WASIWASI WA UDUKUZI FACEBOOK

Mwanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg amesema kuwa amezungumza na Rais Barack Obama kumwelezea kero lake kuhusu udukuzi unaofanywa na serikali kwa mitambo ya Dijital.

Zuckerberg mwenye umri wa miaka 29, amesema kuwa serikali ya Marekani inapaswa kupigia debe internet badala ya kuwa adui wa mitandao ya kijamii.

Matamshi yake yanakuja siku moja baada ya ripoti kuwa shirikala ujasusi la Marekani ilibuni mtandao bandia wa Facebook ili kuweza kuvamia mitambo ya Kompyuta inayotumiwa kwa uchunguzi.

Shirika la NSA lilisema kuwa taarifa hiyo sio ya kweli.

Mnamo mwezi Septemba, Zuckerberg alisema kuwa Marekani ilikosea sana taarifa zilipoibuka kuwa inafaya udukuzi kwenye mitandao.

Mwanateknolojia huyo alisema kuwa huenda ikachukua muda mrefu sana kwa mageuzi yoyote kufanyika.

Zuckerberg alisema, "wakati wahandisi wetu wanapofanya kila hali kuboresha usalama kwenye mtandao, kwetu ni kama tunawalinda kutokana nawahalifu kwenye mitandao, sio serikali yetu.''

"Serikali ya Marekani lazima ipigie debe Internet sio kuwa adui wa mtandao. Lazima waelezee wanachokifanya la sivyo, watu hawatakuwa na imani tena na serikali.''

Shughuli za shirika la ujasusi la Marekani lilijipata motoni baada ya ufichuzi kutolewa na aliyekuwa jasusi wakati mmoja Edward Snowden, mwaka jana.

Ufichuzi wake ulionyesha kuwa shirika hilo lilikuwa linakusanya taarifa za simu za watu, kufanya udukuzi na kuvamia mitandao ya watu.