MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA DAR ZAZUA MAAFA

Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es salaam, zimesababisha maafa kutokana na baadhi ya magari kupinduka barabarani mengine kukwama kwenye mashimo na msongamano wa muda mrefu kutokana na magari kuteleza na miundombinu ya barabara kuharibika.

Akizungumza katika eneo la tukio Kongowe Mzinga jijini Dar es Salaam kondakta wa lori lililopinduka katika barabara hiyo Casmir Michael amesema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya mwenye daladala kusimama ghafla mbele ya lori lao ndipo breki za gari lao kukataa na tairi kupoteza mwelekeo kisha gari kupinduka.

Baadhi ya mashuhuda wa ajali ya haisi wamesema chanzo ni baada ya haisi kuigonga gari nyeupe iliyokuwa imeharibika barabarani lenye namba za usjaili T591 CGP na kushindwa kushika breki saa chache kabla halijatumbukia mtaroni kwa kuwa mbele kulikuwa na shimo kubwa lililochimbika baada ya kunyesha kwa mvua.

Nao madereva waliokumbwa na adha ya mrundikano wa foleni barabani wameiomba serikali kutengeneza makarabati imara na barabara za pembeni ili magari yaweze kupita kwa urahisi zinapotokea ajali kwenye barabara hiyo.

Imeshuhudiwa gari la magereza nalo likiwa limenasa kwenye barabara ya pembeni hali iliyowalazimu askari magereza kushuka kwenye gari lao kisha kulisukuma walipokwama wakiwa njiani kuelekea wilayani Mkuranga mkoani Pwani kusindikiza mahabusu wao.