OFISI ZA CHADEMA MPANDA ZAFUNGWA

MGOGORO wa uongozi ndani ya Chadema, umeingia katika hatua nyingine baada ya makada wa chama hicho wanaopingana kimisimamo, kufunga ofisi za chama hicho mjini Mpanda kwa zaidi ya wiki sasa.

Makada hao wamegawanyika na kuwa na kambi mbili tofauti, ambapo kila upande umeweka kufuli lake na walinzi wake, kuhakikisha hakuna atakayevunja na kuingia ofisini humo.

Ofisi za chama hicho ambazo ziko katika Mtaa wa Mji wa Zamani mjini hapa, kabla ya kufungwa zilikuwa zikitumiwa na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa pamoja na viongozi Jimbo la Mpanda Mjini ambalo kwa sasa Mbunge wake ni Said Arfi (Chadema).

Mvutano huu wa uongozi uliibuka mwanzoni mwa wiki iliyopita, ambapo viongozi wa chama hicho waliosimamishwa hivi karibuni, walifika ofisini hapo ili waendelee na shughuli zao za kiofisi na kukutaofisi zimefungwa kwa kufuli linginetofauti na waliloliweka wao.

Baada ya kubaini hivyo, viongozi hao wa Jimbo la Mpanda Mjini, walilazimika kuwahoji wenzao wa wilaya kulikoni ofisi za chama hicho kufungwa kwa kufuli lingine, tofauti na hilo, ndipo walipojibiwa kuwa wao si viongozi tena, kwa kuwa tayari wamesimamishwa uongozi.

Pia, uongozi wa wilaya wa chama hicho, wanadaiwa kuwajibu wenzao hao kuwa kwa kuwa wamesimamishwa uongozi, hawana mamlaka tena ya kufanya shughuli zozote za chama ndani ya ofisi hizo.

Hivi karibuni kikao cha maridhianoya chama hicho kilichofanyika kwenye ofisi cha chama hicho zilizopo katika mtaa wa Mji wa Zamani mjini hapa, kiliwasimamisha uongozi baadhi yaviongozi waandamizi wa chama hicho mkoani hapa na wengine wawili kusimamishwa uanachama.

Kikao hicho kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda Magharibi, Masanja Katabi, kiliwasimamisha uongozi Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Katavi, John Malack, Katibu Mwenezi wa chama hicho mkoani hapa, John Matongo na Mwenyekitiwa Jimbo la Mpanda Mjini, Seif Sipia.

Wengine ni Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini Joseph Mona, ambaye pia ndiye Katibu wa Mbunge, Arfi na Katibu Mwenezi wa Jimbo la Mpanda Mjini, Godfrey Kapufi.

Mbali ya kusimamishwa uongozi, kikao hicho kimependekeza Kapufi na Diwani wa Kata ya Makanyagio, Idd Nziguye wavuliwe uanachama, kama ilivyokuwa kwa akina Dk Mkumbo na Mwigamba.

Pia, kikao hicho pia kiliazimia Arfi achunguzwe, wakimtuhumu kudhamini mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Maridadi mjini hapa, unaodaiwa kutumika kuwakashifu Lema na Mnyika.