WABUNGE WASHAMBULIWA LIBYA

Wabunge wawili nchini Libya walipigwa risasi na kuumizwa baada ya kundi la waandamanaji kuwashambulia bungeni katika mji mkuu wa Tripoli.

Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa wawili hao walipigwa risasi walipojaribu kutoroka kutoka katika eneo hilo.

Waandamanaji hao waliokuwa na ghadhabu walilishambulia bunge hilo, huku wakitaka bunge lifungwe na tarehe mpya ya uchaguzi wa mapema itangazwe.

Kumekuwa na wimbi la maandamano nchini humo kutokana na uamuzi wa bunge la nchi hiyo kuahirisha tarehe ya uchaguzi hadi baadaye mwakani.

Waliolishambulia bunge siku ya Jumapili walisema kuwa walighadhabishwa pia na "kutekwa nyara" kwa waandamanaji waliokuwa na kikao nje ya bunge.

Walisema kuwa waliohusika na utekaji nyara huo walikuwa chini ya uongozi wa waasi wanaotumikia amri ya bunge.

Waandamanaji hao ambao wengi wao ni vijana walijihami kwa visu na vijiti, wakalishambulia bunge huku wakiwa na ujumbe kwa wabunge kwa kuimba "jiuzulu, jiuzulu", kwa mujibu wa taarifa ya ashirika la habari la AFP.

Bunge la nchi ya Libya limeshambuliwa mara kadhaa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Nuri Abu Sahmein ambaye ni spika wa bunge hilo aliambia kituo cha televisheni cha Al-Nabaa kuwa maandamano yaliyokuwa ya amani, yalivurugwa na watu waliojihami.

"Wabunge wawili walipigwa risasi pale walipojaribu kutoweka mahali hapo kwa kutumia magariyao," alisema.

Haikuwezakana kubaini papo hapo idadi ya wabunge walioumia.

Picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha waandamanaji wakivuta kile kilichokusudiwa kuwa kiti cha Spika wa bunge hilo nje ya bungena kukichoma.

Mwandishi wa BBC Rana Jawad ambaye yuko Tripoli anasema kuwa bunge la Libya limeshambuliwa mara kadhaa na makundi tofauti, yakiwemo makundi ya waasi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Uchaguzi uliokuwa wa amani ulifanywa na nchi ya Libya katika mwezi wa Julai mwaka jana, ila bado nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ingali inang'ang'ana kupata utulivu, miaka mitatu baadaye tangu kufurushwa kutoka maamlakani kwa aliyekuwa rais, hayati Muammar Gaddafi.