WANAFUNZI DARASA LA SABA WAOANA

MWANAFUNZI aliyehitimu Darasa la Saba mwaka jana, jina tunalo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, kwa madai ya kumuoa msichana waliyekuwa wakisoma naye darasa moja mwenye umri wa miaka 15.

Binti huyo alifanikiwa kupata nafasiya kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Chala wilayani Nkasi, lakini ameshindwa kujiunga kwa kuwa ni mke wa mtu. Wawili hao walikuwa wakisoma Shule ya Msingi Kacheche kijijini Kacheche wilayani Nkasi.

Mshitakiwa ambaye kwa sasa ni mkulima katika kijiji cha Kacheche alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Ibrahim Mgalamalira ambapo alikana shtaka hilo. Mtuhumiwa alidai kuwa anafahamu kuwa amemaliza elimu ya msingi, lakini hakuwa na taarifa kama alikuwa amechaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari mapema mwaka huu.

Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alimuoa msichana huyo, Februari 24, mwaka huu na kuishi naye nyumba moja kijijini Kacheche kama mume na mke kwa siku sita hadi alipotiwa nguvuni Machi 3, mwaka huu.

"Msichana huyu bado ni mwanafunzi kwa kuwa alichaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Chala wilayani hapa lakini ameshindwa kuendeleana masomo kwa kuwa alikuwa ameolewa na mtuhumiwa ambaye sasa amemkatisha masomo yake," alidai mahakamani hapo Mwendesha Mashtaka.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alipohojiwa kwa mara ya kwanza kabla ya kufikishwa mahakamani hapo, alikiri kumuoa msichana huyo kwa kuwa alifahamu kuwa ameshamaliza darasa la saba mwaka jana.

Hakimu Mgalamalira aliamuru mshtakiwa arudishwe rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo alimtaka awe na wadhamini wawili wenye mali zisizoweza kuhamishika zenye thamani isiyopungua Sh milioni moja. Shauri hilo limeahirishwa hadi Machi 26, mwaka huu litakapotajwa tena.


Chanzo:Habari leo