UHURU KENYATTA AHIMIZA USHIRIKIANO AFRIKA MASHARIKI

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amewataka wabunge wa bunge lajumuia ya Afrika Mashariki kuhimiza utekelezaji wa sheria zilizopitishwa na wabunge hao ili ziweze kuridhiwa na kutekelezwa na nchi washirika.

Miongoni mwa sheria zilizopitishwa na bunge hilo ni ushuru wa forodha, soko la pamoja na sarafu ya pamoja, mkataba ambao bado haujaanza kutekelezwa.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa wakuu wa nchi za jumuiya hiyo yuko mjini Arusha makao makuu ya jumuiya hiyo kuzungumza na wafanyakazi na pia kuwafungulia kikao cha bunge kitakachodumu kwa wiki mbili zijazo.

Rais Kenyatta amezidi kusisitiza kuwa ushirikiano wa nchi hizo ndio ukombozi wao kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Rais Kenyatta kadhalika ameelezea nia ya mataifa yote ya jumuiya ya Afrika Mashariki kupambana vikali na tatizo la ujangili na kuutokomeza.

Rais Uhuru Kenyatta pia amesema jukumu la kukabiliana na vitendo vya ujangili ni la wananchi wote kwa sababu lina athari kwa kila mtu mkaazi wa Afrika Mashariki.

Ama kuhusu suala la uhuru wa uhamishaji wa mitaji na uhuru wawananchi wa Afrika Mashariki kutembea kutoka nchi moja kwenda nyingine, amesema jambo hilo linaweza kumalizwa pindi kila nchi itapokamilisha taratibu za matumizi ya vitambulisho kwa raia wake:

Rais Uhuru Kenyatta na ujumbe wake wamerejea nyumbani kwa njia ya barabara kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga.