Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amekerwa na tabia ya baadhi ya watu wanaosambaza uzushi katika mitandao ya kijamii kwa kutumia jina lake.
Lowassa alisema kuna watu wanaoendeleza kusambasa picha yanoti ya Sh500 yenye picha yake huku wakiongeza maneno mabaya juu yake.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Lowassa alisema, "Kitendo hicho siyo utani, bali ni dhihaka na dharau kwa alama za Taifa na mamlaka ya nchi."
"Hizi ni alama za Taifa ambazo zinatakiwa kulindwa na kuheshimiwa na watu wote, si busara kwa hao wanaozichezea kuendelea kufanya hivyo, kwani ni dharau kubwa kwa Taifa' alisema.
Katika noti hiyo ya Sh500 inaonekana upande wa kulia wa noti hiyo picha ya Edward Lowassa, huku ikikaribiana na ngao ya Taifa huku ikionyesha kuwa ilitolewa na Benki Kuu ya Tanzania..
Alisema anaheshimu maoni ya watu na nguvu ya mitandao ya kijamii, lakini anasisitiza umuhimu kwa wananchi hao kutumia nguvu hiyo ya mitandao kwa kujadili maendeleo ya nchi badala ya kuzusha mambo yasiyo na tija. Kwa nyakati tofauti, picha hiyo imekuwa ikisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwamo ya Facebook, Instagram, Whatsapp, na Twitter huku kukiwa na maneno kama "timu Lowassa" na mengineyo.
Ikumbukwe kuwa Lowassa yupo katika adhabu ya kutoshiriki katika masuala yoyote yahusianayo na kampeni za chinichini za urais, baada ya kamati ya maadili ya CCM)kutoa hukumu yake mwezi uliopita.
Adhabu hiyo pia iliwakumba wengine watano wakiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Moja ya sababu ya adhabu hiyo ya miezi 12 ilikuwa ni kuanzisha kampeni za chinichini za kugombea urais mwaka ujao nje ya muda uliopangwa, ambapo baadhi ya wanachama akiwamo Lowassa walituhumiwa kuhusika kuandaa makundi na fulana za kujinadi.