WANAFUNZI WAMKATA MWALIMU NA PANGA

Wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari ya Kibara, wilayani Bunda wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Bunda wakikabiliwa na shtaka la kumshambulia na kumjeruhi kwa panga mwalimu mkuu wa shule hiyo.

Ilielezwa kuwa wanafunzi hao walimjeruhi mwalimu huyo baada ya kutaka kurejeshewa fedha zao zaada kwa vile hawakuwa na mpango tena wa kuendelea na masomo shuleni hapo.

Hata hivyo imeelezwa kuwa uongozi wa shule hiyo ulipinga azma hiyo ya wanafunzi kuacha shule na kurejeshewa fedha zao.

Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed aliwataja washtakiwa hao wanaosoma kidato cha tatu kuwa ni Amosi Shirima (22) na James Athuman (22).

Washtakiwa kwa pamoja wanadai wakutenda kosa hilo Machi 17 mwaka huu.

Mohamed alidai kuwa siku ya tukio,saa 5:00 asubuhi, washtakiwa hao kwa pamoja walimvamia mkuu wa shule, aliyetajwa kwa jina la Awadh Said wakati akiwa ofisini kwake shuleni hapo.

Baada ya kuvamia ofisini kwake, watuhumiwa walimshambulia sehemu mbalimbali za mwili kwa panga na kusababisha majeraha makubwa.

Masoud alisema baada ya mwalimu kuona anashambuliwa, alipiga kelele za kuomba msaada kabla ya watu kujitokeza na kuwakamata watuhumiwa na baadaye kuwapeleka kituo cha polisi.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa hali ya mwalimu huyo siyo nzuri naanaendelea kupata matibabu hospitalini alikolazwa.

Washtakiwa kwa pamoja wamekana shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Safina Semfukwe.

Hakimu Semfukwe aliamuru washtakiwa kurudishwa rumande mpaka kesi yao itakapo tajwa Aprili Mosi, 2014.