Mshitakiwa alitiwa hatiani na mahakama hiyo kwa kumuua kwa kukusudia Ibrahim Juma (44) mkaziwa kijiji hicho cha Igalula. Inadaiwa alitumia shoka kumchinja kisha kuufukia ardhini mwili wa mdai wake.
Hukumu hiyo ilitolewa jana katika kikao cha Mahakama Kuu kilichofanyika katika mahakama ya wilaya ya Mpanda na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Jaji Kasukulo Sambo.
Awali Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Njoloyota Mwashubila alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 9 mwaka 2009 katika muda usiofahamika.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa siku hiyo ya tukio marehemu alimuaga mkewe aitwaye Hamisa Hassan kuwa anakwenda nyumbanikwa mshitakiwa Malambi Lukwaja ili kuchukua magunia yake ya mpunga ambayo alikuwa akimdai ambapo walikubaliana amlipe magunia hayo ya mpunga baada yakuvuna.
Mwanasheria huyo wa Serikali aliieleza mahakama hiyo kuwa tangu siku hiyo alipoondoka marehemu hakurudi nyumbani hivyo kusababisha mke wake apateshaka na kutoa taarifa kwa ndugu wa marehemu juu ya kutoonekana kwake kwa kipindi cha wiki tatu.
Alieleza ndugu wa marehemu walipopewa taarifa hizo waliamua kumfuatilia nyumbani kwa mshitakiwa ambapo aliwaeleza marehemu alifika kwake na alishaondoka nyumbani kwake baada ya majibu hayo ndugu hao waliamua kurudi nyumbani.
Mwashubila alidai kuwa wakati ndugu hao wa marehemu wakiwa wanarudi nyumbani waliitwa na jirani yake na mshitakiwa ambae aliwatahadharisha kutojenga mazoea ya kwenda kwa mshitakiwa kwani kuna mtu mmoja alikwenda hapo na hajaonekana tena.
Alieleza baada ya kuelezwa hivyo ndugu hao walikwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji na kisha walimkamata mshitakiwa na kumpeleka kituo cha Polisi cha Mpanda.
Mwanasheria huyo aliendelea kueleza baadhi ya wanakijiji walibaki nyumbani kwa mshitakiwa wakiendelea kumhoji mkewe ambae aliwaeleza marehemu siku hiyo aliondoka na mumewe kwenda shamba, lakini kesho yake mshitakiwa alirudi akiwa peke yake na alipojaribu kumuuliza mume alikuwa mkali.
Ilidaiwa mke huyo wa mshitakiwa aliamua kuwapeleka lilipo shamba lao la mpunga na walipofika walishituka kuona kuna eneo limefukuliwa ambapo waliamua kulifukua eneo hilo ghafla waliona miguu ya marehemu ndipo walipotoa taarifa polisi ambao walifika kwenye eneo hilo na kuendelea na ufukuaji mwili wote wa marehemu ukiwa umechinjwa na kiwiliwili chake kutenganishwa na kichwa ambapo kwenye kichaka waliiona baiskeli ya marehemu na nguo zake.
Chanzo: Habari leo