Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen aliyeongea na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula akiwa ameongozana na uongozi wa mkoa, alisema ajali hiyo ilitokea saa 5 asubuhi mita kama 100 kutoka eneo la ufukwe wa kienyeji baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupatwa na misukosuko.
Zelothe alisema ajali hiyo imesababisha vifo vitatu, majeruhi 21 wakiwemo watoto wadogo wawili kati ya mwaka mmoja na kuwataka wananchi kuwa makini na vyombo wanavyotumia kusafiria ikizingatiwa kwa sasa hali ya hewa siyo nzuri kutoka na na mvua zinazoendelea kunyesha.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Mwanahamis Juma (31) na Habiba Masoud (13) wote wakazi waMwalena Rahma Abdul (25) mkazi wa kitongoji cha Ngw'ale.
Naye Mkuu wa Mkoa, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia alieleza kuwa ajali hiyo imesikitisha sana nakwamba kifo hakina matarajio kwani waliokumbwa na mkasa huo walikuwa wakienda kwenye shughuli zao za kila kujitafutia kipato.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk Shaibu Maarifa alikiri kupokea majeruhi na maiti za ajali hiyo na kusema kuwa wanawahudumia ipasavyo ili waweze kurudi katika hali zao za kawaida.
Mmoja wa majeruhi walionusirika katika ajali hiyo, Sophia Kassim (28) alimwambia mwandishi wa habari hizi wakati wa mahojiano kuwa mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulijaza watu kupita kiasi na kwamba abria wote walikuwa wanawake isipokuwa dereva na msaidizi wake.