Aidha katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Suleiman Rashid, kwa Vyombo vya habari imeeeleza kuwa Ugonjwa huo ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam, mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014.
Hata hivyo hadi sasa idadi ya Wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huo, kuanzia kipindi hicho kuwa ni 70, ikiwa ni wagonjwa 58 Kinondoni, 7 Temeke na 5 Ilala, ambapo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita idadi ya wagonjwa hao iliongezeka mara mbili kuliko siku za nyuma na kusababisha kifo cha mtu mmoja katika hosipitali ya Mwananyamala.
Aidha, Dk. Rashid amesema ugonjwa huo sio mpya hapa nchini, kwani uligundulika Kwa mara ya kwanza Juni 2010 mkoani Dar es Salaam, ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa huo ilikuwa 40, pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huo.
*Wananchi wapewa angalizo
Wananchi wameshauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huo, bali wameshauriwa kwenda katika Vituo vya tiba mara wanapoona dalili za ugonjwa huo.
Amesema hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa Kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka hapa nchini, ambapo Wizara inaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.
Hata hivyo Wizara hiyo imesema jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo, ni Kuangamiza mazalio ya mbu, kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama, kuondoa vitu vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, na magurudumu ya magari
Hatua zilizochukuliwa na Wizara hiyo hadi sasa ni pamoja na uchunguzi unaondelea katika Mikoa na Wilaya nyingine, ambapo wameanza na wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa hiyo.
*Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni weusi na madoadoa meupe yenye kungaa.
Mbali na hayo Dalili za ugonjwa huo zimeelezwa kuwa ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususani sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu.
"Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya denge, mgonjwa mwenye dalili za homa ya denge anashauriwa kuwahi mapema kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata huduma stahiki kwani endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, anaweza kupoteza maisha" alisema Dk. Rashid
HOMA YA DENGUE YAUWA MMOJA DAR ES SALAAM
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imewatahadharisha Wananchi kuchukua tahadhari ya kuwepo kwa Ugonjwa wa homa ya dengue hapa nchini.