JELA MIAKA 10 KWA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imemhukumu mfanyabiashara wa mbuzi, Adam Shaban Hole (46) kwenda jela miaka 10 baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi, kushiriki kumtoa mimba na kusababisha kifo chake.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo, Godlisten Raymond (37) ambaye kwa wakati huo alikuwa tabibu, alipewa adhabu kama hiyo ya miaka 10 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumtoa mimba na kusababisha kifo cha mwanafunzi.

Mwanasheria wa Serikali, Neema Mwanda alidai katika mahakama hiyo, mbele ya Jaji Mfawidhi, Cresentia Makuru kuwa tukio hilo ni la Septemba 7, 2006 katika Zahanati ya Tumaini mjini Singida.

Alidai kuwa Hole, ambaye ni mkaziwa kijiji cha Kintandaa Wilaya ya Ikungi mkoani hapa, alimpa mimba mwanafunzi, Hamida Athuman (16) kisha kushiriki kumtoa hatua iliyosababisha kifo chake.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa darasala saba kwa wakati huo, alifariki siku chache kabla ya kufanya mtihani wake wa kumaliza elimu ya msingi.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mfanyabiashara huyo, ambaye ana mashine ya kusaga nafaka kijijini hapo, katika kipindi hicho hicho, alimpa mimba mwanafunzi mwingine, Rukia Juma aliyekuwa anasoma darasa moja na Hamida.

Ilidaiwa kuwa baada ya kutolewa mimba, Rukia alilazwa Hospitali ya Mkoa wa Singida, ambapo alipatiwa matibabu sahihi na hivyo kuepuka kifo.

Mwendesha Mashitaka, Neema Mwanda aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwao na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Wakili Deus Nyabiri kutoka Dodoma aliyekuwa akimtetea mshitakiwa wa kwanza, Godlisten Raymond aliiomba mahakama impe mteja wake adhabu nafuu, kwa kuwa hilo lilikuwa ni kosa lake la kwanza.

Wakili Raymond Kimu ambaye alikuwa anamtetea Hole, aliiomba mahakama hiyo impe mteja wake adhabu ndogo au imwachie huru, kwa kuwa baada ya kuwapa mimba wanafunzi hao wawili, alikimbiwa na mke na kutengwa na familia yake.

Hata hivyo, Jaji Mfawidhi Makuru alisema katika hukumu yake kuwa kwa mazingira ya kawaida, kosa walililotenda washitakiwa, hawastahili huruma ya mahakama yoyote nchini.