MCHUNGAJI ASHIKILIWA KWA MAUWAJI

MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Anglikana, Usharika wa Mfarasi kata ya Madilu wilayani Ludewa, mkoani Njombe, Petro Chambachamba (87) anashikiliwa Polisi akihusishwa kwenye kesi ya mauaji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani, amesema jana kuwa Chambachamba pamoja na watu wengine wanane, wamekamatwa wakihusishwa na mauaji yaliyotokea Februari 25, mwaka huu saa 8 mchana katika kijiji cha Mfarasi.

Alisema watu hao wanatuhumiwa kuchukua sheria mkononi kwa kumpiga hadi kumsababishia kifo Boniface Mtweve (35), mkazi wa kijiji cha Ilininda kilichoko kata ya Madilu wakimtuhumu kuiba simu tatu mali ya Nuru Ngairo.

Kamanda alisema kwa kupitia taarifa za siri kutoka kwa wakazi wakijiji hicho, Februari 28, watu hao walikamatwa na kufikishwa mikononi mwa dola. Wengine waliokamatwa ni Linus Chaula, Stanley Katembo, Ery Mwapinga, Kedimoni Mwapinga, Phillimon Mgimba, Richard Mvalla, Meshack Mgaya na Nuru Ngairo.

"Ushahidi wa awali unawahusisha watu hao tisa akiwemo mchungaji huyo, hata hivyo wanaweza kuachiwa huru endapo baadaye wataonekana kutohusika na tuhuma hiyo na uchunguzi unaendelea," alisema Kamanda.

Hata hivyo, waumini wa usharika huo wamedai vyanzo vya taarifa za Polisi zinazomuhusisha mzee huyo katika kesi hiyo, ni vya uongo na wameomba aachiwe huru.

Zaidi ya wananchi 600 wa kijiji hicho, juzi walishiriki mkutano maalumu wakishutumu kuchukuliwa kwa mchungaji pamoja na watuhumiwa wengine.

Katika mkutano wa kijiji uliofanyika katika kijijini Mfarasi, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Petro Mwapinga alisema, " inasikitisha Polisi walivamia kijijini hapa usiku wa manane na kuwakamata ndugu zetu bila kushirikisha uongozi wa kijiji."

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Samwel Mtewele alisema wote wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji hayo, ni wale waliotoa taarifa katika kituo cha Polisi cha Lugarawa wilayani Ludewa, kwamba nyumba zao zilivunjwa na mali zao mbalimbali ziliibwa.

Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisala Anglikana Dayosisi ya Kusini Magharibi, Michael Lugome, alieleza kushangazwa na hatua ya Polisi kumkamata mchungaji huyo na wenzake.

"Taarifa tuliyopewa na Kijiji inaonesha kwamba kabla ya mauajihayo, Mchungaji wetu mstaafu na watuhumiwa wengine, walivunjiwa nyumba zao na mali zao kuibwa; taarifa hizo zilipelekwa Polisi, na askari walipaswa kuzifanyia kazi taarifa za wizi huo," alisema Lugome.

"Hili ni tukio la aina yake na yawezekana likawa la kwanza; lakini tuna maswali ya kujiuliza ni wapi na katika mazingira gani tukiohilo lilitokea na watu hawa akiwemo mzee huyo wa miaka 87 alishirikije katika tukio hilo," alisema Mwenyekiti wa Idara ya Uinjilisti ya Dayosisi hiyo, Nicholaus Mgaya.

Mke wa Mchungaji huyo, Lea Chambachamba, alisema mumewealikuwa nyumbani wakati watu wenye hasira kali kijijini hapo wakimpiga mtuhumiwa.

Alisema kabla ya tukio hilo, nyumba yake ilivunjwa na vitu kuibwa ambavyo inadaiwa mtuhumiwa huyo aliyeuawa, alikutwa navyo.

"Polisi hawajatenda haki, mume wangu ana miaka 87, mimi nina miaka 70; mzee wa umri huo anawezaje kwenda kwenye kundi lenye watu wengi na kushiriki kumshambulia mtu?" alisema.


Source: Habari Leo