MAOMBI YA ASANTE KWA MUSEVENI

Rais Museveni aliidhinisha sheria yaadhabu kali kwa Mashoga nchini Uganda mwezi Februari

Raia wa Uganda kutoka dini mbali mbali hii leo wamekusanyika katika uwanja wa Kololo mjini Kampala kwa maombi maalum na kutoa shukurani kwa Rais Yoweri Museveni kwa kutia saini mswaada wa sheria unaozuia mapenzi ya jinsia moja.

Viongozi wa dini mbalimbali wakristo na waislamu wamehimiza waumini wao kujitokeza kwa wingi katika ibaada hiyo maalum.

Hii ni mara ya kwanza viongozi wa dini mbali mbali nchini Uganda kujitokeza kwa pamoja na kuandaa Ibaada maalum ya kumshukuru Rais Museveni na kuliombea taifa kuepuka vitendo vya ushoga.

Rais Museveni aliidhinisha sheria hiyo ambayo raia wengi wa Uganda wameipigia debe sana.

Ibaada hiyo maalum inafanyika uwanja wa uhuru wa Kololo mjini Kampala, baada ya karibu mwezi mmoja na nusu tangu rais Yoweri Museveni kuiidhinisha.

Tangu Rais Museveni kuidhinisha sheria hiyo kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa mataifa ya Magharibi yakimtaka kubadili msimo wake, huku baadhi ya mataifa yakipunguza msaada kwa Uganda.

Lakini raia wengi wa Uganda walimsifu Rais Museveni kwa hatua yake.

WANAJESHI TISA WAFUTWA KAZI

Jeshi la angani la Marekani limewafuta kazi maafisa wake tisa katika kambi moja ya silaha za kinyuklia baada ya kudanya katika mtihani.

Afisa mwengine katika kambi hiyo ya Malmstrom mjini Montana amejiuzulu.

Wachunguzi wanasema kuwa maafisa hao wa jeshi walihisi kulazimishwa kupasi asilimia 100% katika kila mtihani.

Uchunguzi huo umebaini kuwa maafisa hao hawakushiriki katika udanganyifu lakini walishindwa kutoa usimamizi wa kutosha.

Udanganyifu huo ulibainika kufuatia uchunguzi wa utumizi wamihadarati katika kambi hiyo.

WAZIRI MKUU KATIKA TUHUMA ZA RUSHWA

Hali ya hewa jana ilichafuka kwenye Bunge la Katiba baada ya mjumbe Ezekiel Wenje kuwatuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kuwa waliwahonga baadhi ya wajumbe wakundi la 201.

Katika tuhuma hizo, Wenje alimtaja Waziri Profesa Jumanne Maghembe, Dk. Shukuru Kawambwa na Gaudensia Kabaka akisema kuwa walitoa rushwa ya vyakula, maji na vinywaji kwa wajumbe hao ili waunge mkono msimamo wa serikali mbili.

Kauli hiyo, iliyotolewa katika mjadala wa mabadiliko ya kanuni, ilisababisha mawaziri hao kunyanyuka kujibu tuhuma hizo, huku Wenje akisisitiza kuwa aliyoyasema ni kweli tupu.

Vilevile baadhi ya wajumbe wanaotoka katika kundi hilo walicharuka na kujaribu kujitetea huku mmoja wapo akitishia kuwa iwapo Wenje asingeomba radhi, asingetoka ndani ya Bunge hilo.

*Hoja ilipoanzia

Wenje, ambaye pia ni mbunge wa Nyamagana (Chadema), alianza kwa kueleza kwamba wapinzani "walilia" sana kuwa Bunge la Katiba lisingekuwa na usawa kutokana na Chama cha Mapinduzi kuwa na wajumbe wengi, ndipo ikaonekana wapatikane wajumbe wengine 201, lakini jambo la ajabu ni kwamba walioteuliwa katika kundi hilo asilimia 80 ni makada wa CCM akiwamo mzee maarufu ambaye ameingizwa kama mganga wa jadi.

Ingawa hakumtaja jina, Wenje alikuwa anamaanisha kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyeteuliwa kupitia kundi la waganga wa jadi.

Kuhusu rushwa, Wenje alisema:"…Sasa kuna wajumbe wa kundi la 201 walipelekwa kwa Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamepeana rushwa, vikao vingi vilifanyika usiku. Hii haikubaliki."

Baada ya kauli hiyo ya Wenje, Profesa Maghembe alisimama ghafla huku akionekana kutaharuki, ambapo Makamu Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan alimpa nafasi ya kujieleza.

Profesa Maghembe alikiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe wa kundi hilo, akieleza kwamba ilikuwa ni katika hali ya ukarimu uliozoeleka miongoni mwa jamii ya Kitanzania.

"Kuna kundi lipo hapa ambalo linafanya kazi ya kudhalilisha wenzao. Ni kweli niliwaalika kwa chakula wajumbe hao kwa taratibu za kawaida, lakini hakuna mbunge hapa anayeshindwa kujinunulia chakula, hakuna anayeweza kupewa rushwa.

"Kwa sababu hiyo ninaomba kiti chako kimtake mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo aniombe radhi. Wenje aniombe radhi," alisema Profesa Maghembe akiwa katika hali ya hasira, huku kukiwa nasauti za kuzomea na kushangilia kutoka kwa wajumbe.

Makamu mwenyekiti pia alifanya jitihada za kuwataka wajumbe kuwa wavumilivu, huku akitoa nafasi kwa Dk. Kawambwa kujieleza akisisitiza kwamba ni tuhuma nzito.

Kawambwa alisema: "Ni kweli nilikutana nao; ni wajumbe ambao wanatoka kwenye taasisi zinazojihusisha na masuala ya elimu, lakini mbona wameshafanya mikutano yao mingine mingi ambayo mimi hawakuniita. Kama mtu akiwa hana hoja bora akae chini.

"Makamu Mwenyekiti alimtaka Wenje aombe radhi kutokana na kauli yake, lakini katika hali ya kushangaza mjumbe huyo alisisitiza kwamba Profesa Maghembe na Dk. Kawambwa wamekiri."

Maghembe amekiri aliwaita wafugaji na wavuvi ndiyo waliokula chakula cha rushwa, pia wapo wengine walienda kwa Waziri Gaudensia Kabaka, kuna ushahidi mama mmoja siwezi kumtaja jina hapa alikwenda huko akafukuzwa, nitakupa jina lake mwenyekiti baadaye.

Aliambiwa kwamba anatoasiri… hoja iliyojadiliwa huko ilikuwa ni kwamba msimamo ni wa serikali mbili… rushwa ya chakula, maji na bahasha walipewa," alisema Wenje na kusababisha kulipuka kwa kelele zaidi.

Wenje aliongeza kuwa kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku.

Alisema wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha.

Baada ya Wenje kukaa, baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 walichachamaa wakitaka kutetea hadhi yao, akiwamo mjumbe kutoka kundi la wafugaji, Esther Juma aliyesema hawatendewi haki kama kundi kusema kwamba walihongwa.Alisema yeye ana ng'ombe 3,000 na asingeweza kwenda kupokea rushwa ya chakula na kumtaka mbunge huyo kuwaomba radhi la sivyo asingetoka mlangoni.

Wakati mjadala huo ukiendelea, mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta aliyekuwa ametoka kwa udhuru, alirejea kimya kimya, na kumtaka Wenje kueleza iwapo anadhani kauliyake haikuwaudhi baadhi ya wajumbe.

Wenje alikiri kuwa ni kweli baadhi ya wajumbe wameudhika kutokana na ukweli aliosema dhidi yao na kuwaomba radhi kwa ukweli huo.

Kauli hiyo ilimfanya Sitta kutangaza kuwa anapeleka suala hilo kwenye Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge na uamuzi utakaotolewa atautangaza bungeni.

TIM SHERWOOD ANAONEKANA BADO AMEKALIA KUTI KAVU

*Benitez, Van Gaal, Laudrup watajwa

Tottenham Hotspur hapajatulia, licha ya ukweli kwamba kocha wao mpya, Mwingereza Tim Sherwood anaonekana kujaribu kufurukuta.

Ushindi aliopata katika mechi ya wikiendi dhidi ya Southampton umempa moyo kwamba huenda Mwenyekiti Daniel Levy atamwacha, lakini kuna kila tetesi kaskazini mwa London kwamba mahasimu hao wa Arsenal wanatafuta kocha mwingine.

Spurs hawaendi vizuri licha ya kusajili wachezaji wengi na ghali wa kimataifa, ambapo ni majuzi tu wametolewa kwenye Kombe la Ligi ya Europa baada ya kupokea kichapo cha 1-0 kutoka kwa Arsenal.

Sherwood wakati mwingine ameonesha hasira na hamaki kwenye eneo la makocha kiasi kwamba katika mechi ya marudiano ya Europa dhidi ya Benfica nchini Ureno aliamua kukaa kwenye jukwaa la watazamaji ili asikorofishane na kocha wa klabu pinzani kama ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza jijini London.

Wakubwa wa Spurs wamekuwa kimya kwa muda, Waswahili wanasema kimya kikuu kina mshindo mkuu, lakini Sherwood anayepambwa na baadhi ya wachambuzi wa Kiingereza amekuwa akisema uamuzi wa mwisho kumwondoa au kumwacha upo mikononi mwa Levy, kama alivyofanya kwa mtangulizi wake, Andre Vilas-Boas.

Wameanza kutajwa makocha wanaoweza kuchukua nafasi hiyo, mmoja wapo akiwa mchezaji wa zamani wa Barcelona na Real Madrid ambaye pia alikuwa kocha wa Swansea, Michael Laudrup.

Mwingine anayetajwa ni Kocha wa Frank de Boer ambaye amewezesha timu yake kutwaa mataji matatu ya ligi yao – Eredivisie na sasa anaelekea kuwapatia kombe kwa mara ya nne mfululizo. Kaka yake De Boer, Ronald, anadai kwamba Spurs walimfuata Januari kumwomba aichukue timu Januari mwaka huu ikashindikana.

Baada ya kufundisha Liverpool kwa mafanikio kisha kwenda kupumzika Mashariki ya Kati kabla ya kuwa kocha wa muda wa Chelsea na sasa Inter Milan, Kocha Rafa Benitez anaweza kurudi tena kwenye Premier League na kuichukua Spurs.

Anaifahamu vyema EPL na hivyo anaweza kuwa kocha mzuri wa kuwavusha Spurs msimu ujao na pia ana historia ya kushinda na kutwaa mataji, kuanzia ya nchi, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Europa. Amepata pia kuwafundisha Valencia wa Hispania.

Spurs wanatajwa pia kutaka kumchukua kocha wa sasa wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal ambaye nafasi yake itachukuliwa huko na Guus Hiddink baada ya fainali za Kombe la Dunia la Fifa mwaka huu nchini Brazil.

Alipoulizwa juu ya uwezekano wake kuwafundisha Spurs, Van Gaal alisema hivi: "Tazama wasifu wangu. Nimetwaa kombe kila msimu enzi zangu nikiwa kwenye klabu…utauliza, je, bado nafanya mawasiliano na Spurs? Wakati utafika ambapo nitaweza kuzungumzia suala hilo."

Van Gaal ametwaa mataji ya Uefa na Ujerumani, Uholanzi na Hispania kwa hiyo ni kana kwamba sifa zake zipo juu mno kufundisha timu kama Spurs ambao inawawia hata ngumu kukamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu ya England. Aweza kwenda Spurs kama hakuna nafasi wazi kwenye klabu nyingine kubwa.

MWIGULU ACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENI

Naibu Katibu wa Fedha, Mwigulu Nchemba katika Bunge Maalum La Katiba alichafua hali ya hewa baada ya kumwambia Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa kwamba wanataka wabunge wa bunge hilo watumie kura ya siri badala ya wazi kwa kuwa ni mashoga.

"Wanaotetea kura ya siri itumike katika kupitisha Katiba ya Watanzania, wanaunga mkono sera za ushoga, ni wale ambao vyama vyao vinazaminiwa na wanaotetea sera za ushoga," alisema Nchemba bungeni.

Kutokana na Kauli ya Nchemba, bunge hilo lilipuka likitaka aombe radhi huku akionyesha kusita kuomba radhi, lakini Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samia Suluhu Hassan alimtaka aombe radhi mara kadhaa.

"Mheshimiwa Mwigulu, naomba usimame na kuomba radhi wabunge wenzako, tafadhali simama".

Baada ya kauli ya Makamu Mwenyekiti Samia, Mwigulu alisimama huku akisema: Mheshimwa Makamu Mwenyekiti, Naomba radhi kwa wote wanaodhani wao wako hivyo kama nilivyosema."

Kauli hiyo ilionekana kuendelea kuwachefua wabunge wa bunge hilo huku wakimzomea na kumtaka aombe radhi kwa kuwa bado alikuwa hajaomba radhi moja kwa moja bali kauli yake imeonekana kuwa na utata.

Kwa mara nyingine, Makamu Mwenyekiti, Samia alisimama tena na kumtaka aombe radhi.

"Mheshimiwa Mwigulu tafadhali omba radhi bila condition, tafadhali, bila kuomba radhi, Bunge haliwezi kuendela, na ninyi wabunge wengine kaeni kimya bila utulivu hatuwezi kusikilizana, tafadhali," alisema Samia.

Baada ya kauli ya Makamu Mwenyekiti, Samia, Mwigulu alisimama tena na kuomba radhi kwa heshima na bunge kuendelea na utaratibu wake.

"Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, nakiheshimu hicho kiti hapo mbele, siwezi kudharau, Naomba radhi kwa wote nilowaudhi," alisema Mwigukulu na kukaa chini.

Basi baada ya kauli ya Mwigulu ya kuomba radhi, shughuli za bunge ziliendelea kama kawaida.

UTURUKI YAIFUNGIA YOUTUBE

Serikali ya Uturuki imebana matumizi ya mtandao wa kijamii wa YouTube, siku moja baada ya mahakama kuamuru kusitishwa kwamuda marufuku ya Twitter ambayo waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan alitangaza wiki jana.

Duru zinasema kuwa halmashauri ya usimamizi wa teknolojia ya mawasiliano nchini humo, imechukua hatua za kuudhibiti mtandao huo ingawa taarifa tofauti zinasema kuwa mazungumzo yanaendelea ikiwa hatua hiyo ichukuliwe.

Baadhi ya watumiaji wa mtandao huo walishindwa kuutumia kwani ulikuwa umebanwa wakati watu wenine katika sehemu mbali mbali walifanikiwa kuutumia.

Awali, kilichoonekana kama mawasiliano kati ya maafisa wa serikali hiyo wakizungumzia Syria yalifichuliwa kwenye mtandao huo wa kijamii.

Inaarifiwa mashauriano hayo yaligusia operesheni ya kijeshi dhidi ya Syria na yaliwashirikisha wakuu wa ujasusi , waziri wa mambo ya njena naibu mkuu wa jeshi.

Shirika la habari la Reuters linasema kuwa haliwezi kuthibitishakanda hiyo ingawa inaonekana kuwa taarifa muhimu sana ya serikali ya Uturuki kuwahi kufichuliwa.

Bwana Erdogan, atakayeshiriki uchaguzi mkuu siku ya Jumapili, anatuhumu mitandao ya kijami wa kueneza taarifa zisizo kweli, na alitishia kupiga marufuku YouTube na Facebook.

JAJI MKUU: KUKIMBILIA MAHAKAMANI NI UPUMBAVU

Jaji mkuu wa Kenya Daktari Willy Mutunga amewakanganya wakenya baada ya kusema wanapaswa kuwatembelea waganga kutafuta suluhu ya matatizo yao badala ya kutegemea tu mahakama ya nchi hiyo.

Jaji Mutunga amewataka wakenya kutumia njia mbadala kama mazungumzo ili kutafuta suluhu wakati wa migogoro.

Jaji huyo amewashauri wakenya kutumia wazee wa vijiji, makanisa na miskiti kutatua migogoro na kusema kuwa yeye binafsi amewaambia watu wa jimbo la Kitui anakotoka kuwatembelea wachawi na waganga kutatua baadhi ya masuala yao.

Jaji mkuu aliyasema haya akiwa Gatundu katika eneo la kati alipokuwa akifungua mahakama mapya ya Kiambu.

Amesema kuwa huduma za mahakama ni ghali mno na akatoa wito kwa wanaotafuta haki mahakamani haswa kuhusu maswala ya familia, kutumia vikao vingine huku akiongeza kuwa mfumo wa kisheria

"Kusema tukutane kortini ni upumbavu mtupu kwa sababu pesa zenu zitaliwa na mawakili."

Afadhali muende kwa wazee au kwa viongozi wa kidini wa mahakama huchukua muda mrefu kuamua kesi na unaweza kusababisha mgawanyiko katika familia.

Amesema kuwa katiba, inaruhusu watu kutumia njia mbadala kutatua migogoro badala ya kutumia masaa mengi na kiasi kikubwa cha fedha kwa mawakili.

Kipengee cha 159 ya Katiba ya Kenya inawaruhusu wakenya kutafuta njia mbadala za kusuluhisha ubishi miongoni mwao.

Kesi zaidi ya 600,000 zipo kortini zikisubiri kuamuliwa na kulinganana jaji mkuu wa Kenya asilimia kubwa ya kesi hizi zinaweza suluhishwa nje ya mahakama.

Katika utamaduni wa Kiafrika ubishi mwingi ulikuwa unaamuliwa na wazee lakini maamuzi yao haswa katika maswala mengine kama vile ubakaji uhalifu na mauaji yakasababisha serikali kuingilia kati kwa kuwafikisha watuhumiwa mahakamani na hivyo ikapunguza hadhi ya vikao hivyo vya wazee miongoni mwa wakenya.

Katika sehemu nyingi nchini Kenya waganga na madaktari wa kienyeji huwa wanatumika kuwanasa wezi na washukiwa wa uhalifu.

Hata hivyo, kumetokea idadi kubwa ya watu wanaonadi huduma zao katika maeneo ya miji na kushukiwa kuwa ni walaghai tu kutokana na idadi kubwa ya magonjwa wanayodai kutibu ikiwemomagongwa ambayo hayana tiba kama vile Ukimwi.

Hoja yake tayari imezua mjadala mkubwa nchini Kenya ,Kiongozi wa Serikali bungeni Adan Duale, akimpuzilia mbali na kudai kuwa hiyo ni dalili kuwa ameshindwa na majukumu yake.

Idara ya mahakama nchini Kenya imelaumiwa kwa kushindwa kutoa uamuzi wa kesi haraka na kupelekea watu wengi kukata tamaa ya kupata suluhu baada ya kesi zao kutoamuliwa kwa zaidi yamiaka 5 hadi miaka kumi.

MAALIM SEIF: HATUTAKI SERIKALI MBILI

Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake cha CUF hakiko tayari kujadili mfumo wa Muungano wa serikali mbili kama inavyotetewa na wabunge wa CCM na Rais Jakaya Kikwete.

Amesema tayari amewaandikia barua Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuwaeleza juu ya msimamo huo.

Maalim Seif alitoa msimamo huo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.

Isitoshe, alisema CUF imebaini kuwa kuna njama za kufuta kipengele katika Katiba ya Zanzibar kinachosema; "Zanzibar ni nchi" na kwamba hiyo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa Wazanzibari kamwe hawatakubali kufanya hivyo.Maalim Seif alisema haikuwa mwafaka kwa Rais Kikwete kukosoa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba yanayotaka mfumo wa Muungano kuwa wa serikali tatu.

Alisema Jaji Warioba aliweka kandoitikadi yake ya CCM katika utendaji wake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuja na uamuzi huo kwa vile ndiyo tiba ya kero za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

"Mapendekezo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba hayakuwa maoni yake, yale ni maoni ya wananchi, Tanganyika imevaa koti la Muungano, ametoa ushahidi wake ili kujenga mwafaka katika kuendeleza Muungano wenye mfumo wa serikali tatu," alisema Maalim Seif.

Alisema Muungano wa serikali mbili hauvumiliki na kama kuna watu wanaendelea kuutetea mfumo huo, Zanzibar inaweza kutumia sheria yake ya kura ya maoni kuwauliza wananchi wanaotaka na wasiotaka jambo hilo.

"Nimemwandikia barua Rais Kikwete, nakala nimempelekea Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, Tanzania Bara wanataka Zanzibar iondoe kifungu cha Katiba kinachosema Zanzibar ni nchi, jambo hilo halitapita...tutafanya kampeni wananchi walikatae," alieleza Katibu Mkuu huyo wa CUF.

Alisema ni jambo la kusikitisha katika hotuba yake alijisahau kama ni mkuu wa nchi na analihutubia Bunge Maalumu badala yake akaegemea kuwa mwenyekiti wa CCM.

Alisema haikuwa sahihi kutoa vitisho na kutaja ikiwa Serikali ya Muungano chini ya Serikali tatu italegalega, jeshi litachukua madaraka ya nchi.

"Rafiki na ndugu yangu Kikwete, usifikiri huu ni wakati ule wa Julius Nyerere, akisema yeye hakuna wa kumpinga.

Mambo ya mebadilika, usijifanye ni Nyerere mpya, hakunaatakayekusikiliza na kubabaika," alisisitiza Maalim Seif.

Alisema ikiwa viongozi wa Muungano wanajiandaa kutisha watu na kusababisha ghasia katika nchi, mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ipo na watakao sababisha fujo na umwagaji wa damu watafikishwa mbele ya mikono ya sheria bila ya kujali nyadhifa na madaraka yao.

Chanzo:Mwananchi

HOMA YA DENGUE YAUWA MMOJA DAR ES SALAAM

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imewatahadharisha Wananchi kuchukua tahadhari ya kuwepo kwa Ugonjwa wa homa ya dengue hapa nchini.

Aidha katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Suleiman Rashid,  kwa Vyombo vya habari imeeeleza kuwa Ugonjwa huo ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam, mwishoni mwa mwezi wa Januari 2014.
 
Hata hivyo hadi sasa idadi ya Wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huo, kuanzia kipindi hicho kuwa ni 70, ikiwa ni wagonjwa 58 Kinondoni, 7 Temeke na 5 Ilala, ambapo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita idadi ya wagonjwa hao iliongezeka mara mbili kuliko siku za nyuma na kusababisha kifo cha mtu mmoja katika hosipitali ya Mwananyamala.
Aidha, Dk. Rashid amesema ugonjwa huo sio mpya hapa nchini, kwani uligundulika Kwa mara ya kwanza Juni 2010 mkoani Dar es Salaam, ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa huo ilikuwa 40, pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huo. 
 
*Wananchi wapewa angalizo
 
Wananchi wameshauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huo, bali wameshauriwa kwenda katika Vituo vya tiba mara wanapoona dalili za ugonjwa huo.
 
Amesema hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa Kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka hapa nchini, ambapo Wizara inaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.
 
Hata hivyo Wizara hiyo imesema jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo, ni Kuangamiza mazalio ya mbu, kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama, kuondoa vitu vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, na magurudumu ya magari
 
Hatua zilizochukuliwa na Wizara hiyo hadi sasa ni pamoja na uchunguzi unaondelea katika Mikoa na Wilaya nyingine, ambapo wameanza na wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa hiyo.
 
*Homa ya Dengue
 
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni weusi na madoadoa meupe yenye kungaa.
 
Mbali na hayo Dalili za ugonjwa huo zimeelezwa kuwa ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususani sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu.
 
 "Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya denge, mgonjwa mwenye dalili za homa ya denge anashauriwa kuwahi mapema kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata huduma stahiki kwani endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, anaweza kupoteza maisha" alisema Dk. Rashid

FIELD MARSHAL ABDUL FATTAH AL-SIS KUGOMBEA URAIS MWEZI UJAO

Mkuu wa majeshi na waziri wa ulinzi Misri, Abdul Fattah al-Sisi, ametangaza kujiuzulu jeshini ili kugombea katika uchaguzi wa urais mwezi ujao.

Wagombea wote wanapaswa kuwa raia.

Akizungumza Kwenye hotuba ya Televisheni huku akiwa amevalia sare ya kijeshi Abdel Fattah El Sissi amesema yeye sio mwanajeshi tena baada ya miaka 44 na kwamba amechukua hatua hiyo ili aweze kutimiza jukumu lingine muhimu.

Ni Bayana bwana Sisi hatakua na kibarua kigumu kujipatia ushindi katika uchaguzi wa Urais.

Anaungwa mkono na idadi kubwaya raia wa Misri na hadi sasa hana wapinzani wowote.

Baadhi ya waliotaka kugombea urais wamejiondoa wakidai kwamba hawataweza kuendesha kampeni zao kwa njia huru.

Wafuasi wake Sisi wanamuona kama kiongozi imara ambaye anaweza kurejesha amani na udhabiti nchini Misri baada ya miaka mingi ya machafuko.

Wakosoaji wake wanasema ana msimamo mkali na amechangia pakubwa katika kusambaratisha na kuhujumu upinzani nchini Misri.

Mkuu huyo wa jeshi atakabiliwa na majukumu mazito ya kufufua uchumi uliofifia , kupambana na uasi na kuileta pamoja nchi iliyogawanyika.

Ameahidi kutekeleza mabadiliko makubwa lakini akaonya kuwa hawezi kufanya miujiza.

KAGAME NA ZUMA WAKUBALI MAZUNGUMZO

Rais Jacob Zuma wa Afrika-Kusini na Paul Kagame wa Rwanda wamekubaliana mjini Luanda Angola, kuanzisha mazungumzo ya pamoja ya kumaliza mzozo wao wa kidiplomasia.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulianza kuzorota pale Rwanda ilipowafukuza maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini, saa chache baada ya Afrika Kusini kuwatimua wanadiplomasia watatu wa Rwanda kuondoka nchini humo karibu wiki tatu zilizopita.

Afrika Kusini ilichukua hatua hiyo baada ya nyumba ya mpinzani mmoja wa Rwanda anayeishi Afrika Kusini Kayumba Nyamwasa kushambuliwa.

Lakini Serikali ya Rwanda ilisema hatua ya kuwatimua maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ni ya haki na ilizingatia uchokozi ambao ulianzishwa na serikali ya Afrika Kusini yenyewe kwa kufukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Rwanda.

Rwanda ilisema kuwa Afrika Kusini ndio ilianza uchokozi kwa kuwatimua mabalozi wake watatu Jenerali Kayumba Nyamwasa, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa majeshi nchini Rwanda, hakuwa nyumbani wakati wa shambulio hilo.

Nyumba yake iliharibiwa huku komputa na baadhi ya nyaraka zilichukuliwa.

Mkutano wa usalama uliofanyika mjini Luanda ulijadili hali kati ya nchi hizo mbili huku viongozi haowawili wakikikutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mzozo huo kutokea.

Rais Zuma alisema kuwa wamekubaliana kusuluhisha mgogoro huo na pia kupata taarifa ya pamoja ili kuweza kusuluhisha tofauti kati yao.

Kadhalika Rais Zuma aliongeza kwamba serikali yake inatekelezawajibu wake wa kimataifa kwa kuwapa hifadhi watu wanaoomba.

Viongozi hao wawili wamekubaliana kukutana kwa ajili ya kuzungumzia swala hilo baadaye.

WASICHANA WA KITANZANIA WALAGHAIWA KUFANYA UKAHABA

Serikali ya Tanzania imesema kuwa imebaini kuwepo kwa biashara haramu ya kusafirisha watoto wa kike kwenda nchini China kwa lengo la kuwashirikisha katika ukahaba ambao unadaiwa kusababisha kunyanyaswa kwa wasichana hao na wengine kuuawa.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimatifa nchini humo Bernard Membe amesema serikali itatuma wachunguzi nchini Uchina kuchunguza biashara hiyo.

Hatua hiyo imechukuliwa mwezi mmoja baada ya msichana mmoja Mtanzania kuuawa kikatili katika mjiwa Guangzhou nchini Uchina.

Waziri Membe amesema huenda baadhi ya wahusika wa bishara hiyo ni Watanzania wanaosafirisha wasichana wa dogo kwa kisingizio cha kuwatafutia ajira.

Baadhi ya wanaosafirishwa hujipata pabaya baada ya kuwasili Uchina ambapo hunyang'anywa hati zao za usafiri na kulazimishwa kushiriki ukahaba.

Baadhi ya wakaazi wa Dar es laam waliozungumza na BBC wameelezea kusikitishwa na vitendo hivyo na kuitaka serikali ichukue hatua.

POLISI WAKAMATA SHABA ZILIZOPORWA

Jeshi la polisi kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa -interpol kanda ya Afrika limefanikiwa kuokoa kwa kuikamata katika kontena shaba yenye thamani ya zaidi ya dola 320,000 sawa na shilingi za kitanzania milioni 500 mali ya mfanyabiashara Fahmy Bin Kleb iliyokuwa imeporwa Februari mwaka huu eneo la mikumi mkoani Morogoro.

Akielezea tukio hilo mmoja wa wenye mzigo huo uliopatikana bwana Salmin Bin Kleb amebainisha kuwa kutokana na upelelezi waliofanya wamegundua kuwa baada ya mzigo huo kuporwa, watekaji wamepitisha mzigo huo maeneo mbalimbali kwa njia za magendo ukiuzwa na watu mbalimbali ikiwemo nchini Kenya na ulikuwa njiani kupelekwa Taiwan kabla ya kuwekewa mtego na kukamatwa katika meli yenye namba 1014 Hermes arrow safmarine ilipopitishwa nchini kuongezea mzigo.

Bwana Kleb pamoja na kupongeza na kushukuru kwa jitihada zilizofanywa na jeshi la polisi ambao wamesha wakamata watu kadhaa kuhusiana na tukio hilo, wizara ya mambo ya nje kupitia balozi wa Tanzania nchini Kenya balozi Batilda Buriani na waziri wa uchukuzi ameomba sheria ifuatwe bila uwepo wa urasimu ili haki itendekea kwa wakati.

MVUTANO WAIBUKA KUHUSU KANUNI BUNGE LA KATIBA

Mwenyekiti wa bunge maalum la katiba Mh Samweli Sitta amelazimika kuliahirisha bunge ili kutoa muda kwa kamati ya kanuni na haki za bunge kukutana kwa lengo la kutafuta tafsiri sahihi ya kanuni ambazo zimeibua mvutano ikiwemo ile kanuni ya 87 kifungu cha pili.

Mvutano huo ulitokana hatua ya mwenyekiti kutaka kutoa ruhusa kwa mwenyekiti wa kanuni na haki za bunge kuwasilisha taarifa yake ndipo Mh Tundu Lisu aliposimama na karatasi aliyodai ni jedwali lilokuwa limeandaliwa kwa lengo la kufanya marekebisho ya kanuni kinyume na utaratibu.

Kutokana na hali hiyo ndipo mwenyekiti alipoamua kuahirisha kikao hicho ili kuruhusu ufumbuzi uweze kupatikana katika kikao kijacho.

Baadhi ya wajumbe wamelaani kitendo hicho na kusema kuwa kinalengo la kurudisha nyuma jitihada za kupatikana kwa katiba mpya huku wengine wakidai kuwa wapo wenzao miongoni mwao ambao wanaagenda tofauti.

Awali dalili za kuharibika kwa mkutano huo zilionekana mapema kufuatia kikao kilichofanywa na wajumbe wa umoja wa katiba ya wananchi ukawa ambao kupitia viongozi wao Mh James Mbatia na Freeman Mbowe walisema zipo njama zimepangwa za kubadili kanuni na hivyo hawatakubali.

ANTI-BALAKA KUTAMBULIKA KAMA MAADUI

Mkuu wa vikosi vya Afrika vya kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ,amesema kuwa vijana wa kulinda amani wa kikristo wanaojulikana kama anti-balaka, watatambulika kama maadui kutoka sasa.

Tangazo hilo la Jean -marie Michel Mokoko linajiri baada ya kadhaa za mapigano ambayo yamesababisha mauaji ya watu 20.

Kundi la Anti-balaka limefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya waislamu baada ya waasiwa kiislamu wa kundi la seleka kuchukua mamlaka mwaka mmoja uliopita.

Jenerali Mokoko pia amelilaumu kundi hilo la anti-balaka kwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya vikosi vya kulinda amani vya Afrika vinavyoshirikiana na wenzao wa Ufaransa ili kuzipokonya silaha pande husika.

Mkuu wa kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu Peter Maurer ameanza ziara yakeya siku tatu nchini humo. Kamati hiyo inasema kuwa taifa hilo linakumbwa na janga la kibinaadamu.

PICHA ZA SATELITE ZA MABAKI YA MH370

Serikali ya Malaysia imesema kuwa picha mpya za Satelite zimeonyeshazaidi ya vifaa miamoja vinavyodhaniwa kuwa mabaki ya ndege yake iliyotoweka zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Waziri wa usafiri wa nchi hiyo, Hishammuddin Hussein, amesema kuwa picha hizo zilizotolewa na Ufaransa, zinaonyesha vifaa hivyo kuwa zaidi ya mita ishirini kwa urefu.

Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi ya mabaki ya ndege hiyo kuonekana.

Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 239, ilikuwa safarini kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Msako uliofanywa baharini na angani, kuitafuta ndege hiyo umeanza tena katika pwani ya Australia baada mawimbi kutulia baharini.

MLINZI WA OBAMA ALEWA CHAKARI

Maafisa watatu kutoka katika idara ya kumlinda Rais wa Marekani Barack Obama katika ziara yake nchini Uholanzi, wamerejeshwa nyumbani kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Jarida la Washington Post nchini Marekani limeripoti kwamba mmoja wa askari hao alipatikana akiwa mlevi chakari kiasi cha kupoteza fahamu katika hoteli mojamjini Amsterdam.

Mapema Jumapili, siku moja kabla ya Obama kuwasili nchini humo, wafanyakazi wa hoteli waliarifu ubalozi wa Marekani nchini Uholanzi kuhusu walivyompata askari huyo katika hali ya kutojitambua.

Msemaji wa idara ya upelelezi Marekani alikataa kutoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo, ingawa alisisitiza kuwa watatu hao wameachishwa kazi kwa muda uchunguzi ukiendelea.

Tukio hilo lilitokea kabla ya Rais Obama kuwasili Uholanzi kwa mkutano kuhusu kawi ya Nuklear.

Shirika hilo la ujasusi limekuwa likijaribu kujisafishia sifa yake hasa baada ya kukumbwa na kashfa mbali mbali.

Mnamo mwaka 2013, majasusi wawili waliondolewa katika kikosi cha ulinzi cha Rais Obama kufuatia tuhuma za kuhusika na kashfa ya ngono na utovu wa nidhamu.

Na mnamo mwaka 2012, majasusi kadhaa waliachishwa kazi kufuatia madai kuwa walikodi makahaba walipokuwa mjini Cartagena, Colombia.

UHURU KENYATTA AHIMIZA USHIRIKIANO AFRIKA MASHARIKI

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amewataka wabunge wa bunge lajumuia ya Afrika Mashariki kuhimiza utekelezaji wa sheria zilizopitishwa na wabunge hao ili ziweze kuridhiwa na kutekelezwa na nchi washirika.

Miongoni mwa sheria zilizopitishwa na bunge hilo ni ushuru wa forodha, soko la pamoja na sarafu ya pamoja, mkataba ambao bado haujaanza kutekelezwa.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa wakuu wa nchi za jumuiya hiyo yuko mjini Arusha makao makuu ya jumuiya hiyo kuzungumza na wafanyakazi na pia kuwafungulia kikao cha bunge kitakachodumu kwa wiki mbili zijazo.

Rais Kenyatta amezidi kusisitiza kuwa ushirikiano wa nchi hizo ndio ukombozi wao kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Rais Kenyatta kadhalika ameelezea nia ya mataifa yote ya jumuiya ya Afrika Mashariki kupambana vikali na tatizo la ujangili na kuutokomeza.

Rais Uhuru Kenyatta pia amesema jukumu la kukabiliana na vitendo vya ujangili ni la wananchi wote kwa sababu lina athari kwa kila mtu mkaazi wa Afrika Mashariki.

Ama kuhusu suala la uhuru wa uhamishaji wa mitaji na uhuru wawananchi wa Afrika Mashariki kutembea kutoka nchi moja kwenda nyingine, amesema jambo hilo linaweza kumalizwa pindi kila nchi itapokamilisha taratibu za matumizi ya vitambulisho kwa raia wake:

Rais Uhuru Kenyatta na ujumbe wake wamerejea nyumbani kwa njia ya barabara kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga.

POPO WAENEZA EBOLA GUINEA

Popo hutumiwa kutengeza kitoweo maarufu sana katika baadhi ya maeneo ya Guinea, lakini sasa inahofiwa kuwa popo wanachangia kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola kusini mwa nchi hiyo.

NI marufuku kula na kuuza popo Guinea

Maafisa nchini humo sasa wamepiga marufuku uuzaji na ulaji wa nyama ya popo katika juhudi za kudhibiti ugonjwa hatari wa Ebola, ambao kufikia sasa umesababisha vifo vya watu 62.

Nchi za kanda hiyo zikiwemo Liberia na Sierra Leone, zimechukua hatua kabambe kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo zikiwemo kuwafanyia uchunguzi wa kiafya watu wanaongia mipakani.

Maafisa wa afya wanapata msaada kutoka shirika la afya duniani na ujumbe wa kuhamasisha watu unapeperushwa kupitia televisheni.

Watu watano kati ya sita walioingia nchini Liberia kutoka Guinea walikua na ishara za ugonjwa huo na wamethibitishwa kufa.

Hata hivyo maafisa wa utawala nchini Liberia bado hawajathibitisha kikamilifu kama kweli walikufa kutokana na ugonjwa wa Ebola.

OBAMA AKUTANA NA NATO NA UMOJA WA ULAYA

Rais Obama yuko mjini Brussels ambapo atakutana na viongozi wa muungano wa Ulaya na shirika la kujihami la NATO, kuzungumzia mzozo wa Ukraine.

Rais Obama anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa usalama Marekani na Ulaya.

Kwenye hotuba muhimu kuhusu sera Rais Obama anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa usalama wa Marekani na nchi za Ulaya na pia kuonya Urusi dhidi ya kukiuka sheria za kimataifa.

Akizungumza mjini the Hague kablaya kuelekea Brussel Rais Obama ameitaja hatua ya Urusi kutwaa eneo la Crimea kutoka kwa Ukraine kama ishara ya udhaifu.

Hata hivyo amesema bado kuna nafasi ya Urusi kusuluhisha mzozo huo kwa njia ya amani la sivyo ikabiliwe na vikwazo zaidi vya kiuchumi. Amesema japo huenda vikwazo hivyo vikaathiri uchumi wa dunia, Urusi ndio itakayoathirika zaidi.

Mkutano huo pia unatarajiwa kuzingatia maswala ya kibiashara napia wasiwasi kwamba Marekani imekuwa ikichunguza kisiri shuguli za washirika wake kutoka nchi za Ulaya.

ORODHA KAMILI YA KINYANG'ANYIRO CHA KILIMANJARO MUSIC AWARD

Orodha Kamili ya waliongia katika kinyang'anyiro cha Kilimanjaro Tanzania Music Awards 2014:


Wimbo bora wa mwaka
1 Number one-Diamond
2 Joto hasira-Lady Jaydee Ft Prof Jay
3 I love u-Cassim Mganga
4 Yahaya-Lady JayDee
5 Kidela -Abdu Kiba Feat Ali Kiba
6 Muziki gani-Ney ft Diamond

Wimbo bora wenye vionjo vya asiliya Kitanzania
1 Kwejaga nyangisha-Batarokota
2 Nalonji-Kumpeneka
3 Bora Mchawi-Dar Bongo massive
4 Tumbo lamsokota-Ashimba
5 Aliponji -Wanakijiji
6 Agwemwana-Cocodo African music band

Wimbo bora wa kiswahili -Bendi
1 Ushamba mzigo-Mashujaa Band
2 Shamba la Bibi -Victoria Sound
3 Chuki ya nini -FM Academia
4 Yarabi nafsi -Mapacha Watatu
5 Kiapo mara 3 -Talent Band

Wimbo bora wa Reggae
1 Niwe na wewe-Dabo
2 Hakuna Matata-Lonka
3 Tell Me-Dj Aron ft Fidempha
4 Bado nahitaji-Chikaka ft Bless p& Lazzy B
5 Bongo Reggae-Warriorsfrom theeast

Wimbo bora wa Afrika Mashashariki
1 Tubonge-Jose Chamelleone
2 Nakupenda Pia-Waire Ft Allain
3 Badilisha-Jose Chamelleone
4 Kipepeo-Jaguar
5 Kiboko Changu-Aman FT Weizal and Radio

Wimbo bora wa Afro pop
1 Number one-Diamond
2 Joto hasira-Jay Dee
3 Kidela-abdul kiba ft Ali Kiba
4 I love you-Kassimu
5 Tupogo-Ommy Dimpoz Ft J Martins
6 Roho yangu-Rich Mavoko


Wimbo bora wa Taarab
1 Wasi wasi wako-Mzee Yusuf
2 Asiyekujua Hakuthamini-Isha Ramadhani & Saida Ramadhani
3 Nipe stara -Rahma Machupa
4 Sitaki shari-Leyla Rashid
5 Fahari ya Mwanamke-Khadija Kopa
6 Mambo bado-Khadija Yusuf
7 Kila muomba Mungu -Mwanahawa Ali

Wimbo bora wa Hip hop
1 Bei ya mkaa-Weusi
2 Nje ya box-Nick wa pili ft Joh Makini and , Gnako
3 Siri ya mchezo-Fid q ft Nature
4 2030-Roma
5 Pesa-Mr Blue Ft Becka Title

Wimbo bora wa R&B
1 Listen-Belle 9
2 Closer -Vanessa Mdee
3 So crazy-Maua ft Fa
4 kama huwezi-rama dee ft jay dee
5 Wa ubani-Ben Pol ft. Alice

Wimbo bora wa kushirikisha/kushirikiana
1 Music Gani-Ney Mitego ft Diamond
2 Joto Hasira-Lady JayDee ft. Prof Jay
3 Kidela -Abdul Kiba ft. Ali Kiba
4 Bila Kukunja Goti-Mwana FA na AY ft. Jay Martins
5 Tupogo-Ommy Dimpoz ft. Jay Martins

Wimbo bora wa Ragga/Dancehall
1 Nishai-Chibwa Ft Juru
2 Sex girl-Dr Jahson
3 My sweet-Jettyman Dizano
4 Feel Alright-Lucky Stone
5 Wine-Princess Delyla

Wimbo bora wa Zouk /Rhumba
1 Yahaya-Lady Jaydee
2 Yamoto-Mkubwa na wanawe
3 Msaliti-Christian Bella
4 Nakuhitaji-Malaika Band
5 Narudi kazini-Beka

Mwimbaji bora wa kike -kizazi kipya
1 Vanessa Mdee
2 Lady Jaydee
3 Linah
4 Maua

Mwimbaji bora wa kiume -kizazi kipya
1 Ben Pol
2 Rich Mavoko
3 Diamond
4 Ommy Dimpoz
5 Cassim Mganga

Mwimbaji bora wa kike -Taarab
1 Khadija Kopa
2 Isha Ramadhani
3 Khadija Yusuf
4 Mwanahawa Ali
5 Leyla Rashid

Mwimbaji bora wa kiume -Taarab
1 Mzee Yusuf
2 Hashimu Saidi
3 Mohamedi Ali aka Mtoto Pori

Mwimbaji bora wa kiume -Bendi
1 Jose Mara
2 Kalala Junior
3 Charz Baba
4 Khalid Chokoraa
5 Christian Bella

Mwimbaji bora wa kike -Bendi
1 Luiza Mbutu
2 Catherine (Cindy)
3 Ciana

Msanii bora wa -Hip hop
1 FID Q
2 Stamina
3 Young killer (Msodoki)
4 Nick wa pili
5 Gnako


Msanii bora chipukizi anayeibukia
1 Young Killer(Msodoki)
2 Walter Chilambo
3 Y Tony
4 Snura
5 Meninah

Rapa bora wa mwaka -Bendi
1 Kitokololo
2 Chokoraa
3 Furguson
4 Canal Top
5 Totoo ze Bingwa

Mtumbuizaji bora wa kike wa Muziki
1 Khadija Kopa
2 Vanessa Mdee
3 Isha Ramadanni
4 Luiza Mbutu
5 Catherine (Cindy)

Mtumbuizaji bora wa kiume wa Muziki
1 Diamond
2 Christian Bella
3 Rich Mavoko
4 Ommy Dimpoz
5 Abdu Kiba

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka -Taarab
1 Enrico
2 Ababuu Mwana ZNZ
3 Bakunde

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka -Kizazi kipya
1 Marco chali-Mj Records
2 Man Water-Combination Sound
3 Mazoo-Mazoo Records
4 Sheddy Clever-Burnz Records
5 Nahreel -Home Town Record

Mtayarishaji bora wa nyimbo wa mwaka -Bendi
1 Allan Mapigo
2 C9
3 Enrico
4 Amoroso
5 Ababuu Mwana ZNZ

Mtunzi bora wa mwaka -Taarabu
1 Mzee Yusuf
2 El-Ahad Omary
3 El-khatib Rajab
4 Kapten Temba
5 Sadiki Abdul
6 Nassoro Seif

Mtunzi bora wa mwaka -kizazi kipya
1 Belle 9
2 Ben Pol
3 Diamond
4 Rama dee
5 Rich mavoko

Mtunzi bora wa mwaka -Bendi
1 Christia Bella
2 Jose Mara
3 Chaz Baba
4 Nyoshi Saadat
5 Kalala Junior

Mtunzi bora wa mwaka -Hip hop
1 Nikki wa Pili
2 Young Killer(Msodoki)
3 Roma
4 FID Q
5 G- Nako


Video bora ya muziki ya mwaka
1 Number one-Diamond
2 Yahaya-lady Jaydee
3 Joto hasira-Lady Jaydee Ft Prof Jay
4 Uswazi takeaway-Chege Ft Malaika
5 Mama Yeyo-Gnako Ft Ben Pol

Bendi ya mwaka
1 FM Academia
2 Mapacha Watatu
3 African Stars(Twanga Pepeta)
4 Akudo Impact
5 Malaika Band
6 Mashujaa Band

Kikundi cha mwaka cha Taarab
1 Jahaz Modern Taarab
2 Mashauzi Classic
3 Five Stars

Kikundi cha mwaka cha kizazi kipya
1 Makomandoo
2 Navy kenzo
3 Weusi
4 Mkubwa na wanawe

MALAYSIA MH-370 ILIANGUKA BAHARINI

Shirika la ndege la Malaysia limewaambia jamaa na familia za abiria waliokuwa wanasafiri kwa ndege iliyotoweka MH370 kwamba ndege hiyo imepotea na kwamba hakuna manusura.

Tangazo hilo limetolewa kwa familia hizo kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi , ambao BBC iliweza kuuona.

Ndege ya Malaysia MH320 ilitoweka ikiwa na abiria 239 baada ya kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur tarehe 8 mwezi huu.

Aidha tangazo hilo limekuja huku juhudi za kutafuta mabaki ya ndege hiyo Kusini mwa Bara Hindi zikimalizika kwa siku ya tano bila mafaniko.

Waziri mkuu wa Malaysia amesema kuwa ndege hiyo ilianguka Kusini mwa Bahari Hindi, bila ya manusura wowote.

Aliambia waandishi wa bahari kuwa udadisi uliofanyiwa data ya Satelite kutoka Uingereza ndio umewathibitishia kwamba ndege hiyo ilimalizia safari yake Magharibi mwa mji wa Perth mbali na eneo lolote la kutua.

Ameomba vyombo vya habari kuheshimu familia za watu waliokuwa ndani ya ndenge hiyo, akisema kuwa anasikitishwa sana kwani kipindi chote walichosubiri taarifa njema , mwishowe imekuja kuwa taarifa mbaya hata zaidi.

Ndege ya Malaysia MH-370, ilipoteza mawasiliano wiki mbili zilizopita na meli za nchi mbali mbali pamoja na ndege zimekuwa zikitafuta angalau mabaki ya ndege hiyo bila ya kupata chochote.

529 WAHUKUMIWA KIFO

Mahakama nchini Misri imewahukumu kifo watu 529 ambao wanasemekana kuwa wafuasi wa Rais aliyeng'olewa mamlakani Mohammed Morsi.

Watu hao walikabiliwa ma mashitaka mbali mbali yakiwemo mauaji ya polisi pamoja uvamizi dhidi ya polisi.

Wafuasi hao wa chama kilichopigwa marufuku, cha Muslim Brotherhood, ni sehemu ya kundi lengine kubwa la watu zaidi ya 1,200 wanaoaminika kuwa wafuasi wa Morsi.

Maafisa wa utawala nchini Misri wamekuwa wakiendesha msako mkubwa dhidi ya wafuasi wa vuguvugu hilo, tangu Morsi kuondolewa mamlakani mwezi Julai mwaka jana.

Maelfu wamekamatwa huku mamia wakiuawa.

Mahakama hiyo ilitoa hukumu baada ya vikao viwili pekee ambapo mawakili wa watuhumiwa walilalamika kuwa hawakupewa muda wa kuwasilisha kesi yao vyema.

Mauaji wanayodaiwa kufanywa na watuhumiwa yalitokea Kusini mwa Misri, mwezi Agosti, baada ya vikosi vya usalama kuvunja kambi mbili za wafuasi wa Morsi waliokuwa wanataka arejeshwe mamlakani.

VIGOGO WA FIFA, UEFA KIKAANGONI

Maafisa wa Fifa akiwemo Rais wa chama hicho, Sepp Blatter na MichelPlatini wamehojiwa kuhusu uhalali wa mkataba wa kuandaa michuano ya Kombe la dunia mwaka 2018 na 2022 kwa Urusi na Qatar.

Rais wa Fifa, Blatter na Platini wa shirikisho la soka barani ulaya Uefa, walishiriki katika mchakato huo mwezi Desemba mwaka 2010.

Mkuu wa kitengo cha upelelezi ndani ya Fifa anafanya uchunguzi namna ambavyo mchakato huo ulifanyika.

Jumla ya Wajumbe 13 kati ya 24 waliokuwa kwenye kamati wamekuwa wakihojiwa kuhusu sakata hilo.

Baadhi ya walioshiriki kupiga kura wamestaafu huku wengine wakiwa wanatumikia adhabu ya kufungiwa halikadhalika kushinikizwa kuacha kazi baada ya kukutwa na hatia ya kuvunja sheria ya Fifa.

Hatua hii haina uhusiano na uchunguzi uliofanywa na gazeti la Daily Telegraph kuhusu maafisa wa zamani wa Fifa, Mohamed Bin Hammam na Jack Warner wanaohusishwa na utoaji wa mkataba wa kuhodhi mashindano yaKombe la dunia kwa Urusi mwaka 2018 na Qatar mwaka 2022.

Juma hili, gazeti hilo limeeleza kuwa shirika la upelelezi FBI linachunguza malipo yanayodaiwa kutolewa na Kampuni ya Bin Hammam kwa Warner na Watoto wake muda mfupi baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.


*REFA AJUTIA KADI YA NYEKUNDU

Refa Andre Marriner huenda akawekwa kando kwenye michezo ya mwishoni mwa juma baada ya kufanya makosa kwenye michuano ya ligi kuu kumwondoa kimakosa mchezaji wa Arsenal wakati timu hiyo ilipopoteza mchezo kwa kuchapwa magoli 6-0 na Chelsea.

Marriner alitoa Penalti wakati wa mchezo wa siku ya Jumamosi baada ya Alex Oxlade-Chamberlain kushika mpira, lakini Kieran Gibbs aliondolewa kimakosa Oxlade-Chamberlain alionekana akimwambia Refa kuwa yeye ndiye aliyeshika mpira, hata hivyo uamuzi wa awali ndio ulikua wa mwisho.

Hata hivyo baadae Mariner alikirina kuomba radhi kwa makosa yaliyojitokeza, akikiri kufanya makosa kutomtambua aliyepaswa kuadhibiwa katika mchezo huo.

Chama cha waamuzi wa mchezo wa kulipwa kimesema kuwa matukio ya kumwadhibu mchezaji kimamkosa ni nadra kutokea na mara nyingi husababishwa na sababu mbalimbali za kiufundi

MAKAHABA WATUMIA HIJAB KUJIPATIA SOKO

Makahaba katika baadhi ya sehemu za mji mkuu wa Kenya , Nairobi, wametupilia Mbali vazi la 'Mini skirtna kuanza kutumia Hijab kama njia ya kuwavutia wateja wao, jambo ambalo limekashifiwa vikali na wakuu wa dini ya Kiislamu.

Hijab huvaliwa na wanawake wa Kiislamu kama ishara ya kumcha Mungu, lakini makahaba katika mtaa wa Eastleigh, viungani mwa Nairobi wanatumia Hijab ili kuwafanya wateja wao kudhania kuawanatoka sehemu za Pwani.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa mtandao wa shirika la habari la Nation mjini Nairobi.

Mwanamke mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa yeye hupata wateja maradufu kwani huvalia vazi hilo la Hijab, wengi wa wateja wake wakimuona kama mwenye nidhamu.

Uchunguzi ulibaini kuwa wanawake wasio wa kiislamu wanavalia vazi hilo ili kuwavutia wanaume ambao wanaamini kuwa wao wana maadili zaidi ya wale wanaovalia nguo fupi au 'Mini Skirt'.

Nguo fupi ni mavazi yaliyozoeleka kwa makahaba sehemu nyingi duniani

Taarifa hiyo imemnukuu Imam mkuu wa msikiti wa Jamia mjini Nairobi, Mohamed Swalihu akisemakuwa ni jambo la kusikitisha sana kuwa Hijab inatumika kwa njia isiyopaswa na makahaba huku akiongeza kuwa pia wanaume wanalitumia vazi hilo kuendesha shughuli za uhalifu jambo ambalo amelitaja kuwa la kishetani linalostahili kukashifiwa vikali.

Hata hivyo chama cha makahaba nchini Kenya kimewatetea makahaba hao wanaotumia hijab huku likidai kwamba wanafanya hivyo ili kukidhi mahitaji ya wateja wao.

Mratibu wa muungano huo, Bi Phelister Abdalla, aliiomba serikali kuhalalisha ukahaba kwa madai ya viwango vya juu vya ukosefu wa ajira.

Mahojiano na makahaba katika mtaa wa Eastleigh yalibaini kwambawanaume hawa kuwa na haja ya wanawake wenye kuvalia nguo fupi badala yake wakipendelea wanawake wa kiislamu na wale wa kutoka Ethiopia.

WAVETNAM WAPANDISHWA KIZIMBANI

Mpanda Katavi

Watu watatu Raia wa Nchi ya Vetnam wamefikishwa kizimbani kwenye Mahakamaya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kuingia kwenye Makazi ya Wakimbizi ya Katumba Wilaya ya Mlele Mkoani hapa Raia hao wa Nchi yaVetnam waliofikishwa kizimbani katikaMahakama ya Wilaya ya Mpanda mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa.

Waliofikishwa kizimbani kwa tuhuma za kuingia kwenye makazi ya Wakimbizi ya Katumba ni Chuqup Ngtun 29,Phamnquyen Huyadang 34 na Tran Huum 29 wote raia wa Nchi ya Vetnam Mwendesha mashitaka Mkaguzi wa Polisi Ally Mbwijo alidai Mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo hapo machi 21 majira ya saa tano asubuhi.

Alidai kuwa siku hiyo ya tukio Raia hao watatu wa Nchi ya Vetnam walikamatwa wakiwa kwenye Kijiji cha Tambazi kilichoko katika makazi ya wakimbizi ya Katumba Wilayani Mlele wakiwa wameingia ndani ya Makazi hayo bila kuwa na kibali.

Washitakiwa wanadaiwa kuwa baada ya kukamatwa na walipohojiwa walidai kuwa wao ni waandisi wa maswala ya mawasiliano na waliingia kwenye makazi hayo kwa ajiri ya kufanya shughuli ya mawasilano ya mitandao mbalimbali.

Washitakiwa hao watatu Raia wa Vetnam baada ya kusomewa mashitaka hayo na mwendesha Mashita walikana mashitaka hayo ambayo walisomewa mahakamani hapoHakimu Mkazi Mawidhi Chiganga Ntengwa aliamuru washitakiwa kwenda mahabusu katika Gereza la Mpanda mjini hadi hapo machi 25 baada ya washitakiwa kukosa watu wa kuwadhamini licha ya mdhamana wao kuwa wazi.


(Katavi Yetu)

TANZANIA KWANZA

RAIS Jakaya Kikwete amewasihi wajumbe wa Bunge maalum kaulimbiu yao iwe Tanzania kwanzana si vyama vyao vya siasa au makundi wanavyoviwakilisha kwenye Bunge hilo.
Aliwaambia wajumbe hao jana kuwa misimamoya vyama ambavyo wajumbe wamepewa na vyama vyao sio jambo baya kama ni suala la kujenga lakini kama ni suala la kubomoa misimamo hivyo haifai.

Rais amwataka wajumbe wazingatie maslahi mapana kwa taifa lao, kwani wananchi wanawategemea wajumbe hao kuipa Tanzania katiba nzuri na si katiba ambayo itakataliwa na wananchi.

"Kaulimbiu yenu iwe Tanzania kwanza naomba msijali makundi yenu kwanza," alisema Rais Kikwete na kusisitiza kuwa maslahi ya taifa shabaha yake ni kujenga nasi kubomoa.

Aliwataka waunganishe mawazo yote pamoja na si kutumia nguvu ili mawazo ya kundi fulani kupita kwani Katiba ni maridhiano na si kuonyeshana umwamba.

Aliwasihi wafanye kazi pamoja licha ya kuwa na itikadi za vyama tofauti, lakini suala la Katiba ni lazima waweke mawazo yao pamoja hata kama wanachukiana kutokana na itikadi zao.

"Mwisho wa siku hapa ni lazima mpige kura, hivyo toeni hoja zinazojenga ili muweze kushawishiana ili katiba tunayoenda kuandika ipatikane," alisema Kikwete.

Alionya kuwa kama wajumbe hao wasiposikilizana kuna hatari Katiba isipatakane kwani kuna makundi ambayo yanataka serikali mbili ambayo yanahitaji kuwashawishi wa upande mwingine wakubaliane nao na wale ambao wanataka serikali tatu nao wana kazi ya kuwashawishi wa kundi lingine nalo wakubaliane nalo.

Alisema Katiba inayotengenezwa nilazima ije na majawabu ya kero mbalimbali zilizopo, lakini akawataka wajumbe hao kuwa mahodari wa kukubali hoja nzuri za upande mwingine wanaopingana nao.

Alionya kuwa kama kuna kundi linataka kulazimisha upande mwingine ni hatari kubwa hivyo njia pekee ni kushirikiana na asiwepo mshindi bali mwisho wa siku wajumbe wote hao wawe washindi.

Alisema wajumbe hao wasipo jenga daraja, hawata afikiana hivyo akasisitiza suala la maridhiano litawale na akapongeza hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa za kuridhiana katika mambo ambayo yanaleta taofuti za kiitikadi.

Aliwaambia wajumbe hao kuwa walichukua muda mrefu katika kujadili kanuni hivyo akawataka waongeze kasi ya kuhakikisha kuwa mambo ambayo watayajadili wanafidia muda ili waende na wakati.

Rais Kikwete amesema wajumbe hao watafanikiwa tu iwapo watakuwa na mijadala ambayo haina ugomvi na vitendo vingine viovu kama ilivyotokea hapo awali.

"Sitarajii kama hili litatokea tena maana kufanya hivyo ni kuwaangusha wananchi ambao tayari walishakata tama kwa mambo ambayo yalikuwa yanafanyika," alisema Rais Kikwete.

LIBYA YAOMBA MSAADA UN

Libya inaiomba jumuiya ya kimataifa kuisaidia kupambana na kile inachosema ni vita dhidi ya ugaidi.

Katika taarifa iliyosambazwa Jumatano jioni serikali ya muda nchini humo ilisema inaomba hususa ni msaada wa Umoja wa Mataifa katika kutokomeza ugaidi kutoka miji ya Libya. Ilisema makundi ya ugaidi yanaendesha operesheni zake huko Benghazi, Sirte na maeneo mengine.

Benghazi ilikuwa eneo lililotegwa bomu ndani ya gari siku ya Jumatatu tukio ambalo liliuwa watu wasio pungua saba.

Serikali imekuwa ikipambana na vitisho vya usalama tangu kuondolewa kwa Moammar Gadhafi mwaka 2011. Makundi mbali mbali ya wanamgambo ambayo yalisaidia kuondolewa kwa kiongozi wa muda mrefu nchini humo yanaendelea kuendesha operesheni zao kwenye maeneo makubwa ya Libya ikiwemo huko mashariki mwa Libya ambako wamechukua udhibiti wa maeneo makubwa.

Viongozi wa muda wameyaagiza majeshi maalumu nchini Libya kukamata tena bandari katika wiki kadhaa zijazo.

Jumatatu kikosi maalumu cha Marekani cha NAVY SEAL kilichukua udhibiti wa lori moja la mafuta ambalo lilijaza mafuta ghafi kutoka bandari inayoshikiliwa na waasi ya As-Sidra kabla ya kuvamia majeshi ya Libya kwenye eneo lakuingia maji ya kimataifa karibu na Cyprus.

Libya inasema waasi hawawezi kuuza kihalali mafuta nchini humo lakini kupoteza udhibiti wa bandari huko mashariki kumezorotesha serikali kuwa na uwezo wake wenyewe wa kuuza mafuta na kusababisha usafirishaji wa nje kushuka kwa asilimia 80.

Umoja wa Mataifa ulijibu juu ya hali hiyo hapo Jumatano kwa azimio la Baraza la Usalama kupiga marufuku uuzaji usio halali wa mafuta ghafi kutoka Libya.

BAN KI MOON ATUA URUSI

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon anatarajiwa kufanya mazungumzo leo na rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow katika juhudi za kutafuta suluhu ya kidiplomasia kuhusu Crimea.

Mkutano huo unafuatia majibizano makali baina ya mabalozi wa Marekani na Urusi katika Umoja wa Mataifa katika kikao cha baraza la usalama la Umoja huo New York.

Balozi wa Urusi Vitaly Churkin alisema watu wa Crimea walitekeleza haki yao kuhusu malengo yao.

Akijibu hoja hiyo balozi wa Marekani Samantha Power alisema kile kinachoitwa kura ya maoni ilikuwa ni maigizo na maelezo ya bwana Churkin yanaonyesha tu ndoto za ubabe wa Urusi.

Churkin alitishia kuwa Urusi inaweza kujiondoa katika masuala mengine ya ushirikiano.

Ziara ya Bwana Ban inafanyika wakati mkutano wa siku mbili wa Muungano wa ulaya ukianza mjini Brussels ambapo viongozi watafanya mazungumzo magumujuu ya uwezekano wa kuweka vikwazo zaidi dhidi ya Urusi.

AUSTRALIA YATOA TAARIFA YA VITU KUONEKANA BAHARINI KAMA NDEGE YA MH370

Waziri mkuu wa Australia amesema kuwa mitambo ya satelite ya nchi hiyo imenasa picha za vitu vinavyoonekana kama vifusi ambavyo huenda ni vya ndege ya Malaysia iliyopotea siku 13 zilizopita.

Waziri mkuu huyo, Tony Abbott, ameambia bunge mjini Canberra kwamba picha za Satelite zimeonyesha vitu viwili vinavyofanana na vifusi vya ndege hiyo.

Taarifa hii imejitokeza karibu wiki mbili baada ya ndege hiyo kutoweka na abiria zaidi ya miambili kutoka mjini Kuala Lumpur Malaysia kuelekea Beijing.

Msemaji wa halmashauri ya usalama wa safari za ndege, John Young, baadaye alisema kuwa vifaa hivyo ambavyo kimoja kina ukubwa wa mita 24, vimeonekana umbali wa kilomita2500 kusini Magharibi mwa pwani ya Australia.

Aliongeza kwamba,vifusi itakuwa vigumu kuviona vifusi hivyo na pia huenda sio vya ndege hiyo.

Wakati taarifa hii ilipotolewa, kulikuwa na ndege ya Australia katika neo hilo , ndege zaidi zinatarajiwa kuwasili katika eneo lenyewe na pia manowari ya jeshi inaelekea huko.

*UDADISI WA PICHA ZA SATELITE

Australia inadadisi picha za Satelite za vitu viwili vinavyodhaniwa kuwa mabaki ya ndege iliyopotea ya Malaysia.

Nchi hio inashirikiana na Norway,New Zealand na Marekani kutafuta mabaki hayo.

Upepo mkali na mvua zilitatiza juhudi hizo hii leo na kusababisha shughuli hiyo kusitishwa. Hata hivyo msako huo utaendelea siku ya Ijumaa.

Bwana Tony Abbott, aliambia bunge kuwa hii ni taarifa mpya na iliyothibitishwa.

Lakini maafisa wakuu nchini Malaysia wametahadharisha kuwa mabaki hayo huenda sio ya ndege yake, ambayo ilipotea siku kumi na tatu zilizopita ikiwa imewabeba watu 239 kuelekea Beijing.

Mabaki hayo yalionekana umbali wa kilomita elfu mbili miatano Kusini Magharibi mwa mji wa Perth.

MUGABE KUFYEKA MISHAHARA YA WAKUU

Rais Robert Mugabe ameamua kupunguza hasira ya umma kwa kukata mishahara ya wakuu wa makampuni yanayo milikiwa na serikali.

Mugabe mwenye umri wa miaka 90 amekuwa akikabiiliwa na shinikizo kubwa kuchukua hatua baada ya kufichuliwa kwa taarifa kwamba wengi wa vigogo hao wanapokea kitita cha hadi dola$500,000 kwa mwezi.

Serikali yake itapunguza malipo ya wakuu wa taasisi hadi dola 72,000 kwa mwaka, yakiwemo marupurupu.

Kipato cha wastani cha mhudumuwa serikali nchini Zimbabwe ni dola $370 kwa mwezi.

" Mbele ya macho ya umma , mishahara hii minono na marupurupu si ufisadi tu bali ni aibu ," Alieleza waziri wa fedha Patrick Chinamasa.

Ilifichuliwa kuwa mkuu wa shirikala habari la taifa la Zimbabwe (ZBC) alikuwa akipokea kitita cha dola 37,050 pesa taslim kila mwezi , ili hali chombo hicho cha habari kinachodhibitiwa na serikali kilishindwa kuwalipa wafanyakazi wake kwa zaidi ya miezisita mwaka jana.

Sakata nyingine iliyojitokeza ni kwamba - moja ya kampuni ya bimma ya matibabu kwa waajiriwa ilikuwa ikimlipa mkurugenzi wake mkuu mshahara kiasi cha dola 230,000 huku kila mwezi ikimpatia marupurupu ya dola $305,499 yamalipo hayo.

Mwandishi wa BBC aliyeko mjini Harare Brian Hungwe , anasema kashfa hiyo iliyobandikwa jina"salarygate", iliibuka mwishoni mwa mwaka jana.

WANAFUNZI WAMKATA MWALIMU NA PANGA

Wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari ya Kibara, wilayani Bunda wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Bunda wakikabiliwa na shtaka la kumshambulia na kumjeruhi kwa panga mwalimu mkuu wa shule hiyo.

Ilielezwa kuwa wanafunzi hao walimjeruhi mwalimu huyo baada ya kutaka kurejeshewa fedha zao zaada kwa vile hawakuwa na mpango tena wa kuendelea na masomo shuleni hapo.

Hata hivyo imeelezwa kuwa uongozi wa shule hiyo ulipinga azma hiyo ya wanafunzi kuacha shule na kurejeshewa fedha zao.

Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed aliwataja washtakiwa hao wanaosoma kidato cha tatu kuwa ni Amosi Shirima (22) na James Athuman (22).

Washtakiwa kwa pamoja wanadai wakutenda kosa hilo Machi 17 mwaka huu.

Mohamed alidai kuwa siku ya tukio,saa 5:00 asubuhi, washtakiwa hao kwa pamoja walimvamia mkuu wa shule, aliyetajwa kwa jina la Awadh Said wakati akiwa ofisini kwake shuleni hapo.

Baada ya kuvamia ofisini kwake, watuhumiwa walimshambulia sehemu mbalimbali za mwili kwa panga na kusababisha majeraha makubwa.

Masoud alisema baada ya mwalimu kuona anashambuliwa, alipiga kelele za kuomba msaada kabla ya watu kujitokeza na kuwakamata watuhumiwa na baadaye kuwapeleka kituo cha polisi.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa hali ya mwalimu huyo siyo nzuri naanaendelea kupata matibabu hospitalini alikolazwa.

Washtakiwa kwa pamoja wamekana shtaka lao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Safina Semfukwe.

Hakimu Semfukwe aliamuru washtakiwa kurudishwa rumande mpaka kesi yao itakapo tajwa Aprili Mosi, 2014.

MTUHUMIWA MWINGINE AKAMATWA MOMBASA

Polisi mjini Mombasa wamemkamata mshukiwa wa tatu wa ugaidi na kunasa silaha zaidi katika gari lililokuwa limebeba mabomu mawili Jumatatu jioni katika mtaa wa Changamwe.

Mshukiwa huyo alikamatwa na polisi wa kupambana na ugaidi waliopata taarifa kutoka katika idara ya ujasusi na mashirika mengine ya usalama.

Inaaminika kuwa mshukiwa huyo alikuwa kiongozi wa njama ya shambulizi iliyotibuka na alikuwa ametoroka wakati washukiwa wenzake wawili walipokamatwa Jumatatu jioni.

Washukiwa waliokamatwa Jumatatu walikuwa wanapanga kufanya mashambulizi katika sehemu ambazo hawakutaja mjini Mombasa.

Walitarajiwa kufikishwa mahakamani Jumanne ingawa polisi waliomba muda zaidi kufanya uchunguzi.

Kwa mujibu wa kamishna mkuu wa Mombasa, wataalamu wa mabomu walitegua mabomu hayo.

Pia walinasa mitungi sita yenye uzito wa kilo 60 yenye uwezo wa kulipua majengo, maguruneti sita, bunduki aina ya AK-47 na risasi 270 pamoja na vifaa vitano vya kulipua mabomu ikiwemo simu ya mkononi.

Maafisa wa ujasusi waliweza kunasa mawasiliano yao na kuweza kuwakamata washukiwa hao.

Mombasa ni mji unaosifika kwa utalii lakini hivi karibuni umekuwa ukikumbwa na harakatiza vijana wa kiisilamu kukumbatia itikadi kali za kidini.

AVB AIBUKIA URUSI HUKO ST. PETERSBURG

Aliyekua Kocha wa Tottenham na Chelsea, Andre Villas-Boas ameridhia kuingia mkataba wa miaka miwili na klabu ya Zenit St Petersburg, taarifa za klabu hiyo ya Urusi zimeeleza.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 36, aliyetimuliwa na Spurs mwezi Desemba atachukua nafasiya Luciano Spalletti.

Villas-Boas atatangazwa rasmi kuwa Kocha mkuu wa Timu hiyo tarehe 20 mwezi Machi.

Kibarua cha Spalletti kiliota nyasi baada ya Spurs kupoteza mchezo wa kwanza hatua ya 16 bora ambapo ilipigwa mabao 4-2 na Borussia Dortmund.

Villas-Boas alikuwa sehemu ya kikosi cha uongozi cha Jose Mourinho kabla ya kujiunga na Academica na Porto za nchini kwake Portugal.

Aliwezesha ushindi wa kombe la ligi, ligi ya Europa katika msimu wake wa kwanza akiwa na Porto kabla ya kujiunga na Chelsie mwaka 2011, lakini alitemwa na timu hiyo mwezi March mwaka 2012 baada ya kushindwa kuifikisha timu hiyo kwenye viwango bora.

AFISA ELIMU AWEKEWA JENEZA LA PAKA

Familia ya afisaa mmoja wa Elimu nchini Kenya imepigwa na butwaa baada ya kupata jeneza dogo likiwa limewekwa kwenye mlango wao mjini Kisumu Magharibi mwa Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Taifa Leo, familia ya Afisaa huyo Elias Oganda, mwenye umriwa miaka 56, ilipata jeneza hilo dogo likiwa na mzoga wa Paka njeya mlango wao na sasa inaishi kwa hofu kubwa.

Afisaa huyo anayefanya kazi katika wizara ya elimu, alisema kuwa hii ni mara ya nne katika miezi sita kupata jeneza kama hilo nyumbani kwake.

Polisi walifungua jeneza hilo na kupata mzoga wa Paka ndani yake. Walishuku kuwa Paka huyo alinyongwa na kuwekwa ndani ya jeneza hilo kwani hapakuwa na dalili yoyote ya damu.

Afisaa mkuu wa polisi katika eneo hilo amesema kuwa hili sio tukio la kwanza kushuhudiwa katika eneo hilo.

Bwana Oganda naye alisema kuwa jeneza hilo liligunduliwa na mkewe Joyce Oganda, mwenye umri wa miaka 50, usiku wa manane alipotoka nje kujisaidia.

''Nia ya mtu aliyefanya kitendo hicho haijulikani, mimi sijawahi kuhusika na mzozo wa ardhi'' alisema bwana Oganda aliyeongeza kuwa familia yake haijwahi kupata utulivu kwa mwaka mmoja uliopita kwani amekuwa akifanyiwa uchawi mara kwa mara.''

''Hii ni ardhi ya babangu na sielewi kwa nini watu wanataka kunitishia maisha kwa kutumia uchawi.''

Wakazi walikita kambi katika nyumba ya bwana Oganda kushuhudia mchawi aliyeletwa katika nyumba hiyo kutoka Sirarempakani mwa Kenya na Tanzania kujaribu kujua ni nani aliyehusikana kitendo hicho.

CHINA YAANZISHA MSAKO WA ARDHINI WA NDEGE YA MH370

Serikali ya China imeanza juhudi za kuitafuta katika ardhi yake ndege ya Malaysia iliyotoweka mwishoni mwa wiki jana.

Hii ni sehemu ya juhudi za kimataifa zinazoendelea kuitafutandege hiyo.

Wataalamu wanaoendesha shughuli hiyo wanalenga zaidi maeneo mawili ya nchi hio, Kaskazini na Kusini.

China imesema kuwa hakuna abiria yeyote wa nchi hiyo aliyekuwa katika ndege hiyo amehusishwa na ugaidi.

Ndege hiyo ilitoweka tarehe 8 mwezi Machi ikiwa imewabeba watu 239. Nchi 26 zinahusika na msako huo.

Malaysia inasema kuwa ndege hiyo ilibadili mkondo na huenda ilipaa kuelekea Kusini au Kaskazini.

Wapelelezi wanachunguza uwezekano wa ikiwa abiria au rubani na rubani mwenza walihusika na tukio la kutoweka kwa ndege hiyo.

Raia 153 wa China walikuwa katika ndege hiyo ambayo ilikuwainatoka Malaysia kuelekea mjini Beijing, China.

URUSI YAITAMBUA CRIMEA KAMA NCHI HURU

Rais wa Urusi Vladmir Putin ametia saini ilani ya katiba inayotambua jimbo la Crimea kama taifa huru. Hatua hiyo inajiri muda mfupi baada ya marekani na Muungano wa Ulaya kutangaza vikwazo dhidi ya maafisa wa serikali ya Urusi na wa Ukraine waliohusika na njamaya Moscow kuiondoa Crimea katika Ukraine.

Rais Obama amesema kuwa anataka kuweka bayana kwamba kutakuwa na adhabu kwa wale walioanzisha mikakati ya Crimea kujitenga na Ukraine akiongeza kuwa vikwazo zaidi vitatolewa. Hata hivyo amesisitiza kuwa badokuna njia ya kusuluhisha mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia.

Awali bunge la Crimea lilitangaza rasmi kuwa jimbo hilo liko huru kutoka kwa Ukraine na kutoa maombi ya kujiunga na mataifa yanayobuni muungano wa Urusi.

Balozi wa Marekani nchini Ukraine, Geoffrey Pyatt, ameiambia BBC kwamba ilani iliyotiwa saini na rais Putin kutambua uhuru wa Crimea haitabadili mtizamo wa Marekanikuhusu hali ilivyo." Kadri marekani inavyozingatia, hapatakuwa na mabadiliko kuhusiana na makadirio yetu kuhusu hali, mtizamo wetu wa Crimea kama sehemu ya Ukraineiliyo huru na mtizamo wetu kuhusu kwamba kura ya maamuziya siku ya jumapili iliyofanyika baada ya uvamizi wa kijeshi uliotekelezwa na Urusi ni kinyume na sheria kwa vyovyote," anasema.

Msemaji wa Ikulu ya White House Jay Carney, alipoulizwa na waandishi wa habari ikiwa rais Putin atalengwa baadaye na vikwazo hivyo amesema kuwa Marekani haitawasaza baadhi ya watu katika uwezekano wa kuwawekea vikwazo."

Uwezo wa kutoa vikwazo dhidi ya watu mbali mbali upo. Tutatoa tathmini kuhusu hatua mwafaka wakati hali ikiendelea kubadilika.

Hatutawasaza baadhi ya watu. Kutakuwa na gharama kwa Urusi, Gharama ya ziada itakayotolewa kwa Urusi, ikiwa Urusi hatabadili mwelekeo hapa kuhusiana na jinsi inavyoshughulikia hali nchini Ukraine," anasema.

Miongoni mwa maafisa waliolengwa na vikwazo vya Marekani na Muungano wa Ulaya ni maafisa wa ngazi ya juu katika utawala wa jimbo la crimea, rais wa Ukraine aliyengolewa madarakani Viktor Yanukovich, naibu waziri mkuu wa Urusi, wabunge wa Urusi na makamanda wa jeshi.

WALIMU WAONGOZA KWA KUIBIWA MISHAHARA

IMEELEZWA kwamba fedha za walimu wengi huibwa kwa njia ya mtandao licha ya umuhimu wa kada hiyo katika jamii ambayo huzalisha wataalamu mbalimbali.

Hayo yalibainishwa jana na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi, Abrahamu Augustino, wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 77 yenye thamani ya sh milioni tano kwa Shule ya Msingi Muungano wilayani Bukombe, Geita.

"Ni kweli kwamba walimu wengi wanaongoza kwa kuibiwa fedha zao hasa mishahara ambayo hupita benki," alisema meneja huyo.

Augustino alisema benki yake inapokea malalamiko mengi yawalimu kupoteza fedha zao kwenye mtandao wa mashine za fedha (ATM) na kwamba baada ya kuhakiki kwa mfumo wa kamera za benki hukuta sura za wao kwa wao kuibiana ama watu wanaowakopa na kuweka kadi zao za benki kuwa dhamana.

POLISI WANNE WAFUKUZWA KAZI

ASKARI polisi wanne jijini Dar es Salaam wamefukuzwa kazi, kutokana na kile kilichodaiwa ni kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema kufukuzwa kwao kumetokana na uchunguzi uliofanyika na kubaini ushiriki wao katika matukio ya uhalifu, likiwemo la wizi la Machi 9, mwakahuu eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Kova alitaja polisi hao, ambao kwa mujibu wake walifikishwa kwenye Mahakama ya Kijeshi kuwa ni Koplo Rajabu Mkwenda maarufu kama Ugoro, aliyekuwa Makao Makuu ya Polisi.

Wengine ni Konstebo Simon wa Kituo cha Kikuu cha Polisi, Konstebo Albernus Koosa wa Bendiya Polisi, Dar es Salaam na Konstebo Seleman wa Kituo cha Polisi Kigamboni. Kamanda alisema kabla ya kufukuzwa askari hao, walishitakiwa katika Mahakama ya Kijeshi na kupatikanana hatia.

Alisema jalada la kesi hiyo na majalada ya watuhumiwa wengine ambao ni raia, yatapelekwa kwa mwanasheria wa serikali, kabla ya kuwafikisha mahakamani kwa makosa ya jinai.

"Uchunguzi wa kina umefanyika na watuhumiwa 11 (wakiwemo polisi hao wanne) wamepatikana ndipo ilipobainika kwamba askari polisi hao walishiriki katika tukio hilo," alisema Kamanda Kova. Kwa mujibu wa kamanda, katika tukio hilo, raia wengine wanaotuhumiwa kwa ujambazi walikamatwa wakati wakitoroka baada ya gari lao kugonga mti.

Watuhumiwa hao ni Gerald Mtutu (36), Charles Mbelwa (37), Adam Mohamed (40), Ally Salum (38), Salum Mussa (22), Juma Hamis (29)na Juma Ngwele (50).

Inadaiwa siku hiyo Machi 9, walifika katika ofisi za kampuni ya Wachina ijulikanayo kama Hong Yang, inayojishughulisha na ujenzi na useremala.

Kamanda Kova alisema watuhumiwa walitambuliwa na mashahidi mbalimbali.

Kamanda alisema polisi haitavumilia vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya utumishi wake.

Alisema hatua hizo ni fundisho kwa askari yeyote, atakaye jaribu kwenda kinyume na maadili ya kazi.

"Wamefukuzwa kwa fedheha na kawaida ukifukuzwa kwa fedheha huna stahili yoyote. Ikumbukwe kuwa tuko katika mpango wa maboresho kwa jeshi la Polisi kwa maana hiyo hatuwezi kuwa na watuambao ni wachafu ndani yetu," alisema.

WAJUMBE WAMGOMEA WARIOBA

Uwasilishwaji  wa rasimu ya katiba uliokuwa ufanywe na mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba Mh jaji Joseph  Warioba  umeshindwa kufanyika baada  ya baadhi ya wajumbe ambao ni wanachama wa umoja wa katiba ya wananchi kusimama na kuanza kuzomea, kupiga makofi  na  kuzungumza bila ya utaratibu wa kipinga kuwasilishwa kwa rasimu hiyo kwa kile walichodai  kuwa  kanuni zimekiukwa.

Siyo kwamba ni sokoni bali ni wajumbe wa bunge maaalum la katiba ambao wanapinga kuwasilshwa kwa rasimu hiyo ambapo licha ya mwenyekiti wa bunge hilo Mh Samweli  Sitta kumtaka jaji Warioba  kuendelea haikuwezekana.

Baada ya  hali hiyo wabunge ambao wanaunga mkono kitendo kilichofanyika cha  kuzuia kuwasilishwa kwa rasimu hiyo ambapo wali kilaani vikali.

Aidha kwa upande wa wabunge ambao wanaunga  mkono kilichotokea bungeni wamesema mwenyekiti  ameanza kwa kukiuka kanuni kana kwamba wakati zinapitishwa hakuwepo na hivyo hawawezi kamwe  kukubali kuburuzwa.

Hata hivyo licha ya kusitishwa kwa bunge hilo wajumbe waliendelea kukaa ndani ya ukumbi huo  wakipiga soga hatua ambayo pia ilipelekea kutolewa kwa tangozo lingine la kuwataka watoke nje.

AL SHABAAB WASHAMBULIA AMISOM

Kundi la wanamgambo la Al Shabaab nchini Somalia, linasemakuwa limeshambulia msafara wa magari ya kikosi cha Muungano wa Afrika, AMISOM, karibu na mji mkuu Mogadishu.

Walioshuhudia shambulizi hilo wanasema kuwa walisikia milipuko mikubwa katika eneo la Alamada lililo umbali wa kilomita20 kusini mwa mji mkuu.

Shambulizi lilitokea wakati magari ya kikosi hicho yalipolipukiwa na mabomu yaliyokuwa yametegwa ndani ya gari.

Al Shabaab wamasema kuwa wanajeshi saba wa AU waliuawa lakini AMISOM imesema kuwa hapakuwa na majeruhi wowote.

Kikosi hicho kilisema kuwa kilimpiga risasi dereva wa gari hilo alipokuwa anawakaribia ana hivyo kutibua shambulizi hilo.

ALBINO AUA NA KUCHUNA NGOZI MTOTO

POLISI mkoani Singida inawashikilia wanawake wawili, mmoja wao akiwa mlemavu wa ngozi `albino', kwa tuhuma ya kuua na kumchuna ngozi mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Geofrey Kamwela aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Hidaya Omari (20), ambaye ni albino na ni mama wa mtoto aliyeuawa na Neema Paulo (35) ambaye ni mamawa Hidaya.

Watuhumiwa wote ni wakulima na wakazi wa Kijiji cha Nkalankala, Kataya Mwanga, Tarafa ya Nduguti Wilaya ya Mkalama mkoani Singida.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, tukio hilo lilitokea saa 1.30 asubuhi Machi 13, mwaka huu kijijini hapo ambapo mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya kisima cha maji chenye kina cha mita moja ukiwa unaelea.

Alisema kuwa uchunguzi wa awali wa Polisi ulibaini kuwa kabla ya mtoto huyo kuuawa, alinyongwa shingo yake, kisha kuchunwa ngozi katika sehemu zake za siri na kutumbukizwa ndani ya kisima hicho.

Kamanda Kamwela alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo kinaweza kuwa ni imani za kishirikina na kwamba mara baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

MALAYSIA YAOMBA DATA

Wizara ya usafiri ya Malaysia inasema kuwa imeomba ushirikiano wa nchi zote kwenye njia mbili ambapo ndege iliyopotea juma lilopita huenda kuwa imepita.

Imeomba msaada wa data kutoka Satelite na Radar na msaada katika shughuli za msako.

Uchunguzi pia unafanywa kuhusu marubani wawili wa ndege hiyo na nyumba zao zimepekuliwa.

Polisi wa Malaysian wanasema pia wanachunguza historia ya wafanyakazi wengine wa ndege na abiria wote pamoja na wahandisi waliohudumia ndege hiyo.

Waziri wa Usafiri, Hishammuddin Hussein, alisema sasa nchi 25 zimehusika katika msako.

Alisema sasa wanalenga zaidi njia mbili ambazo pengine ndege hiyo ilifuata - kaskazini au kusini.

95.5% WATAKA CRIMEA KUJIUNGA URUSI

Asilimia 95.5 ya wapiga kura wanaunga mkono Crimea ijitenge kutoka kwa Ukraine na kujiunga na Urusi.

Maafisa waliosimamia kura hiyo ya maoni amesema kuwa baada ya kuhesabu takriban nusu ya kura zilizopigwa.

Kiongozi wa jimbo hilo amesema kuwa atatuma rasmi ombi la kutaka kujiunga na urusi hapo kesho.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa ataheshimu uamuzi wa wapiga kura.

Marekani na Jumuiya ya Ulaya wametaja kura hiyo ya Maoni kuwa ni haramu na wamesema kuwa hawatatambua matokeo yake kwani ilipigwa katika ''hali yavitisho vya kupigwa'' vilivyotolewa na wanajeshi wa Urusi.

Siku ilikamilika kwa amani katika rasi hiyo, ingawa kulikuwa na maandamano katika katika miji iliyoko Mashariki mwa Ukraine, kukiwemo mapigano mengine katika Doneski.

Watu wanaounga mkono Urusi walichukua utawala wa jimbo hilola Crimea tangu mwezi Februari.

WATU WATATU WAFIA BAHARINI

Watu watatu mkoani Mtwara wamepoteza maisha kufuatia kuzama kwa mtumbwi waliokuwa wakisafiria katika Bahari ya Hindi kutoka Kitongoji cha Mwale kuja Mtwara Mjini kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen aliyeongea na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula akiwa ameongozana na uongozi wa mkoa, alisema ajali hiyo ilitokea saa 5 asubuhi mita kama 100 kutoka eneo la ufukwe wa kienyeji baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupatwa na misukosuko.

Zelothe alisema ajali hiyo imesababisha vifo vitatu, majeruhi 21 wakiwemo watoto wadogo wawili kati ya mwaka mmoja na kuwataka wananchi kuwa makini na vyombo wanavyotumia kusafiria ikizingatiwa kwa sasa hali ya hewa siyo nzuri kutoka na na mvua zinazoendelea kunyesha.

Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Mwanahamis Juma (31) na Habiba Masoud (13) wote wakazi waMwalena Rahma Abdul (25) mkazi wa kitongoji cha Ngw'ale.

Naye Mkuu wa Mkoa, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia alieleza kuwa ajali hiyo imesikitisha sana nakwamba kifo hakina matarajio kwani waliokumbwa na mkasa huo walikuwa wakienda kwenye shughuli zao za kila kujitafutia kipato.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Dk Shaibu Maarifa alikiri kupokea majeruhi na maiti za ajali hiyo na kusema kuwa wanawahudumia ipasavyo ili waweze kurudi katika hali zao za kawaida.

Mmoja wa majeruhi walionusirika katika ajali hiyo, Sophia Kassim (28) alimwambia mwandishi wa habari hizi wakati wa mahojiano kuwa mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulijaza watu kupita kiasi na kwamba abria wote walikuwa wanawake isipokuwa dereva na msaidizi wake.

NASSARI AUMBUKA BUNGENI

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Joshua Nassari, juzi alijikuta akiumbuka bungeni baada ya kushindwa kutaja kanuni aliyoitumia, kuomba mwongozo.

Hali hiyo ilitokea muda mfupi kablaya wajumbe kupiga kura za kumchagua Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Kuumbuka kwa mjumbe huyo ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Mshariki, kulitokana na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho, kumtakakutaja kanuni aliyoitumia.

Hata hivyo, baada ya kusita kwa muda Nassari bila kutaja kanuni aliyoitumia, alisema wajumbe wengi hawajasikia utaratibu unaotumika katika upigaji kura kwa sababu walichelewa kwenye msongamano wa watu getini.

"Wengi wetu tumeingia tukiwa tumechelewa kwa sababu wengi tunapita katika geti moja. Ningependa ufafanuzi wako kuhusuaina ya kura tunayokwenda kupiga ni ya wazi au ya siri,"alisema.

Hata hivyo, kificho alimjibu kuwa kura zitakazopigwa kumchagua mwenyekiti zitakuwa ni za siri.

Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Bunge hilo kupitisha kanuni za uendeshaji wake ambapo hata hivyo nyingine bado zimekuwa na mgongano wa maridhiano kwa baadhi ya wajumbe kutaka ufafanuzi zaidi.

JK AWAAPISHA VIONGOZI BUNGE LA KATIBA

Rais Jakaya Kikwete jana aliwaapisha Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, hali inayoonyesha kuwa kazi ya Bunge sasa imeanza.

Walioapishwa ni Yahaya Hamisi Hamad ambaye anakuwa Katibu na Dk Thomas Kashilila anashika nafasiya Naibu Katibu wa Bunge hilo.

Shughuli za kuapishwa kwa makatibu hao, zilifanyika katika Viwanja vya Ikulu ndogo iliyoko eneo la Uzunguni mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Viongozi hao ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Mwenyekiti Mteule wa Bunge , Samuel Sitta na Makamu wake Samia Suluhu Hassan.

Baada ya kiapo hicho, Rais Kikwete alikutana na Pinda, Sitta na Suluhu.

Hata hivyo mazungumzo yao yalikuwa ya faragha.

Akizungumzia nafasi yake Katibu waBunge, Yahaya Hamad, alikiri kuwa kazi iliyoko mbele yake ni kubwa lakini ana matumaini makubwa kwamba ataifanya kwa uadilifu mkubwa wa hali ya juu.

Hamad alisema changamoto kubwa anayoiona ni mwingiliano wa masilahi ya wanasiasa kwa sababu wengi wametanguliza misimamo ya vyama.

"Mimi ningewashauri wanasiasa kuacha kila kitu ili tuweze kufanya kazi ya watu iliyotuleta Dodoma, ili tuweze kupata Katiba nzuri itakayodumu kwa muda mrefu. Wanasiasa lazima wakubali kuwa nchi kwanza na vyama baadaye," alisema Hamad.

Kwa upande wake Dk. Kashillilah alisema atatumia uzoefu wake kumshauri na kumsaidia katibu na wenyeviti wa Bunge ili ndoto ya kuwa na Katiba nzuri itimie.Hata hivyo, alikanusha madai kwamba Katiba Mpya haitapatikana kutokana na kelele za wanasiasa.

KIJANA MMOJA AMEKUFA BAADA YA KULIPUKIWA NA SIMU

ALI Bakari Ali (20) mkazi wa Kisima Majongoo mjini Unguja amekufa baada ya simu yake aliyokuwa akitumia ambayo ilikuwa imeunganishwa na chaja ya umeme kupata hitilafu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema Ali alikufa baada ya kupata mshtuko wa umeme unaotokana na simu yake iliyokuwa imewekwa katika chaja ya umeme huku akifanya mawasiliano.

"Ni kweli tumepata taarifa ya kifo cha kijana Bakari Ali ambaye alikuwa akisikiliza simu yake iliyokuwa imewekwa katika chaja ya umeme na kusababisha mshtuko mkubwa," alisema.

Kamanda Mkadam alitoa wito kwa wananchi na kuwataka wakati wanaposikiliza simu zao kwanza kuziondoa katika umeme ili kuepusha ajali.

AHUKUMIWA KUNYONGWA MPAKA KUFA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga imemhukumu Malambi Lukwaja (47) mkazi wa Kijiji cha Igalula Tarafa ya Kabungu Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.

Mshitakiwa alitiwa hatiani na mahakama hiyo kwa kumuua kwa kukusudia Ibrahim Juma (44) mkaziwa kijiji hicho cha Igalula. Inadaiwa alitumia shoka kumchinja kisha kuufukia ardhini mwili wa mdai wake.

Hukumu hiyo ilitolewa jana katika kikao cha Mahakama Kuu kilichofanyika katika mahakama ya wilaya ya Mpanda na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Jaji Kasukulo Sambo.

Awali Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Njoloyota Mwashubila alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 9 mwaka 2009 katika muda usiofahamika.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa siku hiyo ya tukio marehemu alimuaga mkewe aitwaye Hamisa Hassan kuwa anakwenda nyumbanikwa mshitakiwa Malambi Lukwaja ili kuchukua magunia yake ya mpunga ambayo alikuwa akimdai ambapo walikubaliana amlipe magunia hayo ya mpunga baada yakuvuna.

Mwanasheria huyo wa Serikali aliieleza mahakama hiyo kuwa tangu siku hiyo alipoondoka marehemu hakurudi nyumbani hivyo kusababisha mke wake apateshaka na kutoa taarifa kwa ndugu wa marehemu juu ya kutoonekana kwake kwa kipindi cha wiki tatu.

Alieleza ndugu wa marehemu walipopewa taarifa hizo waliamua kumfuatilia nyumbani kwa mshitakiwa ambapo aliwaeleza marehemu alifika kwake na alishaondoka nyumbani kwake baada ya majibu hayo ndugu hao waliamua kurudi nyumbani.

Mwashubila alidai kuwa wakati ndugu hao wa marehemu wakiwa wanarudi nyumbani waliitwa na jirani yake na mshitakiwa ambae aliwatahadharisha kutojenga mazoea ya kwenda kwa mshitakiwa kwani kuna mtu mmoja alikwenda hapo na hajaonekana tena.

Alieleza baada ya kuelezwa hivyo ndugu hao walikwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji na kisha walimkamata mshitakiwa na kumpeleka kituo cha Polisi cha Mpanda.

Mwanasheria huyo aliendelea kueleza baadhi ya wanakijiji walibaki nyumbani kwa mshitakiwa wakiendelea kumhoji mkewe ambae aliwaeleza marehemu siku hiyo aliondoka na mumewe kwenda shamba, lakini kesho yake mshitakiwa alirudi akiwa peke yake na alipojaribu kumuuliza mume alikuwa mkali.

Ilidaiwa mke huyo wa mshitakiwa aliamua kuwapeleka lilipo shamba lao la mpunga na walipofika walishituka kuona kuna eneo limefukuliwa ambapo waliamua kulifukua eneo hilo ghafla waliona miguu ya marehemu ndipo walipotoa taarifa polisi ambao walifika kwenye eneo hilo na kuendelea na ufukuaji mwili wote wa marehemu ukiwa umechinjwa na kiwiliwili chake kutenganishwa na kichwa ambapo kwenye kichaka waliiona baiskeli ya marehemu na nguo zake.


Chanzo: Habari leo

WANAFUNZI DARASA LA SABA WAOANA

MWANAFUNZI aliyehitimu Darasa la Saba mwaka jana, jina tunalo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, kwa madai ya kumuoa msichana waliyekuwa wakisoma naye darasa moja mwenye umri wa miaka 15.

Binti huyo alifanikiwa kupata nafasiya kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Chala wilayani Nkasi, lakini ameshindwa kujiunga kwa kuwa ni mke wa mtu. Wawili hao walikuwa wakisoma Shule ya Msingi Kacheche kijijini Kacheche wilayani Nkasi.

Mshitakiwa ambaye kwa sasa ni mkulima katika kijiji cha Kacheche alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Ibrahim Mgalamalira ambapo alikana shtaka hilo. Mtuhumiwa alidai kuwa anafahamu kuwa amemaliza elimu ya msingi, lakini hakuwa na taarifa kama alikuwa amechaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari mapema mwaka huu.

Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alimuoa msichana huyo, Februari 24, mwaka huu na kuishi naye nyumba moja kijijini Kacheche kama mume na mke kwa siku sita hadi alipotiwa nguvuni Machi 3, mwaka huu.

"Msichana huyu bado ni mwanafunzi kwa kuwa alichaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Chala wilayani hapa lakini ameshindwa kuendeleana masomo kwa kuwa alikuwa ameolewa na mtuhumiwa ambaye sasa amemkatisha masomo yake," alidai mahakamani hapo Mwendesha Mashtaka.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alipohojiwa kwa mara ya kwanza kabla ya kufikishwa mahakamani hapo, alikiri kumuoa msichana huyo kwa kuwa alifahamu kuwa ameshamaliza darasa la saba mwaka jana.

Hakimu Mgalamalira aliamuru mshtakiwa arudishwe rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo alimtaka awe na wadhamini wawili wenye mali zisizoweza kuhamishika zenye thamani isiyopungua Sh milioni moja. Shauri hilo limeahirishwa hadi Machi 26, mwaka huu litakapotajwa tena.


Chanzo:Habari leo

ANELKA ATEMWA NA WEST BROM

Ishara aliyofanya anelka ya msanii wa ufaransa M'bala

Mchezaji wa klabu ya soka ya West Brom, Nicolas Anelka amefutwa kazi kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Klabu hiyo iliamua kuchukua hatua hiyo baada ya Anelka kutangaza kupitia mtandao wa kijamii kuwa anaacha kazi.

Anelka alisema kuwa anaondoka katika klabu hiyo baada ya kukosa kutatua tofauti zilizopo kati yake na Albion kuhusu ishara yake yenye utata ambayo inasemekana kuwa ya kibaguzi dhidi ya wayahudi.

Mshambuluaji huyo mwenye umri wa miaka 35, alipigwa marufuku kutocheza mechi tano na kutozwa faini ya pauni 80,000 na shirikisho la soka Uingereza,kwa kufanya ishara hiyo, baada yakuingiza bao dhidi ya klabu ya West Ham mwezi Disemba.

West Brom imechukua hatua ya kumfuta kazi Anelka kutokana na ishara hiyo na pia kwa sababu ya matamshi yake kwenye mtandao wa kijamii.

Awali aliachishwa kazi mwa mudana Albion, wakati klabu hiyo ilipokuwa inafanya uchunguzi wake binafsi.

Mapema siku ya Ijumaa, Anelka alitangaza kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaondoka katika klabu hiyo.

Aliandika: "kufuatia mazungumzo kati yangu na maafisa wa klabu, kuna masharti kadhaa ambayo wamenipa kabla ya kujiunga tena na klabu hiyo, Masharti ambayo siwezi kuyakubali.''

Hata hivyo klabu ilisema kuwa masharti yaliyotolewa kwa Anelka ni pamoja na kumtaka awaombe msahama mashabiki , wadhamini na jamii kwa ujumla kwa athari iliyotokana na ishara yake aliyoifanya Disemba tarehe 28 na pili akubali kutozwa faini.

MARTINEZ KUMRITHI WENGER

Kocha wa Everton, Roberto Martinez ameanza kufikiriwa na wakubwa wa Arsenal kuwa ndiye chaguo sahihi la kumrithi Arsene Wenger.

Martinez, Mhispania aliyeoa mke Mwingereza alijiunga na Everton akitoka Wigan Athletic walioshuka daraja msimu uliopita, lakini anawavutia sana wadau wa Emirateskwa tabia zake uwanjani na hata nje.

Hata jinsi alivyopokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Arsenal wikiendi iliyopita kwa namna ya kipekee akionesha heshima na utulivu badala ya hasira na fujo, kimemwongezea maksi miongoni mwa wakubwa wa Arsenal.

Hata hivyo, kukubalika huko kwa Martinez hakumaanishi kwamba Wenger anaondoka kesho au keshokutwa, hapana. Wenger anakaribia kuanguka saini kwa ajili ya kuendelea kuwanoa Arsenal kwa miaka mingine miwili.

Hata hivyo, wamiliki na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Arsenal wameamua kuanza kufikiria mrithi wa Wenger ili wasikutwe na mshangao wakikosa la kufanya ikitokea siku Wenger kweli anaondoka.

Kwa hiyo wamekuwa wakikuna vichwa juu ya nani angeweza kuwa chaguo lao, na jina la Martinez linashika namba moja kwa sasa, wakipendezwa na aina ya soka analowafundisha vijana wake, pasi kama zile ambazo washabiki wa Arsenal wanazipenda na wamezizoea chini ya Wenger.

Kadhalika Martinez ni muumini wa kuhamasisha kuendeleza ukuzaji vipaji kupitia timu za vijana, falsafa ambayo Arsenal wamekuwa nayo kwa muda mrefu na hata nyota waowengi waliowakimbia walikuwa mazao yao.

RWANDA NA A.KUSINI ZALIPIZANA KISASI

Serikali ya Rwanda imesema hatua ya kuwatimua maafisa sita wa ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ni ya haki na ilizingatia uchokozi ambao ulianzishwa na serikali ya Afrika Kusini yenyewe kwa kufukuza maafisa watatu wa ubalozi wa Rwanda.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ,Bi Louise Mushikiwabo, kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter ameeleza kwamba Rwanda ilikuwa na haki zote kuwafukuza mabalozi wa Afrika Kusini mjini Kigali ikizingatia hatua ambayo nchi hiyo ilianzisha yenyewe kwa kuwatimua maafisa wa ubalozi wa Rwanda mjini Johannesburg.

Katika ujumbe wake mfupi kwenye mtandao huo Bi Mushikiwabo, anailaumu Serikali ya Afrika Kusini kwa kutochukua hatua dhidi ya wanyarwanda waliokimbilia nchini humo ambao serikali ya Rwanda inawatuhumu kuendelea na hujumaza kigaidi dhidi ya Rwanda na kwamba Pretoria haijatekeleza muafaka uliofikiwa awali.

Kulingana na kiongozi huyo kupitia mtandao wa twitter, mahusiano mema kati ya Rwanda na Afrika Kusini yatafikiwa wakati suala la kisheria kuhusu wanyarwanda waliokimbilia nchini humo itapata ufumbuzi.

Wakati haya yakiarifiwa ,mjumbe maalum wa Rais Baracka Obama wa Marekani katika mataifa ya ukanda wa maziwa makuu, Russ Feingold, alisema kuwa Marekani inafuatilia kwa karibu mzozo huo ambao alielezea waandishi kwamba mataifa ya Rwanda na Afrika ya kusini hayana budi kumaliza tofauti zao kwa njia ya kidiplomasia.

Mjumbe huyo alikutana na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukutana na Rais Paul Kagame.

Miongoni mwa wanyarwanda waliokimbilia Afrika ya kusini ni Generali Kayumba Nyamwasa ambaye amekuwa akilaumu utawalawa Rwanda kwa kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi yake ambayo amenusurika.

Kwa upande mwingine Serikali ya Rwanda inakanusha vikali kuhusika na tuhuma hizo.

Kayumba Nyamwasa anajulikana kama mtu aliyetangaza wazi kupiga vita utawala wa Rwanda na anatuhumiwa kuhusika katika mashambulizi ya hapa na pale yanayogharimu maisha ya watu na mali.

WASIWASI WA UDUKUZI FACEBOOK

Mwanzilishi wa Facebook Mark Zuckerberg amesema kuwa amezungumza na Rais Barack Obama kumwelezea kero lake kuhusu udukuzi unaofanywa na serikali kwa mitambo ya Dijital.

Zuckerberg mwenye umri wa miaka 29, amesema kuwa serikali ya Marekani inapaswa kupigia debe internet badala ya kuwa adui wa mitandao ya kijamii.

Matamshi yake yanakuja siku moja baada ya ripoti kuwa shirikala ujasusi la Marekani ilibuni mtandao bandia wa Facebook ili kuweza kuvamia mitambo ya Kompyuta inayotumiwa kwa uchunguzi.

Shirika la NSA lilisema kuwa taarifa hiyo sio ya kweli.

Mnamo mwezi Septemba, Zuckerberg alisema kuwa Marekani ilikosea sana taarifa zilipoibuka kuwa inafaya udukuzi kwenye mitandao.

Mwanateknolojia huyo alisema kuwa huenda ikachukua muda mrefu sana kwa mageuzi yoyote kufanyika.

Zuckerberg alisema, "wakati wahandisi wetu wanapofanya kila hali kuboresha usalama kwenye mtandao, kwetu ni kama tunawalinda kutokana nawahalifu kwenye mitandao, sio serikali yetu.''

"Serikali ya Marekani lazima ipigie debe Internet sio kuwa adui wa mtandao. Lazima waelezee wanachokifanya la sivyo, watu hawatakuwa na imani tena na serikali.''

Shughuli za shirika la ujasusi la Marekani lilijipata motoni baada ya ufichuzi kutolewa na aliyekuwa jasusi wakati mmoja Edward Snowden, mwaka jana.

Ufichuzi wake ulionyesha kuwa shirika hilo lilikuwa linakusanya taarifa za simu za watu, kufanya udukuzi na kuvamia mitandao ya watu.

RWANDA YAHUSISHWA NA UVAMIZI A.KUSINI

Afrika Kusini imewatuhumu wanadiplomasia watatu wa Rwanda waliofurushwa kutoka nchini humo kwa kuhusika na mauaji na njama ya mauaji dhidi ya wapinzani wa serikali ya Rwanda wanaoishi Afrika Kusini.

Waziri wa sheria wa Afrika Kusini, Jeff Radebe amesema kuwa ana ushahidi wa kutosha unaowahusisha watatu hao na vitendo vyinavyokiuka sheria.

Wanadiplomasia hao, walifurushwa siku ya Ijumaa baada ya kutokea uvamizi nyumbani kwa Generali Kayumba Nyamwasa aliyekuwa wakati mmoja mwandani wa Rais Kagame, mjini Johannesburg.

Rwanda ambayo nayo iliwafurushwa wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini kutoka mjiniKigali, imekanusha madai ya kuhusika na njama hiyo.

Msemaji wa Bwana Radebe, Mthunzi Mhaga, aliambia BBC kuwa uchunguzi ulibaini kuwa watatu hao walihusika na uvamizi huo na mashambulizi mengine dhidi ya watu wanaoonekana kuwa wapinzani wa serikali ya Rwanda wanaoishi nchini Afrika Kusini.

Watu waliokuwa wamejihami, walivamia nyumba ya Luteni Generali Nyamwasa, mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda wiki jana lakini hakuwepo nyumbani wakati wa uvamizi huo.

Wavamizi hao walifanya msako ndani ya nyumba hiyo na kuondoka wakiwa wamebeba Komputa na stakabadhi kadhaa.

Generali Nyamwasa ameponea majaribio mawili ya kumuua ikiwemo kupigwa risasi mjini Johannesburg mwaka 2010 baadaya kutoroka Rwanda.

Alitafuta hifadhi nchini Afrika Kusini baada ya uhusiano wake na Kagame kuvunjika.

Januari mwaka huu mwili wa aliyekuwa jasusi mkuu wa Rwanda, Patrick Karegeya, ulipatikana ndani ya hoteli moja mjini Johannesburg akiwa na alama za kunyongwa.

Maafisa wa zamani wa serikali ya Rwanda waliokimbilia usalama wao katika nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza na Marekani wanasema kuwa maafisa wa usalama wa serikali wametishia kuwaua.Muda mfupi baada ya kifo cha Karegeya Rais Kagame alionya kuwa wale ambao wanasaliti nchi hiyo watakiona cha mtema kuni.

Afrika Kusini ilikuwa wakati mmoja mshirika mkubwa wa Afrika Kusini na hata kununua silaha kutoka kwake, lakini uhusiano kati ya nchi hizo umeendelea kuzorota kila kukicha kufuatia mashambulizi dhidi ya waliokuwa maafisa wa Rwanda waliokimbilia nchini humo.

ALIYEKUWA RAIS WA SIERRA LEONE AFARIKI DUNIA

Bwana Kabbah anasifiwa zaidi duniani kwa kurejesha amani nchini Sierra Leone baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Amefariki nyumbani kwake akiwana miaka 82.

Alhaji Ahmad Tejan Kabbah alizaliwa February 16, 1932. Aliongoza Sierra Leone katiya mwaka wa 1996 hadi 1997 na kisha tena mwaka wa 98 hadi mwaka wa 2007.

Katika miaka mingi ya utu uzima wake, alihudumu kama mtaalamu wa uchumi na sheria. Alifanya kazi kwa miaka mingi na shirika la maendeleo la Umoja wa mataifa UNDP. Baada ya kujiuzulu kutoka umoja huo mwaka wa 92, alirudi zake nchini Sierra Leone na kujiingiza katika siasa za nchi hiyo.


*Maisha yake ya siasa

Mnamo mwaka wa tisini na sita, bwana Kabbah alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama Sierra Leone's People's Party (SLPP) na kuwania urais kwa tikiti ya chama hicho mwaka wa 96.

Katika kinyanganyiro hicho, alishinda na kuwa rais kwa 59% ya kura na kumpiku mpinzani wake mkuu John Karefa-Smart wachama cha United National People's Party (UNPP) aliyepata 40% tu ya kura.

Waangalizi wa kimataifa walitangaza kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Kikubwa atakachokumbukwa nacho ni hotuba yake ya kuapishwa mjini Freetown, alipoahidi kumaliza kabisa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, jambo alilotekeleza baada ya kuwa rais.

Bwana Kabbah ni wa kabila la Mandingo kiasilia na ndiye aliyekuwa rais wa kwanza wa kiislamu wa Sierra Leone. Alizaliwa katika kijijji cha Pendembu, wilaya ya Kailahun mashariki mwa Sierra Leone, japo udogoni mwake alikulia mji mkuu wa Free town.


*Utawala wa Kabbah

Sehemu kubwa ya uongozi wa Kabbah ilishawishiwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyotokea nchini Sierra Leone kwa muda mrefu, huku akikumbwa na mapinduzi yamuda yaliyofanywa na wanamgambo wa United Front wakiongozwa na Foday Sankoh. Mapinduzi hayo yalim'ngoa madarakani kati ya Mei 97 hadi March 98.

Hata hivyo alirejeshwa madarakani kufuatia usaidizi wa kijeshi kutoka kikosi cha Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kilichoongozwa na Nigeria.

Awamu ya pili ya machafuko ya ndani na mauaji ilisababisha kuingiliwa na Umoja wa mataifa pamoja na Uingereza nchini humo mwaka wa 2000.


*Harakati za amani

Katika wadhifa wake kama rais, Kabbah alianzisha mazungumzo na wanamgambo hao wa RUF ili kumaliza mapigano hayo ya ndani. Alisaini mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano na kiongozi wa waasi Foday Sankoh, ukiwemo ule mkataba wa mwaka wa 1999 wa mjini Lome' ambapo kwa mara ya kwanza waasi hao walitekeleza na kusitisha kabisa mapigano na mashambulio dhidi ya serikali.

Na pale mkataba huo ulipovunjika baadaye, Kabbah alifanya kampeini kuomba usaidizi kutoka Umoja wa Mataifa, Uingereza, Jumuiya ya ECOWAS na hata Muungano wa Afrika, AU ili kurejesha amani.

Kabbah alitagaza rasmi kumalizika kwa vita vya ndani vya Sierra Leone mwaka wa 2002. Maelfu ya raia wa Sierra Leone walikimbia katika barabara kuu zanchi hiyo kusherehekea hatimaye kupatikana amani.

Miaka michache baadaye Kabbah alipata ushindi wa rahisi sana kuongoza nchi hiyo kwa muhula mwingine wa miaka mitano alipopata 70% ya kura na kumpiku mpinzani wake mkuu Ernest Bai Koroma wa chama cha All People's Congress (APC). Hapopia, waangalizi wa kimataifa walitangaza uchaguzi kuwa huru na wa haki.

WACHINA MIAKA MITANO JELA AU FAINI YA MILIONI MOJA

RAIA wawili wa China wamehukumiwa kifungo cha miakamitano jela au kulipa faini ya Sh milioni moja baada ya kukutwa wakisafirisha meno ya tembo.

Qui Wu (30) na Zou Zhihong (51) ambao walikutwa na meno ya tembo, zilizotengenezwa kama bangili na kinyago.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Janeth Kinyage alisema washitakiwa watatumikia kifungo cha miaka mitano au kulipa faini.

Zhihong aliomba mahakama impunguzie adhabu, kwa kuwa ana matatizo ya moyo na ana familia inamtegemea na mama yake ni mzee.

Mwendesha Mashitaka Nassoro Katuga alidai Februari 23 mwaka huu eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Wilaya ya Ilala, raia hao wa China walikutwa na vipande nane vya bangili, vilivyotengenezwa kwa meno ya tembo vyenye thamani ya Sh 249,600.

Pia, mshitakiwa Zhihong alikutwa na bangili mbili na kinyago, vilivyotengenezwa kwa meno ya tembo yenye kilogramu 0.25 yenye thamani ya Sh 240,000.

JELA MIAKA 10 KWA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imemhukumu mfanyabiashara wa mbuzi, Adam Shaban Hole (46) kwenda jela miaka 10 baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumpa mimba mwanafunzi, kushiriki kumtoa mimba na kusababisha kifo chake.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo, Godlisten Raymond (37) ambaye kwa wakati huo alikuwa tabibu, alipewa adhabu kama hiyo ya miaka 10 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumtoa mimba na kusababisha kifo cha mwanafunzi.

Mwanasheria wa Serikali, Neema Mwanda alidai katika mahakama hiyo, mbele ya Jaji Mfawidhi, Cresentia Makuru kuwa tukio hilo ni la Septemba 7, 2006 katika Zahanati ya Tumaini mjini Singida.

Alidai kuwa Hole, ambaye ni mkaziwa kijiji cha Kintandaa Wilaya ya Ikungi mkoani hapa, alimpa mimba mwanafunzi, Hamida Athuman (16) kisha kushiriki kumtoa hatua iliyosababisha kifo chake.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa darasala saba kwa wakati huo, alifariki siku chache kabla ya kufanya mtihani wake wa kumaliza elimu ya msingi.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mfanyabiashara huyo, ambaye ana mashine ya kusaga nafaka kijijini hapo, katika kipindi hicho hicho, alimpa mimba mwanafunzi mwingine, Rukia Juma aliyekuwa anasoma darasa moja na Hamida.

Ilidaiwa kuwa baada ya kutolewa mimba, Rukia alilazwa Hospitali ya Mkoa wa Singida, ambapo alipatiwa matibabu sahihi na hivyo kuepuka kifo.

Mwendesha Mashitaka, Neema Mwanda aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwao na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Wakili Deus Nyabiri kutoka Dodoma aliyekuwa akimtetea mshitakiwa wa kwanza, Godlisten Raymond aliiomba mahakama impe mteja wake adhabu nafuu, kwa kuwa hilo lilikuwa ni kosa lake la kwanza.

Wakili Raymond Kimu ambaye alikuwa anamtetea Hole, aliiomba mahakama hiyo impe mteja wake adhabu ndogo au imwachie huru, kwa kuwa baada ya kuwapa mimba wanafunzi hao wawili, alikimbiwa na mke na kutengwa na familia yake.

Hata hivyo, Jaji Mfawidhi Makuru alisema katika hukumu yake kuwa kwa mazingira ya kawaida, kosa walililotenda washitakiwa, hawastahili huruma ya mahakama yoyote nchini.

WAZIRI MKUU AZUILIWA KUSAFIRI

Kiongozi wa mashtaka Nchini Libya Abdel-al-Qader Radwan amemzuia Waziri mkuu wa taifa hilo aliyevuliwa madaraka, Ali Zeidan, kusafiri nje ya taifa hilo hadi pale uchunguzi dhidi yake utakapo kamilika.

Anatuhumiwa kwa madai ya ubathirifu wa pesa za umma.

Bwana Zeidan amesimamishwa kazi mapema siku ya Jumanne na Bunge la taifa hilo, baada ya Wabunge kudai kuwa meli ya mzigo ya Korea Kaskazini iliyokuwa imezuiliwa baada ya kunaswa ikibeba mafuta ghafi toka bandari moja linalokaliwana waasi huko Libya, ilivunja nanga na kusafiri baharini.

Kura ya kutokuwa na imani na Bwana Zeidan iliitishwa baada ya meli hiyo iliyokuwa na bendera ya Korea Kaskazini kuabiri na kufikia maji makuu ya mipaka ya kimataifa baharini.

Mafuta hayo yalikuwa yamenunuliwa kutoka kwa waasi wanaodhibiti bandari ya Al- Sidra.


*Wabunge hawana imani na Waziri Mkuu

Bunge la Libya limemuachisha kazi Waziri huyo mkuu, baada ya kupitisha agizo la kutokuwa na imani naye.

Hilo limeafikiwa baada ya meli ya Korea Kaskazini kuingia katika bandari ya taifa hilo na kuondoka na mafuta ghafi bila idhini ya serikali.

Makundi ya wapiganaji yamekuwa yakidhibiti baadhi ya bandari ya taifa hilo mashariki mwa taifa, tangu Julai mwaka jana na kuuza mafuta nje ya taifa.

Mwaandishi wa BBC Rana Jawad anatuarifu kutoka Tripoli.

Bunge la Libya limekuwa likijadiliana namna ya kumtimua Waziri mkuu Ali Zeidan kwa miezi kadhaa sasa.

Wabunge 200 wa taifa hilo walipiga kura na kupata maoni 124 iliyotosha kumuondoa madarakani.


*Serikali ya mpito

Waziri wa sasa wa ulinzi Abdullah Al-Thani amechukua mahala pake kama kama kaimu waziri mkuu.

Anatarajiwa kuhudumu kwa kipindi cha majuma mawili, kuruhusu bunge kukubaliana kumteuwa mridhi wa wadhifa huo.

Chama cha Libya National Congress, tume ya kwanza ya uchaguzi ndio yenye majukumu ya kumteuwa waziri mkuu mpya.

Lakini shinikizo kali limekuwepo Nchini humo la kutaka Bunge livunjwe.

Bwana Zeidan amekuwa akilaumu baadhi ya wanasiasa katika tume hiyo, hasa kutoka ndani ya vyama vya kiislamu ya kutaka kumtimua toka uongozini.

Hatua hiyo ya hivi punde inatazamiwa kuibua maswala mbalimbali ya udhibiti wa uongozi Nchini Libya, inapojikakamua kutafuta uungwaji mkono kutoka pembe zote za Nchi.