WANAFUNZI WA KIKE WAPATWA NA UGONJWA WAKUANGUKA

WAZAZI na walezi ambao watoto wao wanasoma katika Shule ya Msingi Inyonga wilayani Mlele, mkoani Katavi wameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutumatimu ya wataalamu wa afya kuchuguza ugonjwa wa ajabu unaowakumba wasichana wanaosoma katika shule hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wazazi hao wameelezea kupata hofu ya afya ya watoto wao wanaosoma katika shule hiyo, baada ya kukumbwa na ugonjwa huo wa ajabu ambao unasababisha waanguke wakiwa shuleni huku wakiweweseka na kupiga kelele.

"Tunaiomba Serikali iingilie kati ili kunusuru maisha ya watoto wetu hawa ambao sasa hawasomi tena, tunaomba watume wataalamu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuja huku kufanya uchunguzi wa kitabibu ili kubaini ugonjwa huu," anasema mmoja wa wazazi hao, Isabela John.

Isabela alisema wasichana hao wanaosoma darasa la tatu hadi la saba wakiwa na umri wa miaka katiya 12 na 16, wamekuwa wakishambuliwa na ugonjwa huo kwa zaidi ya miezi minne sasa.

"Ajabu ni kwamba watoto wetu hawa wanakumbwa na ugonjwa huu wa ajabu ambao hata wataalamu wa afya wilayani hapa wamekiri kuwa kila wanapowachunguza kitabibu watoto hawa hawaoni ugonjwa wowote. Isitoshe watoto hawa wakifika nyumbani, hawashambuliwi na ugonjwa huo isipokuwa pale wanapokuwa katika eneo hilo la shule," alisema mzazi mwingine, Patrick Ndolezi.

Wazazi wengine waliohojiwa na gazeti hili wamekiri kuwahamisha watoto wao wanaosoma katika shule hiyo wakihofia afya zao na wakiri kuhusisha ugonjwa huo na imani za kishirikiana kwamba shulehiyo imekumbwa na pepo wabaya.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, Mganga Mkuu wa Wilayaya Mlele, Dk Admihabesi Koni, alisema ugonjwa umewastaajabisha hata wataalamu wa afya wilayani humo kwani unawakumba wasichana tu wanaosoma katika shule hiyo wakati wanasoma pamoja na wenzao wa kiume."

Watoto hao wakikumbwa na ugonjwa huo hakika wanakuwa na nguvu ya ajabu, ni vigumu watu kuwathibiti kirahisi …Ugonjwa huu ulianza kwa wasichana wanaosoma darasa la tano, sita na saba lakini sasa umewakumba pia wanafunzi wa kike wanaosoma darasa la nne na la tatu.

"Lakini wanafunzi wa kike wanaosoma darasa la kwanza na la pili hawajakumbwa na ugonjwa huuna wamekuwa wakiendelea na masomo yao shuleni hapo kama kawaida," alisema.

Kwa mujibu wa Dk Koni, wanafunzi hao wanapokumbwa na ugonjwa huo wamekuwa wakifikishwa hospitalini kwa matibabu na kutibiwa kwa kudungwa sindano za 'valium' ambapo baadae wakizinduka hushikwa na butwaa na kuhoji walipo na kwa nini wamefikishwa hapo.

"Sisi wataalamu wa afya hatuamini kama ugonjwa huu unahusu imani za kishirikina, isipokuwa wanapofika hospitali kwa matibabu tunawakagua kitabibu na kuthibitisha kuwa hakuna dalili za ugonjwa wowote uliowakumba," alisema.

Aliongeza kuwa jitihada kadhaa zimeshafanyika ili kunusuru hali hiyo kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kuitwa kufanya ibada maalumu, lakini hali haijabadilika.

"Kulikuwa na uvumi uliozagaa kuwashule hiyo imekumbwa na mapepo wachafu na majini, hivyo waganga wa jadi walifika shuleni hapa na kufanya vitu vyao lakini wapi bila ya mafanikio yoyote yale," alisema Dk Koni.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mlele, Ephras Tenganamba alipozungumza na gazeti hili, amesema jitihada kadhaa zimefanyika bila mafanikio na hata baada ya kuwahamishia wanafunzi hao katika Shule ya Sekondari Inyonga jirani na shule hiyo, bado watoto hao waliendelea kuanguka huku wakipiga kelele.


Chanzo: Habari leo