Tottenham Hotspur hapajatulia, licha ya ukweli kwamba kocha wao mpya, Mwingereza Tim Sherwood anaonekana kujaribu kufurukuta.
Ushindi aliopata katika mechi ya wikiendi dhidi ya Southampton umempa moyo kwamba huenda Mwenyekiti Daniel Levy atamwacha, lakini kuna kila tetesi kaskazini mwa London kwamba mahasimu hao wa Arsenal wanatafuta kocha mwingine.
Spurs hawaendi vizuri licha ya kusajili wachezaji wengi na ghali wa kimataifa, ambapo ni majuzi tu wametolewa kwenye Kombe la Ligi ya Europa baada ya kupokea kichapo cha 1-0 kutoka kwa Arsenal.
Sherwood wakati mwingine ameonesha hasira na hamaki kwenye eneo la makocha kiasi kwamba katika mechi ya marudiano ya Europa dhidi ya Benfica nchini Ureno aliamua kukaa kwenye jukwaa la watazamaji ili asikorofishane na kocha wa klabu pinzani kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza jijini London.
Wakubwa wa Spurs wamekuwa kimya kwa muda, Waswahili wanasema kimya kikuu kina mshindo mkuu, lakini Sherwood anayepambwa na baadhi ya wachambuzi wa Kiingereza amekuwa akisema uamuzi wa mwisho kumwondoa au kumwacha upo mikononi mwa Levy, kama alivyofanya kwa mtangulizi wake, Andre Vilas-Boas.
Wameanza kutajwa makocha wanaoweza kuchukua nafasi hiyo, mmoja wapo akiwa mchezaji wa zamani wa Barcelona na Real Madrid ambaye pia alikuwa kocha wa Swansea, Michael Laudrup.
Mwingine anayetajwa ni Kocha wa Frank de Boer ambaye amewezesha timu yake kutwaa mataji matatu ya ligi yao – Eredivisie na sasa anaelekea kuwapatia kombe kwa mara ya nne mfululizo. Kaka yake De Boer, Ronald, anadai kwamba Spurs walimfuata Januari kumwomba aichukue timu Januari mwaka huu ikashindikana.
Baada ya kufundisha Liverpool kwa mafanikio kisha kwenda kupumzika Mashariki ya Kati kabla ya kuwa kocha wa muda wa Chelsea na sasa Inter Milan, Kocha Rafa Benitez anaweza kurudi tena kwenye Premier League na kuichukua Spurs.
Anaifahamu vyema EPL na hivyo anaweza kuwa kocha mzuri wa kuwavusha Spurs msimu ujao na pia ana historia ya kushinda na kutwaa mataji, kuanzia ya nchi, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Europa. Amepata pia kuwafundisha Valencia wa Hispania.
Spurs wanatajwa pia kutaka kumchukua kocha wa sasa wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal ambaye nafasi yake itachukuliwa huko na Guus Hiddink baada ya fainali za Kombe la Dunia la Fifa mwaka huu nchini Brazil.
Alipoulizwa juu ya uwezekano wake kuwafundisha Spurs, Van Gaal alisema hivi: "Tazama wasifu wangu. Nimetwaa kombe kila msimu enzi zangu nikiwa kwenye klabu…utauliza, je, bado nafanya mawasiliano na Spurs? Wakati utafika ambapo nitaweza kuzungumzia suala hilo."
Van Gaal ametwaa mataji ya Uefa na Ujerumani, Uholanzi na Hispania kwa hiyo ni kana kwamba sifa zake zipo juu mno kufundisha timu kama Spurs ambao inawawia hata ngumu kukamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu ya England. Aweza kwenda Spurs kama hakuna nafasi wazi kwenye klabu nyingine kubwa.