SAMUEL ETO'O ANA UMRI WA MIAKA 39

KOCHA, Claude Le Roy, amesema alizungumza na Samuel Eto'o kwenye simu na kwamba alikasirikasana kwa kitendo cha umri wake kuhojiwa.

Kocha wa sasa anayemnoa straika huyo wa Cameroon kwenye klabu ya Chelsea, Jose Mourinho, kwenye mazungumzo yake ya kawaida tu natajiri mtengeneza saa wa Uswisi ambayo yalinaswa kwa siri na kurekodiwa, alisema hafahamu umri halisi wa Eto'o kama ni miaka 32 kama ilivyo kwenye pasipoti yake ya kusafiria au ni miaka 35.

Kabla ya kufikia kwenye kuhoji umri wa Eto'o, Mreno Mourinho alikuwa akijadili uwezo wa mastraika wake kwenye klabu ya Chelsea na mustakabali wa kunyakua ubingwa msimu huu.

Mourinho alilalamika kwamba washambuliaji wake wote wanamwangusha kutokana na kushindwa kufunga mabao. Washambuliaji waliopo kweye kikosi cha Chelsea wote ni makini; Demba Ba, Fernando Torres na Eto'o, lakini wote hao wamekuwa butu na kushindwa kufunga mabao.

"Tatizo la Chelsea hakuna wafungaji," alisema Mourinho. "Ninaye Eto'o, lakini umri wake ni miaka 32, pengine inaweza kuwa 35, huwezi kujua," alisema Mourinho.

Kocha, Le Roy, aliyewahi kumnoa Eto'o kwenye kikosi cha Cameroon, anasema straika huyo hakupendezwa na kauli ya Mourinho kumsema kwamba umri wake ni mkubwa kuliko unaotambulika rasmi.Eto'o amesisitiza kwamba umri wake ni miaka 32. Jumatano iliyopita, Chelsea ilikuwa na mechi muhimu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray na kwamba iliaminika kwamba baada ya mchezo huo, Mourinho na Eto'o watahitaji kuwekana sawa.

Lakini, wakati Eto'o akisisitiza kwamba umri wake ni miaka 32, kama ulivyoandikwa kwenye pasipoti yake, mke wa zamani wa staa huyo ameibuka na kuchafua zaidi hali ya hewa baada ya kueleza kwamba umri wa supastaa huyo wa zamani wa Barcelona ni mkubwa kuliko hata uliotajwa na Mourinho.


*MKEWE AFICHUA

Mrembo, Anna Barranca, ambaye alizaa na Eto'o mtoto mmoja, amefichua wazi na kusema umri wastaa huyo ni miaka 39.

Mourinho alihisi Eto'o anaweza kuwa na umri wa miaka 35, lakini mwanamke huyo wa Kitaliano ametoa kali baada ya kudai kwamba Eto'o amepunguza miaka saba ya umri wake wa kweli.

Anna anasema: "Nadhani Samuel umri wake si miaka 35 ni zaidi ya 39. Samuel alizaliwa 1974 na sasa ana umri wa miaka 39."

Anna umri wake wa sasa ni miaka 43, mtoto aliyezaa na Eto'o anaitwa Annie.

Baada ya mjadala wa umri wa Eto'o kushika kasi, gazeti la The Sun lilimtafuta aliyekuwa mke wa staa huyo na kufanya mahojiano naye ilikufahamu ukweli halisi, ndipo mwanamke huyo alipasua kwamba Mcamerooni huyo ana umri wa miaka 39.

Anna na Eto'o walimzaa Annie wakati mchezaji huyo alipokuwa akiichezea Mallorca. Kuna wakati fulani, mwanamke huyo aliwahi kumlalamikia mchezaji huyo kutokana na kushindwa kutoa huduma kwa ajili ya malezi ya mtoto.


*TABIA YA ANNA

Mwanamke huyo anayefanya kazi saluni, anadaiwa kuwahi kuuza habari zake kwenye gazeti akimtuhumu Eto'o kwamba hana anachokifanya kwa mtoto wake na kwamba haishi kwa kutegemea pesa za mwanasoka huyo.

Mrembo huyo alisema Eto'o amekuwa akishindwa kutimiza wajibu wake wa kumlea mtoto wao,kabla ya sasa kuibuka na kusisitiza kwamba umri wa mchezaji huyo si miaka 32 na kwamba umri wake ni zaidi ya miaka 39.


*ETO'O ANG'AKA

Kwenye hali ya kuonekana kuwa na hasira, Eto'o alijifanya kupuuza kauli ya Mourinho kudai kwamba staa huyo ana umri mkubwa baada ya kusisitiza kwamba ataendelea kufunga mabao hata kama atafikisha umri wa miaka 50.Staa huyo kwa kejeli alisema aliweza kuifunga 'hat-trick' Manchester United licha ya kuwa na umri huo mkubwa, hivyo suala la kufunga mabao kwake ni jambo la kawaida.

"Mimi ni Samuel Eto'o, nitasemaje sasa?" Alisema alipozungumza na Sky Sports News baada ya mechi dhidi ya Galatasaray.

"Kama kwenye umri wa miaka 36 na 37 naweza kuifunga mabao matatu Manchester United kwenye mechi moja, hiyo ina maana kwamba naweza kuendelea kutikisanyavu hadi nitakapokuwa na umri wa miaka 50. Mimi sijali kitu, kitu muhimu kwangu ni kujitolea kwa nguvu zote katika kuisaidia timu yangu ili kutwaa mataji."

Kwenye mchezo dhidi ya Galatasaray, Eto'o aliingizwa katika dakika 68, kuchukua nafasi ya Torres ambaye alifunga bao kwenye sare ya bao 1-1 katika mchezo huo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliofanyika Istanbul, Uturuki, Jumatano iliyopita.


Chanzo:Mwanaspoti