WABUNGE WA BUNGE LA KATIBA WATOFAUTIANA

Wajumbe wa bunge la katiba wamekuwa na mtazamo tofauti wa kuwasilisha mapendekezo ya vifungu vya rasimu ya kanuni za bunge vilivyo na matatizo baada ya baadhi ya wabunge kuonyesha kutokubaliana na pendekezo la mwenyekiti wa muda lililotaka wawasilishe kwa maandishi kwa kamati ya kanuni.

Hatua hiyo ya wajumbe ilizua kutokusikilizana kwa baadhi ya wajumbe na mwenyekiti huku wajumbe wengine wakisimama na wengine kuwasha vipaza sauti bila ya utaratibu hali iliyomlazimu wa mwenyekiti wa semina ya wajumbe kuzungumza.

Katika semina hiyo baadhi ya wajumbe wameshauri rasimu hiyo ipitiwe kurasa kwa kurasa huku wengine wakipongeza utaratibu wa mwenyekiti wa muda unaotaka mapendekezo yawasilishwe kwa kamati ya kanuni kwa maandishi.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wamelalamikia wajumbe wa kamati ya kanuni kuzingatia zaidi hoja za makundi makubwa na kuziacha hoja za watu wachache katika kutengeneza rasimu ya kanuni za bunge maalum.