hilo.
Shughuli za kuapishwa kwa makatibu hao, zilifanyika katika Viwanja vya Ikulu ndogo iliyoko eneo la Uzunguni mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
Viongozi hao ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Mwenyekiti Mteule wa Bunge , Samuel Sitta na Makamu wake Samia Suluhu Hassan.
Baada ya kiapo hicho, Rais Kikwete alikutana na Pinda, Sitta na Suluhu.
Hata hivyo mazungumzo yao yalikuwa ya faragha.
Akizungumzia nafasi yake Katibu waBunge, Yahaya Hamad, alikiri kuwa kazi iliyoko mbele yake ni kubwa lakini ana matumaini makubwa kwamba ataifanya kwa uadilifu mkubwa wa hali ya juu.
Hamad alisema changamoto kubwa anayoiona ni mwingiliano wa masilahi ya wanasiasa kwa sababu wengi wametanguliza misimamo ya vyama.
"Mimi ningewashauri wanasiasa kuacha kila kitu ili tuweze kufanya kazi ya watu iliyotuleta Dodoma, ili tuweze kupata Katiba nzuri itakayodumu kwa muda mrefu. Wanasiasa lazima wakubali kuwa nchi kwanza na vyama baadaye," alisema Hamad.
Kwa upande wake Dk. Kashillilah alisema atatumia uzoefu wake kumshauri na kumsaidia katibu na wenyeviti wa Bunge ili ndoto ya kuwa na Katiba nzuri itimie.Hata hivyo, alikanusha madai kwamba Katiba Mpya haitapatikana kutokana na kelele za wanasiasa.