AUSTRALIA YATOA TAARIFA YA VITU KUONEKANA BAHARINI KAMA NDEGE YA MH370

Waziri mkuu wa Australia amesema kuwa mitambo ya satelite ya nchi hiyo imenasa picha za vitu vinavyoonekana kama vifusi ambavyo huenda ni vya ndege ya Malaysia iliyopotea siku 13 zilizopita.

Waziri mkuu huyo, Tony Abbott, ameambia bunge mjini Canberra kwamba picha za Satelite zimeonyesha vitu viwili vinavyofanana na vifusi vya ndege hiyo.

Taarifa hii imejitokeza karibu wiki mbili baada ya ndege hiyo kutoweka na abiria zaidi ya miambili kutoka mjini Kuala Lumpur Malaysia kuelekea Beijing.

Msemaji wa halmashauri ya usalama wa safari za ndege, John Young, baadaye alisema kuwa vifaa hivyo ambavyo kimoja kina ukubwa wa mita 24, vimeonekana umbali wa kilomita2500 kusini Magharibi mwa pwani ya Australia.

Aliongeza kwamba,vifusi itakuwa vigumu kuviona vifusi hivyo na pia huenda sio vya ndege hiyo.

Wakati taarifa hii ilipotolewa, kulikuwa na ndege ya Australia katika neo hilo , ndege zaidi zinatarajiwa kuwasili katika eneo lenyewe na pia manowari ya jeshi inaelekea huko.

*UDADISI WA PICHA ZA SATELITE

Australia inadadisi picha za Satelite za vitu viwili vinavyodhaniwa kuwa mabaki ya ndege iliyopotea ya Malaysia.

Nchi hio inashirikiana na Norway,New Zealand na Marekani kutafuta mabaki hayo.

Upepo mkali na mvua zilitatiza juhudi hizo hii leo na kusababisha shughuli hiyo kusitishwa. Hata hivyo msako huo utaendelea siku ya Ijumaa.

Bwana Tony Abbott, aliambia bunge kuwa hii ni taarifa mpya na iliyothibitishwa.

Lakini maafisa wakuu nchini Malaysia wametahadharisha kuwa mabaki hayo huenda sio ya ndege yake, ambayo ilipotea siku kumi na tatu zilizopita ikiwa imewabeba watu 239 kuelekea Beijing.

Mabaki hayo yalionekana umbali wa kilomita elfu mbili miatano Kusini Magharibi mwa mji wa Perth.