NDUGU WAWILI WATUHUMIWA KUMUUA MPENZI WA MAMA YAO

NDUGU wawili wa kiume wa familia moja wilayani Mlele mkoa wa Katavi, wanatuhumiwa kumuua mpenzi wa mama yao kwa kumchinja, kisha kutelekeza mwili wake porini. Wakazi hao ambao mmoja ni mtoto mwenye umri wa miaka 16 ni wakazi wa Kitongoji cha Milumba Kata ya Kibaoni na aliyeuawa ni Kitungulu Luhende (65).

Inadaiwa mama yao, Sai Mponje (65) ambaye ni mjane anayeshikiliwa na polisi kwa sasa, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Luhende, jambo ambalo watoto hao hawakufurahishwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alitaja watuhumiwa hao ni Nyengu Kashele (19) na nduguye mwenye umri wa miaka 16.

Mtoto huyo anashikiliwa wakati Nyengu amejificha kusikojulikana. Mwili wa marehemu uligundulika Machi 3, mwaka huu saa 3:30 asubuhi katika milima ya kitongoji hicho cha Milumba ukiwa umeharibika.

Mwili huo uligundulika kutokana na msako uliofanywa na askari wa jadi(sungusungu) kwa kushirikiana na polisi na wananchi. Kidavashari alisema Februari 22, mwaka huu saa 2 asubuhi, Luhende ambaye pia ni mkazi wa kitongoji hicho cha Milumba, alimuaga mkewe kwamba anakwenda kijiji cha Kirida ambako ana mke mwingine.

Hata hivyo, Kamanda alidai kuwa badala ya kwenda kijijini Kirida, aliko mke wake mwingine, kwanza alipitia nyumbani kwa rafiki yake katika kitongoji hicho cha Milumba, aitwae Milembe Katembeni ambako aliacha pikipiki yake yenyenambari za usajili T449 BAF. Inadaiwa kisha alikwenda moja kwamoja kwa Sai (mama wa watuhumiwa).

Kamanda alisema tangu hapo hakuonekana hadharani hadi mwili ulipokutwa umetelekezwa eneo la milimani huku pembeni kukiwa na leseni yake ya udereva.

Akielezea sababu za kuanza kumtafuta, Kamanda alisema baada ya kutorejea kwa rafiki yake kuchukua pikipiki, Katembeni aliingiwa wasiwasi ndipo Machi 2 , mwaka huu aliamua kutoa taarifa kwa kiongozi wa sungusungu na kisha polisi, na msako ukaanza.