ALBINO AUA NA KUCHUNA NGOZI MTOTO

POLISI mkoani Singida inawashikilia wanawake wawili, mmoja wao akiwa mlemavu wa ngozi `albino', kwa tuhuma ya kuua na kumchuna ngozi mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Geofrey Kamwela aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Hidaya Omari (20), ambaye ni albino na ni mama wa mtoto aliyeuawa na Neema Paulo (35) ambaye ni mamawa Hidaya.

Watuhumiwa wote ni wakulima na wakazi wa Kijiji cha Nkalankala, Kataya Mwanga, Tarafa ya Nduguti Wilaya ya Mkalama mkoani Singida.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, tukio hilo lilitokea saa 1.30 asubuhi Machi 13, mwaka huu kijijini hapo ambapo mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya kisima cha maji chenye kina cha mita moja ukiwa unaelea.

Alisema kuwa uchunguzi wa awali wa Polisi ulibaini kuwa kabla ya mtoto huyo kuuawa, alinyongwa shingo yake, kisha kuchunwa ngozi katika sehemu zake za siri na kutumbukizwa ndani ya kisima hicho.

Kamanda Kamwela alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo kinaweza kuwa ni imani za kishirikina na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.