Aidha, sambamba na onyo hilo, piaimevitaka vyombo hivyo kuwasilisha kwa mamlaka hiyo miongozo yao ya kuchuja vipindi wanavyorusha hewani baada ya kubaini baadhi yao hawakuwa na miongozo hiyo na kuwataka wazuiewatangazaji kuingia na miziki yao binafsi studio.
Onyo hilo lilitolewa jana, Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Magreth Munyagi, ikiwa ni sehemu ya hukumu kwa vyombo hivyo kwa kukiuka Kanuni za Utangazaji za mwaka 2005 na kuhatarisha mshikamano wa Taifa, usalama wa Taifa na maadili bora.
Akisoma hukumu hiyo mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya TCRA kabla ya kuwakabidhi wahusika, Munyagi alisema Kamati ya Maudhui ya TCRA inayosimamia maadili na maudhui ya utangazaji nchini ilibaini ukiukwaji wa kanuni hizo mwaka jana na mwaka huu na kabla ya uamuzi huo, ilikutana na wahusika kwa majadiliano na kufikia muafaka.
"Hivyo kwanza, kamati inatoa onyo kali kwa wahusika, pili, inawataka kuwasilisha mwongozo wa uchujaji wa vipindi vyao kwa mamlaka na tatu, ikiwa watarudia kosa hili, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Wahusika wana uhuru wa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu katika kipindi cha siku 30 baada ya tamkohili," alisema Munyagi akisoma hukumu hiyo.
Akifafanua kuhusu uvunjifu huo wakanuni, Munyagi alisema kituo cha televisheni cha ITV na Star Tv kwa nyakati tofauti vilirusha hewani tangazo la taasisi ya Policy Forum linalohamasisha wananchi kutolipa kodi katikati ya taarifa za habari za usiku (saa 2:00 hadi 3:00) kinyume cha kanuni namba 5(a) na 6(b) za kanuni hizo.
Kuhusu RFA, alisema Juni 27 mwaka jana katika kipindi cha "Sindano tano za moto" kilichorushwa kati ya saa mbili hadisaa tatu asubuhi na radio hiyo, mtangazaji alipiga wimbo wa msanii Nashi (MC) inayoamsha hisia za uchochezi wa kisiasa, maandamano na uvunjifu wa amani kutokana na maudhui ya wimbo wenyewe.
Kufuatia majadiliano na pande zotembili, Munyagi alisema wahusika walikiri kutoa maudhui hayo kupitia vyombo vyao ambapo katika majadiliano Mkurugenzi wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile alieleza kuwa, wao hawakuona uvunjifu wa amani katika tangazo hilo, bali elimu kwa umma kuhusu misamaha ya kodi na uwajibikaji wa serikali na jamii.
Aidha, Kampuni ya Sahara Media Group inayomiliki Star TV na RFA, kupitia Mkurugenzi wake Anthony Dialo na Meneja Mipango na Utafiti, Nathan Lwehabura, walikiripia kutumia muziki na tangazo hilona kuiomba TCRA isiwape adhabu kali kwa kuwa hawakuwa na mwongozo wa kuchuja muziki na maudhui kabla ya kuyarusha kwa jamii.
Akizungumza jana na waandishi mara baada ya hukumu hiyo, Lwehabura alisema hatua hiyo ni changamoto kwa vyombo vyote vya habari kwa kuwa wao binafsi hawakuona kosa kutokana na ukweli kwamba hata baadhi ya viongozi wa serikali huzungumza wazi wazi kuhusu misamaha ya kodi lakini wanaheshimu uamuzi wa TCRA na tayari wamesitisha matangazo hayo.
"Tumekiri kwamba tulitangaza maudhui yaliyosomwa, lakini hili linazungumzika na pia ni suala la mjadala kwa wanahabari wote, StarTV na ITV ni kama kondoo wa kafara tu, tunapaswa kujadili nini ni uchochezi maana hili la kodi hata Bungeni linazungumzwa, tumejifunza unapopata tangazo kutoka taasisi hizi binafsi, lazima utafsiri kama ni uchochezi ama la,"alisema Lwehabura.