WALIMU WAONGOZA KWA KUIBIWA MISHAHARA

IMEELEZWA kwamba fedha za walimu wengi huibwa kwa njia ya mtandao licha ya umuhimu wa kada hiyo katika jamii ambayo huzalisha wataalamu mbalimbali.

Hayo yalibainishwa jana na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi, Abrahamu Augustino, wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 77 yenye thamani ya sh milioni tano kwa Shule ya Msingi Muungano wilayani Bukombe, Geita.

"Ni kweli kwamba walimu wengi wanaongoza kwa kuibiwa fedha zao hasa mishahara ambayo hupita benki," alisema meneja huyo.

Augustino alisema benki yake inapokea malalamiko mengi yawalimu kupoteza fedha zao kwenye mtandao wa mashine za fedha (ATM) na kwamba baada ya kuhakiki kwa mfumo wa kamera za benki hukuta sura za wao kwa wao kuibiana ama watu wanaowakopa na kuweka kadi zao za benki kuwa dhamana.