MWANAMKE AHUKUMIWA KWA KOSA LA KUMSHAMBULIA POLISI

MWANAMKE mmoja amehukumiwa na mahakama ya wilaya ya Musoma, mkoani Mara, kutumikia kifungo cha miaka mitano na miezi sita jela, baada ya kupatikana na makosa ya kutoa matusi na kushambulia askari polisi wawili waliokuwa wanataka kumkamata.

Aliyekumbwa na adhabu hiyo ni Mary Jumanne, mkazi wa mjini Musoma, ambapo pia ameamriwa kuwalipa fidia ya shilingi laki moja kila mmoja askari polisi hao.

Hukumu hiyo imetolewa juzi na hakimu mwandamizi Richard Maganga, wa mahakama ya wilaya ya Musoma, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.

Awali, imedaiwa mahakamani hapona mwendesha mashitaka wa serikali, Jonas Kaijage, kuwa mshitakwa huyo alitenda kosa hilo machi 3, mwaka huu, mjini Musoma.

Kaijage alisema kuwa mshitaikiwa huyo aliwashambulia na kutoa lugha ya matusi askari polisi wawili, PC. Hamis na WP.Kuruthumu kutoka ofisi ya afisa upelelezi wa mkoa wa Mara, waliokuwa wamekwenda kumkamata akikabiliwa na kosa jingine la kutoa lugha ya matusi.

Alisema kuwa baada ya polisi hao kutaka kumkamata ndipo mwanamke huyo alipowatukana nakisha akamshambulia askari wa kike WP.

Kuruthumu na kumsababishia maumivu makali mwilini mwake. Mshitakiwa huyo baada ya kusomewa mashitaka yake alikiri kutenda makosa hayo huku akiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu, ombi lililotupiliwa mbali na mahakama hiyo.

Kufuatia ushahidi huo hakimu Maganga alihukumu kifungo cha miaka mitano kwa kosa la kushambulia askari na kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kutoa lugha ya matusi.


Source:Habari leo