MARTINEZ KUMRITHI WENGER

Kocha wa Everton, Roberto Martinez ameanza kufikiriwa na wakubwa wa Arsenal kuwa ndiye chaguo sahihi la kumrithi Arsene Wenger.

Martinez, Mhispania aliyeoa mke Mwingereza alijiunga na Everton akitoka Wigan Athletic walioshuka daraja msimu uliopita, lakini anawavutia sana wadau wa Emirateskwa tabia zake uwanjani na hata nje.

Hata jinsi alivyopokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Arsenal wikiendi iliyopita kwa namna ya kipekee akionesha heshima na utulivu badala ya hasira na fujo, kimemwongezea maksi miongoni mwa wakubwa wa Arsenal.

Hata hivyo, kukubalika huko kwa Martinez hakumaanishi kwamba Wenger anaondoka kesho au keshokutwa, hapana. Wenger anakaribia kuanguka saini kwa ajili ya kuendelea kuwanoa Arsenal kwa miaka mingine miwili.

Hata hivyo, wamiliki na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Arsenal wameamua kuanza kufikiria mrithi wa Wenger ili wasikutwe na mshangao wakikosa la kufanya ikitokea siku Wenger kweli anaondoka.

Kwa hiyo wamekuwa wakikuna vichwa juu ya nani angeweza kuwa chaguo lao, na jina la Martinez linashika namba moja kwa sasa, wakipendezwa na aina ya soka analowafundisha vijana wake, pasi kama zile ambazo washabiki wa Arsenal wanazipenda na wamezizoea chini ya Wenger.

Kadhalika Martinez ni muumini wa kuhamasisha kuendeleza ukuzaji vipaji kupitia timu za vijana, falsafa ambayo Arsenal wamekuwa nayo kwa muda mrefu na hata nyota waowengi waliowakimbia walikuwa mazao yao.