MLINZI WA OBAMA ALEWA CHAKARI

Maafisa watatu kutoka katika idara ya kumlinda Rais wa Marekani Barack Obama katika ziara yake nchini Uholanzi, wamerejeshwa nyumbani kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Jarida la Washington Post nchini Marekani limeripoti kwamba mmoja wa askari hao alipatikana akiwa mlevi chakari kiasi cha kupoteza fahamu katika hoteli mojamjini Amsterdam.

Mapema Jumapili, siku moja kabla ya Obama kuwasili nchini humo, wafanyakazi wa hoteli waliarifu ubalozi wa Marekani nchini Uholanzi kuhusu walivyompata askari huyo katika hali ya kutojitambua.

Msemaji wa idara ya upelelezi Marekani alikataa kutoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo, ingawa alisisitiza kuwa watatu hao wameachishwa kazi kwa muda uchunguzi ukiendelea.

Tukio hilo lilitokea kabla ya Rais Obama kuwasili Uholanzi kwa mkutano kuhusu kawi ya Nuklear.

Shirika hilo la ujasusi limekuwa likijaribu kujisafishia sifa yake hasa baada ya kukumbwa na kashfa mbali mbali.

Mnamo mwaka 2013, majasusi wawili waliondolewa katika kikosi cha ulinzi cha Rais Obama kufuatia tuhuma za kuhusika na kashfa ya ngono na utovu wa nidhamu.

Na mnamo mwaka 2012, majasusi kadhaa waliachishwa kazi kufuatia madai kuwa walikodi makahaba walipokuwa mjini Cartagena, Colombia.